Thursday, March 10, 2016

DIWANI AKUMBWA NA BOMOBOMOA KIBAHA


Na John Gagarini, Kibaha
ZOEZI la bomoa bomoa kwa watu waliojenga kwenye hifadhi ya barabara ya Morogoro lililoanza Machi 8 mwaka huu wilayani Kibaha mkoani Pwani limemkumba diwani wa kata ya Sofu Yusuph Mbonde ambaye alijenga chumba cha biashara kwenye  eneo la Picha ya Ndege naye amekumbwa na kadhia hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari kwenye eneo hilo diwani huyo alisema kuwa yeye naye alikuwa akifanya biashara ya kujipatia riziki yake hapo na alijua bomoa bomoa hiyo ilikuwa ni kwenye barabara mpya lakini akashangaa zoezi hilo kupita hadi barabara ya zamani.
“Zoezi hili limeathiri watu wengi na wote tuliojenga hapa na kufanyabiashara hapa tulipewa taarifa ya kubomoa lakini nilijaribu kumwomba meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kutuongezea muda lakini alisema watu wabomoe ambapo walitoa muda wa kubomoa na watu wengi hawakuamini kama watabomolewa kwani taarifa zilikuwa zikitolewa bila utekelezaji,” alisema Mbonde.
Alisema eneo ambalo limebomolewa ni zaidi ya wafanyabiashara 200 ambako ni pamoja na eneo la soko na maduka ya kuuza bidhaa mbalimbali pamoja na nyumba za makazi ya watu wanaokadiriwa kufikia zaidi ya 1,000 kwa mitaa miwili ya Picha ya Ndege na Msufini ambayo ina wakazi 13,000.
“TANROADS iliwataka watu wanaotumia eneo la hifadhi ya barabara kutojenga vibanda vya kudumu lakini watu walijenga vibanda vya kudumu pamoja na nyumba kama siyo sehemu ya muda tunakubaliana na serikali hatuna jinsi tutatafuta eneo mbadala kwa ajili ya kufanya biashara,” alisema Mbonde.
 Naye Zakia Yusuph alisema kuwa zoezi hilo limewaathiri sana hasa akinamama ambao walikuwa wakiendesha biashara zao za kujipatia kipato ambapo wengine ni wajane na wana watoto ambao wanasoma.
Yusph alisema kuwa yeye yeye alikopa mkopo benki wa shilingi milioni tano na hajui atazirudisha vipi na kuiomba serikali kuwapatia eneo lingine kwa ajili ya kufanyia biashara zao za kuwapatia kipato cha kuendeshea familia zao.
Kwa upande wake meneja wa TANROADS Tumaini Sarakikya alisema kuwa zoezi hilo la bomoabomoa litadumu kwa kipindi cha siku 15 ambapo wataondoa nyumba zote zilizojengwa kwenye hifadhi ya barabara zilizo ndani ya mita 22.5 kila upande wa barabara kwa sheria ya barabara ya mwaka 1930 baada ya kutoa notisi za mara kwa mara.
Sarakikya alisema kuwa zoezi hilo ni la kudumu na litafanyika kwenye barabara zote zilizochini ya wakala kwenye wilaya za mkoa huo ambapo kwa njia ya Morogoro zoezi hilo litaenda hadi Bwawani mpakani mwa mikoa ya Pwani na Morogoro.
“Barabara ya Tanga watatekeleza zoezi hilo hadi eneo la Manga mpakani mwa mikoa hiyo huku kwa upande wa Bagamoyo litafanyika hadi Bunju mpakani mwa Pwani na Dar es Salaam na Kongowe hadi Marendego kwa barabara iendayo mikoa ya Kusini,” alisema Sarakikya.
Akizungumzia kuhusu eneo la Maili Moja ambako ndiyo makao makuu ya mkoa wa Pwani amesema kuwa eneo hilo litakuwa la mwisho kutokana na halmashauri kuomba hadi pale watakapojenga Stendi na soko ambavyo ndiyo chanzo kikuu cha mapato ya Halmashauri hiyo lakini mara ujenzi huo utakapokamilika watabomoa ndani ya mita 100 kila upande.

Mwisho.

No comments:

Post a Comment