Na John Gagarini, Kibaha
MADEREVA wa mabasi ya abiria
yanayotoa huduma wilayani Kibaha yanayotokea Mbezi na Ubungo Jijini Dar es
Salaam watakaokatisha ruti watafikishwa mahakamani badala ya kupigwa faini.
Akizungumza na gazeti hili Ofisa
Mfawidhi wa Mamlaka ya Usafirishaji Majini na Nchi Kavu (SUMATRA) mkoani Pwani
Nashon Iroga alisema kuwa wamefikia maamuzi hayo baada ya madereva hao kudharau
faini hizo na kulipa kwa urahisi.
Iroga alisema kuwa wamiliki wa mabasi
hayo maarufu kama Daladala wamekuwa wakilipa faini na kuendelea kukatisha ruti
hivyo kuwapa usumbufu abiria wanokwenda maeneo mbalimbali.
“Madereva hawa wamekuwa kama sugu
licha ya kupigwa faini lakini wanalipa kwani wanaona kama ni afadhili kulipa
faini na kukatisha ruti kuliko kuwafikisha abiria kule waendako,” alisema
Iroga.
Alisema kuwa abiria wengi wanaokwenda
maeneo ya Chalinze, Mkata, Msata na Mlandizi wamekuwa wakilalamika kuwa
madereva hao hukatisha ruti na kugeuzia Kongowe kwa madai kuwa abirai wanaobaki
ni wacheche hivyo wanapta hasara kuwapeleka maeneo hayo.
“Utakuta basi limetokea Ubungo au
Mbezi na leseni yake inaonyesha linakwenda mfano Chalinze, Mkata, Msata na Mlandizi akianza safari anakuwa na abiria
wa kutosha lakini njiani abiria wanashuka hivyo wakifika Kongowe wanageuza wakidai
kuwa abiria ni wachache hivyo hawapatia faida ndiyo wanakatisha ruti,” alisema
Iroga.
Naye Kamanda wa Kikosi cha Usalama
Barabarani mkoa wa Pwani (RTO) Abdi Isango alisema kuwa hadi juzi madereva sita
walipandishwa kizimbani kutokana na kukatisha ruti hizo.
Isango alisema kuwa wao waliomba
leseni kufika hayo maeneo ambayo yametajwa na yameandikwa kabisa lakini
hawawafikishi abiria kule walikosema na wamekuwa wakiwafaulisha kwenye mabasi
mengine.
“Tumeona ili kukomesha tabia hiyo ya
kukatisha ruti ni kuwapeleka mahakamani madereva wao wenyewe kwani faini
wanaidharau na kulipa lakini kwa sasa ni kuwafikisha mahakamani tumeona njia
hii itasaidia kwani faini ya shilingi 30,000 au ile ya 250,000 ya SUMATRA zimekuwa
zikilipwa na wamiliki wao,” alisema Isango.
Alisema kuwa madereva 25 wanatafutwa
baada ya kutenda kosa hilo na kukimbia huku wawili wakiyaacha magari na
kukimbia lakini bado wanatafutwa na mara watakapokamatwa watafikishwa mahakani
kujibu tuhuma zinazowakabili.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment