Na John Gagarini, Mkuranga
MKUU wa Mkoa wa Pwani Injinia Evarist Ndikilo ametoa siku
tatu kwa Jeshi la Polisi mkoani humo kuwakamata watu wanaojihusisha na vitendo
vya kuwavamia kisha kuwapora viwanja na kufanya mauji kwa wakazi wa Kijiji cha
Tambani kata ya Tambani wilaya ya Mkuranga.
Kutokana na tishio hilo limesababisha uongozi wa Kijiji hicho
kushindwa kwenda baadhi ya maeneo wakihofia maisha yao kutokana na watu hao
kutumia silaha mbalimbali za kijadi kwa ajili ya kufanya uhalifu.
Aliyasema hayo juzi Kijijini hapo alipotembelea kusikiliza kero
hiyo ambayo imewafanya baadhi ya wakazi wa eneo hilo kuhama na kushindwa
kufanya shughuli za maendeleo kwenye maeneo yao kutokana na hofu ya kuuwawa.
“Natoa siku tatu kuanzia leo hakikisheni mmewakamata watu hao
ambao kwa bahati majina mmnayo hakuna haja ya watu kushindwa kuishi kwa amani
nchi hii haijafikia hatua ya watu kushindwa kukaa kwenye maeneo yao au viongozi
kuogopa kwenda kwenye eneo lao la utawala,” alisema Ndikilo.
Alisema kuwa wananchi wa Kijiji hicho wamekwenda ofisini
kwake zaidi ya mara tano wakilalamikia kundi hilo la watu ambao wametajwa kuwa
ni kikundi cha watu 15 kabila la Kikurya ambao wanadaiwa kutokea eneo la
Msongola wilaya ya Ilala Jijini Dar es Salaam.
“Wananchi wamekuwa wakilalamika kuwa licha ya kulalamika kwa
Jeshi hilo ngazi ya wilaya lakini hakuna hatua zozote zilizochukuliwa ambapo
hadi sasa watu watatu wameuwawa na kundi hilo la watu ambao ni wavamizi wa
ardhi pia wamekuwa wakifanya vitendo vya uhalifu wa kuvunja nyumba, kuiba na
kufanya vitendo vya ubakaji,” alisema Ndikilo.
“Inashangaza kuona kuwa mgogoro huu wa wavamizi ulianza tangu
mwaka 2014 lakini hadi sasa hakuna hatua madhubuti ambazo zimechukuliwa za
kudhibiti kundi hili ambalo ni hatari kwa wananchi ambao hawana hatia na kilio
chao lazima kisikilizwe na si kuwaacha walalamike wakati viongozi wapo,”
alisema Ndikilo.
Awali mwenyekiti wa Kijiji hicho Amir Mbamba alisema kuwa
walishachukua hatua mbalimbali katika kuhakikisha suala hilo linakomeshwa kwa
kulipeleka kwa mkuu wa wilaya lakini kundi hilo bado limeendelea kuendesha
matukio hayo bila ya woga.
Mbamba alisema kuwa wananchi wake kutokana na kuona kuwa
hawasikilizwi walikwenda kwa Waziri Mkuu pamoja Tume ya Haki za Binadamu ili
waweze kusaidiwa tatizo lao na baadaye kwa mkuu wa mkoa ambaye leo umefika
kujua ukweli wa tukio hili.
“Wananchi wamesema kuwa wataandamana hadi Ikulu kwa Rais
endapo suala lao halitashughulikiwa ipasavyo hivyo kwa kuwa mkuu umekuja
mwenyewe ukweli umeupata hatua madhubuti zitasaidia kumaliza mgogoro,” alisema
Mbamba.
Kwa upande wake kamanda wa Polisi mkoani Pwani Bonaventura
Mushongi alisema kuwa watahakikisha kuwa watu hao wanakamatwa na amani itarudi
kama ilivyokuwa zamani kwani watajipanga ili kukomesha uhalifu huo.
Mushongi alisema kuwa kwa kuanzia katika kulikabili suala
hilo watashirikiana na kamati ya ulinzi na usalama ya Kijiji pamoja na mgambo
ili nao washiriki kikamilifu katika kulifuatilia suala hilo ili watu waishi kwa
amani bila ya hofu.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment