Saturday, March 19, 2016

RAS PWANI KUFUNGUA MAFUNZO YA MPIRA WA WAVU

Na John Gagarini, Kibaha
KATIBU Tawala (RAS) Mkoa wa Pwani Mgeni Baruani anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye ufunguzi wa mafunzo ya walimu wa mchezo wa wavu Volleyball yatakayoanza Machi 24 hadi Aprili Mosi mwaka huu kwenye viwanja vya shule ya Msingi Kibaha.
Akizungumza na waandishi wa habari katibu wa chama cha mchezo huo mkoani Pwani (COREVA) Lonjin Mzava alisema kuwa wanatarajia mafunzo hayo yatawahusisha walimu wa mchezo huo kwa shule za msingi walimu wanne , sekondari walimu wanne , vyuo pamoja na wadau wengine wanaopenda kujifunza mchezo huo.  
Mzava alisema kuwa washiriki watatoka wilaya zote za mkoa wa Pwani ambapo kwa walimu tayari barua za kuomba ushiriki wao zimepelekwa kwa wakurugenzi wa Halmashauri ili kuwpaatia ruhusa ya kushiriki mafunzo hayo.
“Wanafunzi wa mchezo huo watajifunza masomo ya darasani pamoja nay a vitendo ili kuwajengea uwezo wa kuujua mchezo huo hata watakapokwenda kuwafundisha wengine wawe na maarifa ya kutosha na mafunzo haya yameandaliwa kwa pamoja na chama cha mchezo huo nchini (TAVA) alisema Mzava.
Alisema kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuwapa ujuzi wa kutosha walimu wa mchezo huo ili waweze kujua sheria na namna mchezo unavyochezwa na kuusimamia kama sheria za mchezo huo zinavyoonyesha na kupitishwa na chama cha mchezo huo cha kimataifa FIVB.
“Hadi sasa walimu kutoka Hlamashauri za Bagamoyo, Mkuranga, Rufiji na Kibaha Mji tayari wamethibitisha kushiriki mafunzo hayo na waliobaki wanapaswa kuthibitisha kabla ya tarehe 22 Machi ili waweze kuwekewa utaratibu wa kushiriki mafunzo hayo,” alisema Mzava.
Aidha alisema kuwa walimu watakaofanya vizuri kwenye mafunzo hayo watapata nafasi ya kushiriki mafunzo ya Kimataifa ya Beach yatakayofanyika Aprili mwaka huu Jijini Dar es Salaam hivyo itasaidia kuutangaza mkoa kupitia mchezo huo.
“Tunaomba wadau mbalimbali wajitokeze kudhamini mafunzo haya kwani hata wakitoa maji au kitu chochote itasaidia kupunguza gharama za kuendesha mafunzo hayo kwani hadi sasa hakuna wadhamini waliojitokeza kuzamini mafunzo hayo,” alisema Mzava.
Alibainisha kuwa matarajio ni kuzalisha walimu wengi wa mchezo huo hasa mashuleni na itasaidia kupunguza gharama za kuwalipa walimu toka nje hawa wakati wa mashindano ya Umoja wa Shule za Msingi na Utamaduni Tanzania( UMITASHUMTA) na Umoja wa Shule za Sekondari na Sanaa Tanzania (UMISSETA).

Mwisho. 

No comments:

Post a Comment