Na John Gagarini, Kibaha
MKUU wa mkoa wa Pwani Injinia Evarist Ndikilo ameunda Tume kutoka
idara ya kazi ya mkoa huo kutembelea kiwanda cha Hong Yu Steel cha kuzalisha
nondo kilichopo wilayani Kibaha kwa kushindwa kuzingatia masharti ya uendeshaji
wa kiwanda na maslahi ya wafanyakazi.
Aliunda tume hiyo ya watu watatu itakayofanya kazi kwa wiki
moja kufuatilia malalamiko hayo ya wafanyakazi kwa lengo la kuleta uwajibikaji
kwa pande zote mbili katia ya wafanyakazi na wamiliki hao baada ya malalamiko
kuzidi na kufanya ziara kujionea hali halisi.
Ndikilo alifikia hatua hiyo baada ya kupata malalamiko toka
kwa wafanyakazi kuwa wamiliki wa kiwanda hicho hawajali usalama kazini kwa
wafanyakazi wao kwa kushindwa kuweka vifaa vya kuwalinda kutokana na mazingira wanayofanyia
kazi ambayo ni hatarishi kwa maisha yao.
“Tumesikia wafanyakazi na tumeona wafanyakazi wakifanya kazi
huku wakiwa hawana vifaa vya kufanyia kazi kama vile baadhi yao hawajavaa kofia
ngumu, gloves na mabuti kwa ajili ya kujikinga na hatari zinazoweza kujitokeza
wakati wa kufanya kazi,” alisema Ndikilo.
Alisema wafanyakazi wamelalamikia mambo mengi ikiwa ni pamoja
na mshahara mdogo, kutokuwa na mikataba ya kazi, kutolipwa masaa ya ziada, kukatwa
mishahara mara wanaposhindwa kwenda kazini kutokana na kuumwa au kuumia kazini,
huduma ya kwanza kuchelewa pamoja na kutokuwa na mapumziko hata nyakati za
sikukuu na mwisho wa wiki.
“Tumeona kuna matatizo mengi hivyo itaundwa tume kwa ajili ya
kukaa na uongozi kwa ajili ya kurekebisha kasoro zilizopo kwa kuzingatia sheria
za kazi kwani kila mtu anamtegemea mwenzake kati ya mwajiri na mfanyakazi hivyo
hakuna sababu ya upande mmoja kumnyanysa mwenzake,” alisema Ndikilo.
Aidha alisema kuwa tume hiyo itatembelea vitengo vyote kwa
kuonana na viongozi wa vitengo husika na baadaye kukaa na uongozi ili kuangalia
namna ya kuboresha mazingira ya kazi pamoja na maslahi ya wafanyakazi.
Kwa upande wake kaimu ofisa kazi wa mkoa Swalehe Njoma
alisema kuwa haki nyingi za wafanyakazi zimevunjwa hivyo kuna haja ya
kurekebisha na kuweka mazingira bora ya kazi ili haki iweze kupatikana kwani
malalamiko ni mengi.
Njoma alisema kuwa moja ya haki za mfanyakazi ni kuwa na muda
wa mapumziko na hata kama atafanya kazi kwa masaa ya ziada lazima alipwe na mfanyakazi
anapoumwa au kuumia kazini hapaswi kukatwa fedha kutokana na kushindwa kwenda
kazini kutokana na kujiuguza.
Naye ofisa mwajiri wa kiwanda hicho Asantemungu Filbert
alikiri kuwepo na matatizo ambapo alisema kuwa yeye ni mgeni na hana muda mrefu
ila kwa mtangulizi wake hakuweza kuweka mazingira mazuri ya wafanyakazi.
Filbert alisema kuwa tayari ameandaa utaratibu wa
kushughulikia kero za wafanyakazi ikiwa ni pamoja na kuboresha mazingira ya
kufanyia kazi ili kukabiliana na changamoto zilizopo na kufanya utendaji kazi
kuwa mzuri.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment