Friday, April 15, 2016

WATUMISHI HEWA WAITIA HASARA SERIKALI KIASI CHA SHILINGI MILIONI 641


Na John Gagarini, Kibaha

MKOA wa Pwani umebaini uwepo wa watumishi hewa 25 wakiwemo walio kufa na wameipa serikali hasara kiasi cha shilingi milioni 641,361,239 kutokana na kupokea mishahara pasipo kufanya kazi ambalo ni kosa kisheria.

Akizungumza na gazeti hili ofisini kwake mjini Kibaha mkuu wa mkoa wa Pwani Injinia Evaristi Ndikilo alisema kuwa hasara hiyo imebainika baada ya kufanya uhakiki kwa mara ya pili na kuona kuwa fedha za mishahara ziliendelea kutolewa kwa watumishi hewa licha ya kutokuwepo kazini.

Ndikilo alisema kuwa kati ya watumishi 19 ni wale waliokufa, waliostaafu na kuacha kazi lakini mishahara yao ilikuwa ikiendelea kutoka na kusababisha hasara hiyo baada ya kuwafanyia uhakiki watumishi 150 ili kuwatafuta watumishi hewa kutokana na agizo la Rais Dk John Magufuli.

“Kundi hili la kwanza limeipa hasara serikali kiasi cha shilingi milioni 69.1 huku wale ambao hawapo kabisa kazini wameipa hasara serikali kiasi cha shilingi milioni 12.4 na watumishi watoro na wale walio na mashauri ya kinidhamu wameipa hasara serikali kiasi cha shilingi milioni 448.2,” alisema Ndikilo.

Alisema kuwa kati ya watumishi 150 waliohakikiwa 31 walibainika kuwa ni watoro na hawakujitokeza siku ya uhakiki lakini walionekana kuwa ni watumishi halali kwa kuonyesha nyaraka muhimu huku 18 wakibainika kuwa ni watoro na wanamashauri ya kinidhamu lakini waliendelea kulipwa mishahara.

“Watumishi 76 ambao ni watoro na wanamashauri ya kinidhamu mishahara yao imesimamishwa ili wasiendee kuitia hasara serikali wakati mashauri yao yanafanyiwa kazi,” alisema Ndikilo

Aidha alisema kuwa wakurugenzi wa Halmashauri saba za wilaya walisema kuwa kiasi cha shilingi milioni 249,452,390  zilirudishwa Hazina na kuwataka wapeleke viambatanisho kama ushahidi vinavyoonyesha kuwa walipeleka hazina na si maneno matupu.

“Kama ni kweli kiasi hicho cha fedha kilipelekwa hazina fedha ziltakazokuwa zimepotea ni kiasi cha zaidi ya shilingi milioni 391.8 ambazo wanapaswa kuonyesha vielelezo vya kuzipeleka hazina kwani maelezo hayo bado hayajaturidhisha wanatakiwa watupe uthibitisho ili tuliamini hilo,” alisema Ndikilo.     


Mwisho.

No comments:

Post a Comment