Na John Gagarini, Kibaha
JESHI la Polisi mkoani Pwani linawashikilia watu wawili kwa
tuhuma za kutaka kumtapeli mtu mmoja kiasi cha shilingi milioni tatu kwa
kumuuzia madini aina ya Almasi ambayo ni bandia.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake kamanda wa
polisi mkoani humo Bonaventura Mushongi alisema kuwa watu hao ambao walikuwa
wanne wengine wawili walifanikiwa kukimbia walikamatwa baada ya kutaka kukimbia
kutokana na mlalamikaji kupiga kelele ya kuomba msaada.
Mushongi alisema kuwa tukio hilo limetokea juzi eneo la CCM
Mkoani wilayani Kibaha majira ya saa 3:30 asubuhi baada ya mlalamikaji kutoka
kuchukua fedha kwenye benki ya NMB Tawi la Kibaha.
“Mlalamikaji mara baada ya kuchukua fedha alikutana na
watuhumiwa hao ambapo waliongea naye na kumwambia kuwa wanauza madini aina ya
Almasi ambapo walikubalina na akawakabidhi fedha hizo,” alisema Mushongi.
Alisema kuwa watuhumiwa hao wakiwa kwenye gari aina ya Primio
lenye namba za usajili T 668 DFY walianza kuondoka lakini mlalamikaji akagundua
kuwa madini yale si halisi na kuanza kupiga kelele za wezi kuomba msaada ndipo
waendesha pikipiki walipoanza kuwafukuza na baadaye polisi nao wakatokea na
kuwakamata.
“Watuhumiwa hao baada ya kuona wamezingirwa walikimbia hata
hivyo wawili walikamatwa na wengine wawili walifanikiwa kutokomea kusiko
julikana nab ado tunaendelea kuwatafuta watuhumiwa wengine ili kuwafikisha
mahakamani kujibu tuhuma hizo,” alisema Mushongi.
Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Mwantumu Juma maarufau kama
Hawa, Fidelis Buberwa au Finas Barongo ambao wanashikiliwa kutokana na tukio
hilo ambapo gari hilo linashikiliwa.
Kufuatia tukio hilo kamanda aliwataka wananchi kutokubali
kuuziwa madini mikononi badala yake waende sehemu husika ambazo ziko rasmi kwa
ajili ya uuzaji wa madini ili kuepukana na watu kama hao.
Mwisho
No comments:
Post a Comment