Na John Gagarini, Kibaha
BAADHI ya wakazi wa Kitongoji cha Vinziko Kijiji cha Kikongo
wilayani Kibaha mkoani Pwani wameitaka Halmashauri ya wilaya kutowaondoa kwenye
eneo ambalo wanaishi kwani hawana pa kwenda.
Serikali iliwapa siku 60 wawe wameondoka kwenye eneo hilo
ambalo lilikuwa chini ya kampuni ya United Framing Cooperation (UFC) ambao
walishindwa kuliendesha na kuwa shamba pori kabla ya serikali haijalifutia hati
Mei 28 mwaka 2015.
Moja ya wakazi wa eneo hilo Athuman Fundi (90) alisema kuwa
wao wako hapo muda mrefu tangu operesheni vijiji ambapo walihamishwa toka
maeneo ya mbali na kupelekwa maeneo ambayo yalikuwa karibu na huduma za
kijamii.
“Sisi tulifikiri ni vema wakatuacha kwenye maeneo yetu haya
na si kutuondoa kwani hatuna pa kwenda na sisi hapa tumeshawekeza kwa kujenga
makazi ya kudumu leo wakituambia tuondoke tutakwenda wapi vinginevyo watulipe
ili tukatafute sehemu nyingine au watupatie maeneo mengine,” alisema Fundi.
Fundi alisema kuwa mbali ya kutakiwa kuondoka pia vyombo vya
dola vimekuwa vikitumia nguvu kubwa kutaka wao waondoke ambapo wenzao wamekuwa
wakikamatwa kutokana na mgogoro huo ambao umewanyima raha.
“Tunaomba tusaidiwe na Waziri wa Ardhi Nyumba na Makazi ili
tupate haki yetu kwani wao kututaka tuondoke bila ya kutupa chochote au
kutotupa maeneo mengine tunaona kama hatujatendewa haki kwani tuna nyumba zetu,
mazao ambavyo vimo humo leo wanatuambia tuviondoe tutaishi wapi,” alisema
Fundi.
Kwa upande wake Sabina Benedict alisema kuwa wamekuwa
wakiteseka sana kutokana na mgogoro huo kwani wazee na vijana wamekuwa
wakikamatwa na polisi na kuwekwa rumande hivyo kuishi kwa woga.
Benedict alisema kuwa tatizo kubwa linatokana na viongozi
ambao wanataka kumuuzia mwekezaji ambaye anatumia kila njia kuhakikisha wao
wanaondoka ili alipate eneo hilo kirahisi.
Naye mwenyekiti wa Kijiji cha Kikongo Sultan Ngandi alisema
kuwa shamba hilo lenye ukubwa wa hekta 3,285 lilikuwa likimilikiwa na kampuni
hiyo ya UFC ambayo ilikuwa ikilima mazao mbalimbali kama vile Pamba, Mbaazi,
Alizeti na mazao mengine ilishindwa kuliendeleza na kuliacha pori ambalo
lilikuwa likitumiwa na wahalifu kuzuru watu.
Ngandi alisema kuwa wananchi waliomba kulima ikiwa ni pamoja
na Umoja wa wakulima wa Ondoa Njaa Kikongo (ONJAKI) lakini walitakiwa wasilime
mazao ya kudumu wala kujenga nyumba za kudumu badala yake walime mazao ya muda
mfupi.
“Hata hivyo baadhi ya watu walikiuka makubaliano na wengine
walianza kujenga nyumba za kudumu, mazao ya muda mrefu na hata wengine
walifikia hatua ya kuayauza kienyeji baadhi ya maeneo nao kuondoka na kuwaacha
watu ambao ndiyo wanaolalamika,” aisema Ngandi.
Akizungumzia suala hilo mkuu wa wilaya ya Kibaha Halima Kihemba
alisema kuwa ni kweli wametoa siku 60 kwa watu walioko kwenye eneo hilo kwani
wamevamia na hawakutakiwa kuwa kwenye neo hilo kwani liko chini ya serikali.
Kihemba alisema kuwa hilo ni moja ya mashamba 16 ambayo
yalifutiwa hati na kwa sasa wanaendelea na mchakato wa kulitengea matumizi na
waliwataka watu walioko kwenye eneo hilo wapeleke vielelezo vya kuonyesha
walipataje maeneo hayo na kusema si kweli kwamba kuna mwekezaji wanataka kumpa
eneo hilo.
Aidha alisema kuwa hadi sasa watu zaidi ya 100 wamepeleka
vielelezo vyao nab ado wanawasubiri watu wengine ambao wako wengi ili wapeleke
vielelezo vyao ili serikali iangalie namna ya kuwasaidia na kuwataka watu hao
waondoke kwenye eneo hilo.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment