Monday, April 4, 2016

UVCCM WATAKIWA KUTUMIA KILIMO KAMA FURSA NA SIO KAMA ADHABU

Na John  Gagarini, Kibaha
VIJANA wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi  CCM (UVCCM) wilayani Kibaha wametakiwa kukitumia kilimo kama moja ya chanzo cha kujikomboa kiuchumi kwani hiyo ni fursa na si adhabu.
Hayo yalisemwa mjini Kibaha na Mjumbe wa Halmashauri Kuu Taifa CCM (MNEC) Rugemalila Rutatina wakati akifungua mkutano wa Baraza la (UVCCM) Kibaha Mjini na kusema kuwa kilimo endapo kitatumia vizuri kinaweza kuboresha uchumi wao badala ya kumtegemea mtu kuwasaidia.
Rutatina alisema kuwa baadhi ya watu wamekuwa wakiwafanya vijana kama ngazi ya kupandia kwa kuwafanikishia mambo yao kisha kuwaacha bila ya kuwajengea mazingira endelevu.
“Uzuri ni kwamba Chama pamoja na umoja wenu una mashamba ambayo ni kama mtaji wa kuanzia kwa ajili ya kilimo cha kisasa ambacho kitakuwa na tija kwa kutumia mipango mbalimbaili ya kuendeleza kilimo ikiwa ni pamoja na Kilimo Kwanza,” alisema Rutatina.
Alisema kuwa ili vijana wajikomboe wanapaswa kuanzisha miradi ya kudumu kupitia rasilimali za chama ambazo endapo zingetumika ipasavyo zingewaondoa vijana ndani ya chama na nje kuwa tegemezi katika kuendesha umoja wao.
“Kilimo ni moja ya njia za kuwakomboa na kuacha kumtegemea mtu lakini endapo mtaanzisha miradi ya kilimo itawaondoa huko mliko na kuwafanya mjitegemee na kuendesha mambo yenu bila kuwa tegemezi,” alisema Rutatina.
Aidha alisema kuwa kwa sasa fursa ni nyingi kwa vijana ikiwa ni pamoja na mikopo kwa ajili kujikwamua kiuchumi na zana za kilimo kama matrekta wanaweza kuazima kwenye chama.
Kwa upande wake katibu wa (UVCCM) Kibaha Mjini David Malecela alisema kuwa wana maeneo mengi ambayo hata hivyo hayajaendelezwa hali ambayo imesababisha watu kuyavamia.
Malecela alisema kuwa kwa sasa wako kwenye mipango ya kuhakikisha wanayamiliki kisheria ili kukabiliana na watu wanaoyavamia maeneo yao ambayo yakiendelezwa yatakuwa ni moja ya vyanzo vikuu vya mapato ya umoja.
Mwisho.

No comments:

Post a Comment