Thursday, March 10, 2016

DK KIGANGWALA AMPA SAA 24 MKURUGENZI KUANDIKA BARUA YA KUJIELEZA KWANINI ASIONDOLEWE KWENYE NAFASI HIYO, AFUNGA CHUMBA CHA MAITI ATAKA WAFANYE MAREKEBISHO NDANI YA SIKU TATU

Na John Gagarini, Kibaha
NAIBU Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Dk Hamis Kigangwala ametoa saa 24 kwa Mkurugenzi wa Shirika la Elimu Kibaha (KEC) Dk Cyprian Mpemba kuandika barua ya kwa nini asiondolewe kwenye nafasi hiyo kwa kushindwa kuendesha Hospitali Teule ya Rufaa ya Tumbi iliyopo wilayani Kibaha mkoani Pwani.
Waziri Dk Simbachawene alitoa agizo hilo huku mkurugenzi huyo akiwa hayupo na kumwagiza Kaimu Mkurugenzi wa Shirika hilo Anase Nko kumfikishia ujumbe huo Dk Mpemba kwa ajili ya kutoa maelezo hayo.
Dk Kigangwala aliyasema hayo jana mara baada ya kutembelea hospitali hiyo kutokana na kuwa na changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na kushindwa kusimamia maslahi ya watumishi ambao wamekosa morali ya kufanya kazi.
Alisema kuwa hali iliyopo kwenye hospitali hiyo ni mbaya sana na inasikitisha sana huku ofisi ya mkurugenzi ikiwa inatumia fedha ambazo zingesaidia kuboresha huduma kwenye hospitali hiyo.
“Shirika limeshindwa kuendesha natoa saa 24 hadi leo saa nane mchana awe ameandika barua ya kujieleza kwanini asiondolewe kwenye nafasi hiyo kwani ameshindwa kusimamia hospitali hiyo kwani vitu vingi haviko sawa kuanzia mochwari ambapo imekuwa ikitoa harufu mbaya kutokana na baadhi ya vifaa vya majokofu kuharibika,” alisema Dk Kigwangala.
“Nataka atoe maelezo yanayojitosheleza kwani inaonekana hakuna jambo ambalo linaweza kufanyika kwenye hospitali bila ya mkurugenzi ambapo fedha za hospitali zimekuwa zikitumika kwenye matumizi mengine,” alisema Dk Kigangwala.
Aidha alisema kuwa mbali ya hivyo pia kuanzia sasa shirika hilo lisisimamie masuala ya fedha za Hospitali hiyo bali ijisimamie yenyewe ili kuangalia vipaumbele vinavyohusu hospitali kwani huduma hazisubiri utaratibu.
“Tumeona kuwa tatizo ni utawala ambao unaonekana umeshindwa kusimamia hospitali nilipokuja nilifikiri tatizo ni meneja wa Huduma za afya Dk Peter Datani lakini una bahati nilikuja kwa ajili ya kukutimua wewe kumbe wewe huusiki,” alisema Dk Kigwangwala.
Alibainisha kuwa kuna changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na chumba cha upasuaji kutokuwa na hadhi kwani ni sawa na stoo, viyoyozi havifanyi kazi, chumba cha wagonjwa mahututi nacho hakiko sawa na vifaa vinaharibika hakuna matengenezo hivyo huduma kuwa mbaya.
“Inashangaza kuona kuwa hospitali inakosa vifaa tiba pamoja na madawa licha ya kuwa inaingiza fedha nyingi kati ya shilingi milioni 120 hadi 150 kwa mwezi lakini inashindwa kujiendesha inashindwa hata kutoa milioni sita kwa ajili ya kununulia mifuko ya kuhifadhia damu inasikitisha sana hospitali hii inaendeshwa kiujanja ujanja tu lazima mjiendeshe kwa mikakati siyo kwenda tu,” alisema Kigwangwala.
Kutokana na hali hiyo ameagiza chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali hiyo ifungwe na iwe imefanyiwa matengenezo ndani ya siku tatu na watajua maiti watazipeleka wapi kwani haiwezekani chumba hicho kuwa kwenye hali hiyo pia miezi mitatu wanatakiwa wawe wamehakikisha maji yanapatikana kwa kujenga matenki ya kuhifadhia maji.
Alimtaka mkuu wa mkoa kupata ushauri kwa  wataalamu ili kuangalia mahusiano baina ya hospitali hiyo na sekretarieti ya mkoa pia inaonekana ni vema hospitali hiyo ikasimamiwa na mkoa badala ya shirika.
Alisisitiza kuwa endapo watashindwa kukarabati chumba hicho cha maiti ndani ya siku tatu atawaondoa kwenye nafasi zao kwani watakuwa wameshindwa kutekeleza agizo la serikali kwani haiwezekani huduma kutolewa kwenye mazingira magumu wakati fedha zinapatikana.
Kwa upande wake msajili wa hospitali nchini Dk Pamela Sawa alisema kuwa walifanya ukaguzi kwenye hospitali mwaka 2010 hadi 2011 ambapo walikuta hospitali nyingi zina mapungufu mengi mafano hospitali ya Mawenzi mkoani Kilimanjaro ilikuwa ikitumia chumba cha upasuaji kilichokuwa kikitumika enzi za mkoloni lakini walibadilisha baada ya kuifunga pia hospitali ya Mbeya nayo ilikuwa na matatizo ya maji.
Naye Dk Datani alisema kuwa changamoto kubwa iliyopo hospitalini hapo ni ukosefu wa fedha kwani waliomba kiasi cha shilingi milioni 600 lakini walipewa kiasi cha milioni sita tu hivyo kujikuta wakiwa kwenye wakati mgumu wa kuboresha maslahi ya wafanyakazi pamoja na kununua vifaa tiba pamoja na madawa.
Mwisho.

   

No comments:

Post a Comment