Saturday, March 19, 2016

VIJANA KUENDESHA MRADI WA SAMAKI MTAA WA KIBONDENI

Na John Gagarini, Kibaha
MTAA wa Kibondeni Kata ya Mkuza wilayani Kibaha utawapatia mafunzo ya ufugaji wa samaki vijana 40 wa mtaa huo ili waendeshe mradi wa ufugaji wa samaki kwenye bwawa la mtaa ambalo limerudishwa baada ya kuuzwa kimakosa kwa mtu binafsi.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi ofisini kwake mjini Kibaha mwenyekiti wa mtaa huo Hamis Mwarizo alisema kuwa vijana hao watapewa mafunzo hayo kutoka ofisi ya kata ili vijana waweze kujua namna ya kufuga samaki.
Mwarizo alisema kuwa mafunzo hayo yatatolewa kwa vijana ambao watakuwa wameunda vikundi ambavyo vitaendesha mradi huo ambao utatoa ajira kwa vijana hao na watakuwa wakipeana zamu ya kusimamia.
“Lengo la mradi huo ni kuongeza ajira kwa vijana ambapo asilimia 70 ya mapato yatakwenda kwenye kikundi na asilimia 30 yatakwenda kwenye mtaa kwa ajili ya shughuli mbalimbali za maendeleo ya jamii ya mtaa wetu,” alisema Mwarizo.
Alisema kuwa kwa sasa tayari vijana 16 wameshapatikana kwa ajili ya kuanzisha kikundi cha mwanzo na wengine wanaendelea kujiandikisha na baadaye kikundi hicho kitasajiliwa ili kitambulike kisheria baada ya mradi huo kupitishwa ana wananchi kwenye mkutano mkuu wa mtaa.
“Kundi la kwanza litaendesha kwa kipindi cha miaka 10 na baadaye litapewa kundi lingine kwa ajili ya kuendeleza mradi huo ambao mbali ya kuwapatia vijana ajira pia utaipatia jamii ya eneo hilo na maeneo jirani lishe kwa ajili ya kuboresha afya,” alisema Mwarizo.
Katika hatua nyingine alisema kuwa kwa sasa wanaendelea na taratibu za kulipima eneo la bwawa hilo ili kujua mipaka yake halisi ambapo maji yake baada ya kupimwa yalibainika kuwa hayafai kwa kunywa kwani yana viluilui ambavyo vinaweza kusababisha maradhi ya ugonjwa wa tumbo hivyo yatatumika kwa ajili ya kulimia bustani pamoja na kufulia.
Mwisho.


No comments:

Post a Comment