Saturday, March 19, 2016

SHULE YAKABILIWA NA UHABA WA WALIMU INA WALIMU WAWILI TU

Na John Gagarini, Bagamoyo
MAZINGIRA magumu yanayokikabili Kijiji cha Kitame Kata ya makurunge wilayani bagamoyo mkoani Pwani yamesababisha walimu walimu wawili wanaofundisha shule hiyo kufundisha kwa siku 90 kwa mwaka mzima.   
Kutokana na shule hiyo kuwa kwenye mazingira magumu walimu wengi wamekuwa hawako tayari kufundisha shule hiyo yenye wanafunzi 51 wa kuanzia darasa la kwanza hadi la saba ambayo ni idadi ndogo kutokana na mazingira hayo.
Akizungumza mbele ya Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo Dk Shukuru Kawambwa, moja ya wakazi wa Kijiji hicho aliyejitambulisha kwa jina la Adam Rashid alisema kuwa moja ya changamoto zinazowakabili ni pamoja na kutokuwa na usafiri wa uhakika kutokana na ubovu wa miundombinu.
“Usafiri wa kutokana Kijijini hapa hadi makao makuu ya wilaya ni kilometa 54 kwa njia ya barabara na usafiri wake ni pikipiki na gharama yake ni kiasi cha shilingi 50,000 huku ule wa kutumia njia ya bahari mitumbwi gharama yake ni kiasi cha shilingi 60,000 kwenda na kurudi,”  alisema Rashid.
Alisema gharama hizo ni kubwa sana ajambo ambalo linawafanya walimu washindwe kwenda kufundisha kutokana na mazingira hayo ambapo walimu hao wawili wamekuwa wakipokezana kufundisha madarasa hayo.
“Wanafunzi wanafundishwa siku chache kutokana na walimu hao wakati mwingine kutofika kabisa shuleni hali ambayo inawakatisha tamaa wanafunzi na kusababisha kuwa na idadi ndogo ya wanafunzi wanaosoma shuleni hapo,” alisema Rashid.
Aidha aliiomba serikali kusaidia kupatikana kwa walimu ili kukabiliana na hali ya wanafunzi hao kukosa masomo na kusababisha elimu kuwa duni hali ambayo itatoa matokeo mabaya kwa wanafunzi wanaosoma kwenye shule hiyo.
Kwa upande wake diwani wa kata ya Makurunge Kabile Paulo alisema kuwa walimu wengi wanashindwa kwenda kufundisha shuleni hapo kutokana na mazingira magumu kwani hakuna huduma muhimu za jamii hivyo kushindwa kukaa huko.
Paulo alisema kuwa baadhi ya huduma ambazo hazipo ni pamoja na huduma ya afya kwani hakuna zahanati na huduma nyingine muhimu ambazo huwabidi kuzifuata Bagamoyo au maeneo mengine jambo ambalo limekuwa likiwagharimu.
Naye mbunge wa Jimbo hilo la Bagamoyo Dk Shukuru Kawambwa alisema kuwa kweli hiyo ni changamoto ambayo inawakabili wakazi na walimu hao lakini kwa kushirikiana na diwani wa kata hiyo watahakikisha wanaitatua.
Dk Kawambwa alisema kuwa Halmashauri itafanya mgao wa walimu na ataiomba itoe kipaumbele kwa shule hiyo kwa kuwapatia walimu ili waweze kwenda huko na kuongeza nguvu ya ufundishaji kwenye shule hiyo ambayo iko pembezoni na kuwataka vijana waliosoma vyuo vya ualimu na ni wenyeji wa kata hiyo kujitolea kwenda kufundisha kama njia mbadala ya upungufu huo wa walimu.
Mwisho.  
  

No comments:

Post a Comment