Wednesday, March 30, 2016

MABONDIA KUWANIA MKANDA TPBO KIBAHA

Na John Gagarini, Kibaha
MABONDIA Said Seleman Ambokile Chusa wajijini Dar es Salaam leo wanatarajia kupambana kwenye pambano la ngumi la kuwania ubingwa TPBO uzito wa kati pambano litakalo pigwa kwenye ukumbi wa Container Maili Moja wilayani Kibaha mkoani Pwani.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Kibaha moja ya wasimamizi wa pambano hilo ambaye ni mwalimu wa ngumi Gordon Tambwe maarufu kama Mawe alisema kuwa pambano hilo litakuwa kali na la kuvutia.
Mawe alisema kuwa lengo la kufanya pambano hilo Kibaha ni kuhamasisha mchezo huo mikoani pia kuinua vipaji kwa mabondia wa mikoani ili nao waweze kuonyesha uwezo wao.
“Tumeleta pambano hili Kibaha ili kuhamasisha mchezo wa ngumi sehemu mbalimbali mikoani kwani michezo ni ajira na ngumi zimewasaidia vijana wengi kujiajiri kupitia mchezo huo,” alisema Mawe.
Aidha alisema kuwa mabondia hao watapigana raundi 10 na pia kutakuwa na mapambano ya utangulizi ambayo yatausisha mabondia kutoka mkoa wa Pwani na wageni wao kutoka Jijini Dar es Salaam.
Kwa upande wake Seleman alisema kuwa amejiandaa ipasavyo na anatarajia kummaliza mapema mpinzani wake kwa KO kwani hatakuwa na muda wa kupoteza katika kumaliza pambano hilo.
Naye Chusa alisema kuwa amekwenda Kibaha kwa ajili ya kutafuta ubingwa na si kutalii na anatarajia kumpiga mpinzani wake ili kuwapa raha wapenzi wake hivyo wasiwe na wasiwasi. Mgeni rasmi anatarajiwa kuwa diwani wa Viti maalumu Selina Wilson.

Mwisho.

No comments:

Post a Comment