Na John Gagarini, Kibaha
MTU mmoja amefariki dunia wilayani Kibaha mkoani Pwani kutokana
na ugonjwa wa Kipindupindu huku wengine 10 wakiwa wanaugua ugonjwa huo kwenye hospitali
mbalimbali wilayani humo.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Kibaha Ofisa afya wa
mkoa wa Pwani Simon Malulu alisema kuwa ugonjwa huo uligundulika Aprili 17
mwaka huu katika Shule ya Sekondari ya Ruvu wilayani Kibaha.
Malulu alisema kuwa ugonjwa huo uliwakumba wanafunzi 21 wa
shule hiyo ambapo awali waliona kuwa ni mchafuko wa matumbo kwani wanafunzi hao
walikuwa wakiharisha.
“Baada ya kuona hali imezidi kuwa mbaya kwa wanafunzi walimu
waliwapeleka wanafunzi kwenye Zahanati ya Kijiji cha hicho cha Ruvu Station na
kuchukua sampuli ya kinyesi kwa wanafunzi tisa ambapo mmoja aligundulika kuwa
na ugonjwa huo,” alisema Malulu.
Alisema kuwa baada ya kubaini hilo ilibidi mkuu wa wilaya
aifunge shule hiyo ili kuwaepusha wanafunzi zaidi kuambukizwa ugonjwa huo ambapo
wanafunzi waliokumbwa na ugonjwa huo wengi walikuwa ni wanafunzi wakike ambao
wako bweni.
“Hadi sasa kwenye Zahanati ya Ruvu kuna wagonjwa wanne,
Zahanati ya Dutumi watatu na Mlandizi wako watatu ambao wanendelea kupatiwa
matibabu ya ugonjwa huo,” alisema Malulu.
Aidha alisema kuwa chanzo cha kuenea ugonjwa huo ni kinyesi
ambacho kinatokana na watu wengi kujisaidia kwenye Mto Ruvu ambapo maji yake
wanafunzi na wananchi wa Kijiji cha Ruvu Station.
“Tumechukua hatua za kufungua kambi kwenye maeneo yote yenye
ugonjwa ikiwa ni pamoja na Ruvu Station, Dutumi na Mlandizi pia kuwaptia dawa
ya kusafishia maji ili kutibu maji hayo ambayo wananchi wamekuwa wakiyatumia
bila ya kuyachemsha,” alisema Malulu.
Aliongeza kuwa wananchi wanatakiwa kutumia vyoo pia wanatoa
elimu ya jisni ya kujikinga na ugonjwa huo na kufanya ukaguzi wa taasisi za umma, shule, nyumba za
watumishi kuzuia upikwaji wa vyakula na uuzaji wa vinywaji na kuweka mazingira
katika hali ya usafi.
Ugonjwa huo mwaka jana Agosti ulitokea mkoani Pwani na kuisha
Desemba ambapo 293 waliambukizwa huku 98 walibainika kuwa na ugonjwa huo huku
watu watatu walipoteza maisha.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment