Friday, April 22, 2016

KEC SACCOS YAKOPESHA WANACHAMA WAKE MABILIONI YA FEDHA

Na John Gagarini, Kibaha
CHAMA cha Ushirika wa Mikopo cha Shirika la Elimu Kibaha (KEC SACCOS LTD) kimeweza kutoa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 1.3 kwa wanachama wake kwa kipindi cha mwaka mmoja uliopita.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mwenyekiti wa Ushirika huo Kachingwe Kaselenge alisema kuwa mtaji wao kwa sasa umefikia zaidi ya Bilioni 2.
Kaselenge alisema kuwa kwa sasa akiba ndani ya chama imefikia bilioni 1.7 hisa zikiwa ni shilingi milioni 213.9 na mkopo ni bilioni 2.2 ambapo kwa kila mwezi wanatoa mikopo yenye thamani ya shilingi milioni 190.
“Tunamshukuru Mungu kwa sasa chama kinaendelea vizuri kwani marejesho ni asilimia 98 hadi 99 ni wanachama wachache tu ambao wanarejesha kwa matatizo nah ii inatokana na kuwa na mikopo sehemu nyingine kwani sheria inasema mtumishi anapokopa lazima ibaki asilimia 1/3 ya mshahara wake,” alisema Kaselenge.
Alisema kuwa wanachama wao ni watumishi wa Shirika hilo lakini kutokana na kuwa na uwezo mkubwa wameongeza wanachama ambao ni wafanyakazi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha (KDC) na wale wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha (KTC) pamoja na wafanyakazi waofisi ya mkuu wa mkoa.
“Chama chetu ni moja ya vyama vikongwe hapa nchini kwani kwa mwaka huu kinatimiza miaka 50 tangu kunzishwa kwake na tunajivunia mafanikio makubwa tuliyoyapata tangu kuanzishwa kwake kwani wanachama wameweza kunufaika na mikopo inayotolewa kwani zaidi ya watu 5,040 wananufaika kwa siku na mikopo hii kwani wanachama wana miradi mbalimbali kama ya mabasi, shule, ufugaji bodaboda na shughuli nyingine za kimaendeleo,” alisema Kaselenge.
Aidha alisema kuwa mtaji walio nao ni wa ndani kwani hawakopi kwenye mabenki kama baadhi ya vyama vinavyofanya hivyo hawana deni lolote wale mkopo kwenye taasisi za kifedha ambapo hubidi kuweka riba kubwa ili kufidia mikopo kwani kutokana na kuwa na mtaji wa ndani riba yao ni asilimia 1.6.
“Kuna mikopo ya aina mbalimbali ikiwa ni pamoja na ile ya Dharura kama vile misiba na majanga mbalimbali, Maendeleo ikiwa ni pamoja na ujuenzi wa nyumba usafiri na ufugaji, Elimu kusoma na kusomesha na mwanachama anapofariki familia inalipwa 300,000 na kama ni mwenza wake analipwa 200,000 kwani asilimia moja ni bima ya mkopo na endapo anafariki deni linakufa na fedha zake watalipwa ndugu bila ya kukatwa chochote kwani bima itakuwa inalinda mkopo huo,” alisema Kaselenge.
Alibainisha kuwa wanakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwa ni pamoja na kuwa na ushindani mkubwa toka kwenye taasisi za kifedha ambazo zinawashawishi wanachama wao kujiunga nao kwa kuwalipia madeni wanayodaiwa kwenye chama, sheria kutaka vyama hivyo kutolipa kodi lakini wanaaambiwa walipe kodi na mwanachama anauwezo wa kukopa mara tatu ya akiba yake aliyojiwekea kati ya shilingi milioni moja hadi milioni zaidi ya 20.
Ushirika huo ulianzishwa mwaka 1966 ukiwa na wanachama ukiwa na wanachama 66 lakini kwa sasa una wanachama 840 na kilianzishwa kwa ajili ya  kusaidiana na kusaidia jamii inayowazunguka kwa kujitolea misaada sehemu mbalimbali kama hospitali na maeneo yenye uhitaji.
Mwisho.

No comments:

Post a Comment