Na John Gagarini, Bagamoyo
CHUO cha Kilimo na Mifugo Kaole wilayani Bagamoyo kinachomilikiwa
na Jumuiya ya wazazi Tanzania kinakabiliwa na upungufu wa madawa ya kujifunzia
kwenye maabara pamoja na zana za kujifunzia hali ambayo inasababisha wanachuo
kushindwa kujifunza kikamilifu.
Hayo yalisemwa Bagamoyo na Rais wa Chuo hicho Abas Kasusumo
wakati wa ziara iliyofanywa na Jumuiya ya Wazazi wilaya ya Bagamoyo ambao
walitembelewa na Jumuiya hiyo wilaya ya Temeke kuangalia shughuli zinazofanywa
na Jumuiya hiyo.
Kasusumo alisema kuwa changamoto hizo zinawasababisha
washindwe kujifunza ipasavyo hali ambayo inawafanya wawe katika wakati mgumu
kuelewa masomo yao.
“Tunaomba tusaidiwe vifaa vya kujifunzia kama vile matrekta ambayo
hapa yapo lakini hayafanyi kazi hivyo tunaiomba serikali na Jumuiya ambayo
ndiyo wamiliki wa chuo chetu ili tupate vifaa vya kujifunzia,” alisema Kasusumo.
Alisema kuwa kutokana na chuo hichi kuwa cha mifugo pia kuna
changamoto ya ukosefu wa madawa mbalimbali kwa ajili ya kujifunzia masomo yetu
kwani wakitoka hapo watategemewa kufanya kazi kutokana na walivyojifunza.
Kwa upande wake mwalimu mkuu wa chuo hicho Carthert Liwa
alisema kuwa changamoto nyingine ni umeme ambapo wanatumia mita ya Luku ambayo
haiwezi kumudu matumizi makubwa.
Liwa alisema kuwa changamoto zimekuwa nyingi kwani chuo hicho
kimeanza upya baada ya kutokea matatizo hivyo wadau wanaombwa kujitokeza
kukisaidia ili kiweze kutoa mafunzo kwa viwango vinavyotakiwa.
Naye mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi wilaya ya Bagamoyo ambao
ndiyo wamiliki wa chuo hicho Abdul Sharif alisema kuwa watahakikisha
wanshirikiana na wadau wengine ili kuhakikisha kinatoa mafunzo kwa ubora.
Sharif alisema kuwa changamoto zilizotajwa ni za kweli na
Jumuiya kwa kushirikiana na makao makuu watazifanyia kazi changamoto hizo ili
elimu bora iweze kupatikana chuoni hapo. Chuo hicho kina wanafunzi 36 lakini
uwezo wake ni wanachuo 600 ambapo hali hiyo ilitokana na kuchelewa kuandikisha
wanachuo.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment