Na John Gagarini, Kibaha
JUMLA ya mabasi 48 ya abiria ya kwenda mikoani yamekutwa na
makosa mbalimbali kufuatia zoezi la ukaguzi lillofanywa kwa ushirikiano baina ya
Jeshi la Polisi na Mamlaka ya Usafirishaji Majini na Nchi Kavu (SUMATRA).
Zoezi hilo lilifanywa kwenye Stendi Kuu ya Ubungo, Maili Moja
na Chalinze kwa lengo la kudhibiti ajali pamoja na madereva wanaokiuka taratibu
za usalama barabarani kwa mabasi hayo yaendayo mikoani .
Akizungumza na gazeti hili Kaimu Kamanda wa Kikosi cha
Usalama barabarani nchini ACP Fortunatus Musilimu alisema kuwa zoezi hilo
ambalo lilikuwa la kushtukiza litakuwa endelevu ili kuhakikisha ajali zinapungua
na kuwaondolea usumbufu abiria.
Musilimu alisema kuwa waliyafanyia ukaguzi mabasi 169 na
kuyabaini mabasi hayo 48 kuwa na makosa mbalimbali ikiwa ni pamoja na mwendokasi
mabasi 24, kutofunga mikanda mabasi tisa, kuwazidishia nauli nane, ubovu basi
moja, kukiuka ratiba basi moja na leseni basi moja.
“Pia tulimakamata dereva mmoja kwa kutumia kilevi ambapo
alikuwa na kiwango cha juu cha ulevi cha 77.7 ambapo kwa kawaida kinatakiwa
kuwa 00.8 kwa mujibu sheria hali iliyosababisha dereva huyo kushushwa na
kupelekwa rumande,” alisema Musilimu.
Alisema kuwa ukaguzi huo unandelea kote nchi ambapo tayari
makamanda wa usalama barabarani mikoani wameshapewa maagizo ya kufanya ukaguzi
wa mabasi kwani ukaguzi hauwezi kuyakagua mabasi yote kutokana na eneo la
ukaguzi kuwa dogo hali ambayo inawafanya wafanyie ukaguzi mabasi matano matano
kwa wakati mmoja huku mengine yakiendelea na safari.
Aidha alisema kuwa mbali ya kukagua mabasi hayo pia walikagua
malori ya mchanga 13 na kuyakuta na makosa mbalimbali ikiwa ni pamoja na mwendo
kasi magari saba, mabovu matano, kuyapita magari mengine pasipo kuzingatia
sheria.
Aliwataka abiria kutoa taarifa kwenye vyombo husika kwa
madereva ambao wanaoendesha magari kwa mwendo wa kasi pia wasiwashabikie kwani
ni moja ya vyanzo vya ajali za barabarani ambazo zinasababisha vifo vya watu
wengi.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment