Na John Gagarini, Kibaha
WAFANYABIASHARA wa jumla na rejareja wa mazao ya nafaka
kwenye soko la maili Moja wilayani Kibaha mkoani Pwani wameiomba Halmashauri ya
Mji huo kuondoa ushuru wa shilingi 1,000 kwa gunia la kilogramu 100 la nafaka
linaloingia sokoni hapo.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi mjini Kibaha katibu
wa umoja wa wauzaji wa mazao ya nafaka sokoni hapo Ramadhan Maulid alisema kuwa
sheria hiyo ya utozaji wa ushuru wa shilingi 1,000 kwa gunia la la nafaka lenye
uzito wa kilogramu 100 ina kinzana na sheria mama ambayo inataka ushuru ukatwe
mara moja tu.
Maulid alisema kuwa wao wanaponunua nafaka hizo huko mikoani wanatozwa
ushuru wa shilingi kati ya 2,000 hadi 5,000 kutegemeana na Halmashauri hivyo
wanashangaa kutozwa tena mara wanapofikisha mzigo sokoni hapo.
“Kututoza ushuru tena ni sawa na kuwatoza ushuru mara mbili
kwani hata sheria ndogo hiyo iliyowekwa na Halmashauri haikuwashirikisha wao
kama watekelezaji wa sheria hiyo ambayo ilipitishwa mwaka 2007 na kutakiwa
kuanza kutumika mwaka 2008 lakini haikuwahi kutumika licha ya kwamba kwa miaka
ya nyuma ilikuwa ikitumika,” alisema Maulid.
Alisema kuwa waliletewa taarifa ya kutakiwa kulipa ushuru huo
hivi karibuni lakini walijaribu kuonana na viongoizi wa halmashauri bila ya
mafanikio ili kuzungumzia suala hilo ambalo kwao ni moja ya ushuru ambao ni kero.
“Mbali ya kutakiwa kulipia kiasi hicho pia gharama nyingine
ni pamoja na kulipia Kizimba kiasi cha shilingi 9,000, Ardhi 3,000 na mlinzi
6,000 ambazo hulipa kila mwezi hivyo malipo hayo ni sawa na kuwaongezea mzigo
wa ushuru,” alisema Maulid.
Aidha alisema kuwa kwa sasa wanawasiliana na wanasheria ili
kutoa tafsiri ya sheria hizo mbili kati ya sheria mama na sheria ndogo ya Halmashauri
ambapo inaonekana kama zinakinzana na kuleta mkanganyiko kwao.
Kwa upande wake mwenyekiti wa soko hilo Ally Gonzi alisema kuwa
tangu walipoletewa sheria hiyo ndogo ambayo ilipitishwa kwenye baraza la
madiwani walijaribu kufanya vikao mbalimbali na Halmashauri ili kuangalia namna
ya kupunguza ushuru huo lakini ilishindikana ambapo Halmashauri iliwaambia kuwa
kama wanataka uondolewe basi wafuate taratibu.
Naye mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha Gladdys
Dyamvunye alisema kuwa wafanyabiashara hao wanapaswa kulipa ushuru huo kwani
uko kisheria na tayari vyombo vya sheria vimetoa siku 14 kwa wafanyabiashara
hao kulipa na endapo hawatalipa watashitakiwa.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment