Friday, March 4, 2016

ALBINO APOTEA

Na John Gagarini, Mkuranga
KIJANA mwenye ulemavu wa ngozi Albino Said Abdala mkazi wa Kijiji cha Mbezi Mlungwana kata ya Pazuo wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani amepotea tangu Januari 31 mwaka huu na hajulikani alipo baada ya kwenda kutembea nyakati za usiku.
Abdala ambaye alikuwa akiishi na wenzake wawili wenye ulemavu huo akitokea mkoani Morogoro huku wenzake Tabora kwa lengo la kuepuka vitendo vya kushambuliwa na watu ambao wamekuwa wakiwa kata viungo au kuwaua hali iliyowafanya wakae huko chini ya Shirika la Under The Same Sun.
Akizungumza mbele ya mkuu wa mkoa wa Pwani Injinia Evarist Ndikilo, Samwel Masaga alisema kuwa mwenzao aliondoka siku hiyo majira ya jioni kwenda kutembea lakini hakurudi tena hadi wakati anatembelea mkuu huyo.
Masaga alisema kuwa mwenzao alikuwa na tabia ya kutoka na kutembetembea lakini wanashangaa ni kwa nini hajarudi na jitihada za kumtafuta zimeshindikana licha ya kutoa taarifa sehemu mbalimbali ikiwa ni pamoja na polisi na ofisi ya mkuu wa wilaya.
“Tunasikitika kupotea kwa mwenzetu na hatuji tutampataje tunaomba vyombo vinavyohusika vitusaidie ili mwenzetu aweze kupatikana kwani hatujui mwenzetu nini kimemsibu kwani ni muda mrefu umepita hakuna taarifa yoyote juu yake,” alisema Masaga.
Alisema kuwa mazingira wanayosihi kwa bahati mbaya hayana ulinzi wowote lakini wamekuwa wakiishi vizuri na wenyeji wao ambao waliwapokea vizuri na wamekuwa wakiishi vizuri bila ya matatizo ila hawajui mwenzao yuko wapi.
Kwa upande wake mwenyekiti wa Kijiji hicho Hassan Kafeni alisema kuwa walemavu hao wako hapo tangu mwaka 2014 na ni wa awamu ya pili baada ya awamu ya kwanza kukaa hapo kisha kuondoka ndipo walipoombewa hao wakae hapo ili nao waishi kama wanakijiji.
Kafeni alisema kuwa Abdala tangu alipopotea walifanya jitihada za kumtafuta lakini hata hivyo hawajamwona na bado wanaendelea kumtafuta hadi watakapompata na wameshangazwa na tukio la kupotea kwake.
Kutokana na hali hiyo mkuu wa mkoa wa Pwani injinia Evarist Ndikilo alisema kuwa shirika hilo linapaswa kuangalia upya namna ya kuwatunza watu hao kwani mazingira waliyopo usalama wake ni mdogo.
Ndikilo alisema kuwa shirika hilo linaonyesha lina nia nzuri lakini mazingira waliyopo si salama sana kwani hakuna ulinzi wa kutosha hali ambayo imesababisha Abdala kupotea na kuwataka kuwahamishia sehemu nyingine.
“Nawashauri wawatafutie sehemu nyingine ya kuishi kwani pale walipo hakuna usalama kwani kama mtu anania mbaya ni rahisi kuwazuru kwani serikali inataka waishi kwenye mazingira yenye usalama wa maisha yao,” alisema Ndikilo.
Kamanda wa Polisi mkoani Pwani Bonaventura Mushongi alisema kuwa Jeshi hilo linaendelea na msako wa kumtafuta Abdala na watahakikisha wanamtafuta hadi wanampata ili aungane na wenzake waishi kama kawaida.
Mushongi alisema kuwa ushirikiano na wananchi utasaidia kupatikana kwake hivyo watoe ushirikiano ili kufanikisha Abdala kupatikana kwani jambo hilo si la kawaida kutokea na kuwataka wananchi kuwalinda Albino kwani nao wana haki ya kuishi.
Mwisho.           


No comments:

Post a Comment