Na John Gagarini, Kibaha
MAMLAKA ya Usafirishaji Majini na nchi kavu SUMATRA kwa
kushirikiana na Jeshi la Polisi nchini wamefanya operesheni ya kushtukiza ya
kukagua mabasi yaendayo mikoani na kubaini makosa mbalimbali ikiwa ni pamoja na
baadhi ya madereva kutumia vilevi na kuwzidishia nauli abiria.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Kibaha wakati wa
zoezi hilo Mkurugenzi wa SUMATRA, Johnsen Kahatano alisema kuwa operesheni hiyo
imefanywa ili kuwadhibiti wamiliki pamoja na madereva ambao wanakiuka sheria za
usalama barabarani.
Kahatano alisema kuwa operesheni hiyo imefanikiwa kwani
wameweza kukamata makosa kadhaa ambayo mengine ni ya barabarani na mengine ni
ya kuwazidishia nauli abiria jambo ambalo ni kosa kisheria ambapo mabasi
yaliyofanya makosa wamiliki wake watafikishwa mahakamani.
“Tumefanikiwa kumkamata dereva mmoja alikutwa akiwa ametumia
kilevi na tulimkamata na kulizuia basi hilo hadi walipoleta dereva mwingine kwa
ajili ya safari jambo ambalo ni la
hatari kwa usalama wa abiria,” alisema Kahatano.
Alisema kuwa mabasi sita yalikamatwa yakiwa yamezidisha nauli
ambpao abiria waliokuwa wakienda Moshi walkatiwa nauli ya kwenda Arusha ambayo
ni shilingi 33,000 huku nauli halali kwa watu wanaoshukia Moshi ni shilingi
28,500.
“Mabasi yaliyowazidishia abiria walirudishiwa nauli zao kama
taratibu zinavyoonyesha na hili ni kosa kisheria na abiria wanapaswa kulipa
nauli halali ambazo zimepitishwa kisheria na wanapaswa kwenda kulalamika endapo
watabaini wamezidishiwa,” alisema Kahatano.
Naye Kaimu Kamishna wa Usalama Barabarani Fortunatus Musilimu
alisema kuwa abiria nao ni wadau muhimu katika vita ya kupambana na madereva au
wamiliki wanaokiuka taratibu za usalama barabarani na kupunguza ajali hivyo
wanapaswa kutoa taarifa kwao ili hatua ziweze kuchukuliwa.
Musilimu alisema kuwa watu wanataka kuishi na maendeleo si
kukatishwa uhai kutokana na ajali ambazo zinaweza kuzuilika na kutoa taarifa
polisi kwa kutumia njia ya simu ambazo ziko kwenye mabasi yote lengo likiwa ni
kupunguza ajali.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment