Friday, April 22, 2016

KIBAHA WADHIBITI KIPINDUPINDU

Na John Gagarini, Kibaha
HALMASHAURI ya Wilaya ya Kibaha mkoani Pwani imefanikiwa kuudhibiti ugonjwa wa Kipindupindu eneo la Mlandizi ambao uliolipuka Machi mwaka huu na kusababisha vifo vya watu watatu.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisni kwake mjini Kibaha Dk Mariamu Maliwa alisema kuwa walifanikiwa kuudhibiti kwa kufungia biashara za vyakula ambazo hazikutimiza masharti ya afya.
Dk Maliwa alisema kuwa mgonjwa wa mwisho aliyekuwa amelazwa kwenye kituo cha afya Mlandizi aliruhusiwa Aprili 21na kufanya kutokuwa na mgonjwa Kipindupindu hata mmoja kutoka wagonjwa 115 waliogundulika kuwa na ugonjwa huo kuanzia mwezi Machi mwaka huu.
“Kwa zaidi ya kipindi cha wiki moja tulizuia biashara zote za vyakula pamoja na matunda kwani tuliona kuwa sehemu hizo zilikuwa chanzo cha ugonjwa huo na tulipozifungia wagonjwa walipungua lakini kabla ya kuzifungia kulikuwa kunapatikana wagonjwa hadi nane kwa siku moja hali amabayo ilikuwa ni mbaya sana,” alisema Dk Maliwa.
Alisema kuwa mbali ya kuzuia biashara zote za vyakula pia walikuwa wakitoa elimu juu ya kujikinga na ugonjwa kuhamasisha usafi kwenye maeneo ya biashara, majumbani na sehemu zinazozalisha uchafu kwa wingi, uzoaji taka na kuhamasisha matumizi ya vyoo na kwa wale wasio na vyoo wachimbe vyoo.
“Walikaidi kujenga vyoo tumewapeleka mahakamani kwani wanaonekana kukaidi maagizo hayo kwani kujisaidia holela nako kuna changngia kuenea kwa ugonjwa huu,” alisema Dk Maliwa.
Aidha alisema kuwa wagonjwa hao walitoka kwenye maeneo mbalimbali ya Kibaha na nje ya Kibaha ambapo Ruvu walikuja wagonjwa 63, Mlandizi 27, Visiga na Kongowe 13, Dutumi wanane, Vingunguti na Mbezi wawili, Mzenga mmoja na wale waliokufa mmoja alifia hospitali huku wawili wakifia majumbani.
Alisema kuwa wataruhusu wauzaji wa vyakula mara watakapoona kuna mabadiliko ya ufuataji wa kanuni za afya mara baada ya maofisa wa afya kupita na kujiridhisha kuwa vyanzo vyote vya ugonjwa huo vimedhibitiwa na kuzingatiwa kwa kanuni za usafi na kuwataka wananchi kuweka mazingira yao kwenye hali ya usafi.
Mwisho.

No comments:

Post a Comment