Friday, April 22, 2016

SOKO LA MLANDIZI WALILIA USAFI

Na John Gagarini, Kibaha
WAFANYABIASHARA kwenye soko la Mlandizi Wilayani Kibaha mkoani Pwani wameiomba serikali kuwajengea mitaro kwenye soko hilo ili kuruhusu maji kupita wakati wa mvua kwani soko hilo liko kwenye hali mbaya.
Akizungumza na waandishi wa habari Sauda Said alisema kuwa mvua inaponyesha maji yanajaa na kuwa kero kwa wateja wanaofika kununua bidhaa.
Said alisema kuwa mbali ya kutokuwa na mitaro pia soko hilo lina uchafu mwingi kutokana na kutotolewa kwa kipindi kirefu na kusababisha uchafu huo kutoa harufu kali.
“Changamoto nyingine ni ukosefu wa vifaa vya kufanyia usafi kwani mbali ya kutoa kiasi cha shilingi 200 kila siku kama ushuru usafi haufanyiki ipasavyo hivyo kufanya mazingira ya soko kuwa machafu,” alisema Said.
Alisema kuwa soko hili kwa sasa linazalisha uchafu mwingi sana lakini tatizo ni halmashauri kushindwa kuondoa uchafu kwa wakati na kufanya mlundikano wa uchafu kuwa mkubwa hali ambayo ina hatarisha afya za watumiaji.
Naye mwenyekiti wa soko hilo Thobias Michael alisema kuwa soko hilo ni kubwa kuliko masoko yote mkoani Pwani na linahudumia wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya wilaya za Bagamoyo, Kibaha na Kisarawe lakini mazingira yake si rafiki kwa watumiaji kutokana na uchafu kukithiri.
Michael alisema kuwa waliahidiwa kuwa watajengewa soko la kisasa ili kuondokana na changamoto wa soko hilo kwa sasa kuwa dogo kutokana na kuwa na wafanyabiashara wengi.
“Kwa sasa idadi ya wafanyabiashara ni 450 ni kubwa sana na uzalishaji wa uchafu ni mkubwa sana lakini uzoaji taka unakwenda taratibu sana na vifaa vya kufanyia usafi hakuna kwani hata gari la kuzolea taka hakuna inawabidi Halmashauri kukodisha,” alisema Michael.
Kwa upande wake mganga mkuu wa halmashauri ya wilaya ya Kibaha Dk Mariamu Maliwa alisema kuwa changamoto kubwa iliyopo ni ukosefu wa gari la Halmashauri kwa ajili ya kuzolea uchafu lakini wanakodisha gari kwa ajili ya kuzoa uchafu huo.

Mwisho.

No comments:

Post a Comment