Friday, April 1, 2016

SELEMAN TALL ATWAA MKANDA WA TPBO

Na John Gagarini, Kibaha
BONDIA Said Seleman maarufu kama Tall juzi usiku alitwaa ubingwa wa taifa wa ngumi uzito wa kati kupitia shirikisho la ngumi la TPBO baada ya kumshinda kwa pointi Ambokile Chusa.
Pambano hilo ambalo lilipigwa kwenye ukumbi wa Container wilayani Kibaha mkoani Pwani lilikuwa la vuta ni kuvute kutokana na umahiri wa mabondia hao ambao hata hivyo walikuwa wakicheza kwa kuogopana kwa hofu ya kupoteza ushindi.
Hata hivyo Tall alikuwa mjanja na kumzidi mbinu mpinzani wake ambaye muda mwingi alikuwa akijihami kwa kuficha uso ili kukwepa ngumi kali zilizokuwa zikirushwa na mpinzani wake.
Kwenye mapambano mengine Yasini Said alimpiga Julius Jackson, Emanuel Endrew alimpiga Ramadhan Keshi, Ramadhan Kamage alimtwanga Kassim Chuma, Salehe Muntari alimtwanga Aziz Pendeza, Hassan Mgosi alimtwanga Hemed Hemed, Said Chino alimtwanga Idd Mgwinyo kwa TKO, huku Alfred Masinda na Nurdin Mijibwa na Abdala Luwanje na Rajabu Mbena walitoka sare.
Akikabidhi mkanda huo kutoka TPBO mgeni rasmi katika pambano hilo Selina Wilson Diwani wa Viti Maalumu aliwapongeza waandaaji wa pambano hilo Butamanya Promotion kwa kuleta shindano hilo Kibaha.
Wilson alisema kuwa kuleta mchezo huo Kibaha ni kuibua vipaji vilivyopo mikoani na kuwapa uzoefu mabondia wa hapa kuweza kujifunza mbinu za ngumi.
“Mimi ni kijana na nimeona jinsi gani watu wanavyopenda mchezo huu hapa Kibaha na mkoa wa Pwani nitahakikisha naunga mkono mchezo huu na kupeleka halamashauri changamoto zinazowakabili ili ziweze kufanyiwa kazi kwa lengo la kuboresha mchezo huu,” alisema Wilson.
Kwa upande wake bondia wa zamani Habibu Kinyogoli alisema kuwa mabondia wa mkoa wa Pwani wameonyesha uwezo lakini walichokosa ni mbinu za mapigano hivyo atajitolea kuwafundisha mabondia wa mkoa wa Pwani.

Mwisho.

No comments:

Post a Comment