Na John Gagarini, Kibaha
KATIKA kuunga mkono dhamira ya Rais Dk John Magufuli ya
uchumi wa nchi kutegemea viwanda kampuni ya Kilua Steel inatarajia kuanza
uzalishaji wa bidhaa za vyuma zikiwemo nondo pamoja na vyuma mbalimbali ifikapo
mwezi Mei mwaka huu.
Uzalishaji wa vyuma kwenye kiwanda hicho utapunguza bei ya
bidhaa za vyuma kwa asilimia 25 ya bidhaa hizo ambazo nyingi zinaagizwa toka
nje ya nchi hivyo kuongeza mapato ya ndani.
Akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea kiwanda
hicho kilichopo Kitongoji cha Disunyala Mlandizi wilayani Kibaha mkoani Pwani mkurugenzi
wa kiwanda hicho Mohamed Kilua alisema kuwa kiko kwenye hatua za mwisho za
kuunganisha umeme mkubwa wa viwandani kwani uliopo ni mdogo na hauwezi
kuendesha mashine za kiwanda hicho.
Kilua alisema kuwa kiwanda hicho ambacho kitakuwa ni cha
kipekee hapa nchini na barani Afrika kitakuwa na uwezo wa kuzalisha tani
milioni 1.5 kwa mwaka huku kwa siku kikitarajiwa kuzalisha tani 2,000 kwa awamu
ya kwanza na kufikia tani 7,000 itakapofikia awamu ya tatu na itatoa ajira kwa
watu zaidi ya 2,000.
“Tunatarajia kuzalisha vyuma vyenye ubora wa kimataifa ili
viweze kuwa na soko sehemu yoyote ile duniani kwani tuna wataalamu kutoka nchi
ya China ambao ndiyo tunaoshirikiana nao hapa,” alisema Kilua.
Alisema kuwa tayari malighafi za kutengenezea vyuma wanazo
ambazo zinatoka nchi kama vile Brazil na nchi zinazotengeneza vyuma duniani
lakini mara kitakapoanza kazi kitakuwa na malighafi zake.
“Tunarajia malighafi zote mara tutakapoanza uzalishaji
zitapatikana hapa hapa hivyo bei ya vyuma itashuka na nchi itapata maendeleo
kupitia kodi mbalimbali kwenye kiwanda,” alisemaKilua.
Aidha alisema kuwa vyuma vitakavyozalishwa hapo mbali ya
nondo ni pamoja na vyuma vinavyo husika na ujenzi wa madaraja makubwa, mabomba
yatakayotumia gesi, maghorofa kufikia urefu wa ghorofa 50 na kuendelea na vyuma
vya engo tofautitofauti ambavyo vitapatikana na kuwapunguzia gharama wananchi
katika shughuli zao zinazohitaji vyuma.
Kwa upande wake mkurunzi mwenza kutoka nchni China Wang Zuojin
alisema kuwa aliamua kushirikiana na Kilua ikiwa ni moja ya njia za kuenzi
urafiki wa nchi hizo ambao ulianzishwa na Mwalimu Julius Nyerere zaidi ya miaka
50 iliyopita.
Zuojin alisema kuwa nchi ya China miaka mingi iliyopita ya
nyuma ilikuwa maskini lakini walijipanga hasa kupitia viwanda na kuifanya nchi
hiyo kuwa yenye uchumi mkubwa duniani kupitia viwanda.
“Rais Dk John Magufuli ni mtu anayependa maendeleo na
tumeamua kumuunga mkono kwa sera zake za kuinua uchumi wa wananchi wake kwa
kuendeleza sekta ya viwanda ili kuwa na uchumi wa kati kwa kufanya mapinduzi ya
viwanda,” alisema Zuojin.
Alisema kuwa anachokisema Dk Magufuli kinawezekana kwani hata
China ilikuwa chini kiuchumi lakini walipoamua kuwekeza kwenye viwanda
wamefanikiwa na kuwa nchi zenye uchumi mkubwa duniani na kuwaondoa wananchi
wake kwenye umaskini.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment