Na John Gagarini, Kibaha
MKUU wa mkoa wa Pwani Injinia Evarist Ndikilo amesema kuwa
ataituma sekretarieti ya mkoa wa Pwani kufuatialia kwa wakurugenzi wa
Halmashauri za Wilaya za mkoa huo kuchunguza juu ya fedha kiasi cha shilingi
milioni 249, 452,390 kuwa zimerudishwa Hazina ikiwa ni sehemu ya fedha kiasi
cha shilingi milioni 641,361,239 ambazo ni hasara zilizolipwa kwa watumishi
hewa 25.
Mbali ya kuituma sekretarieti kufuatilia suala la fedha hizo
pia amewataka wakuu wa wilaya kutumia vyombo vya dola kama vile Jeshi la
Polisi, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kufuatilia watu
waliohusika kuchukua fedha hizo.
Akizungumza na gazeti hili ofisini kwake mjini Kibaha Ndikilo
alisema kuwa serikali haijaridhishwa na majibu ya wakurugenzi hao kuwa fedha
hizo wamezirejesha Hazina huku kukiwa hakuna viambatanisho vyovyote ambavyo
vinaonyesha kuwa fedha hizo zilipelekwa hazina.
“Serikali inataka kujua ni nani aliyehusika kuchukua fedha
hizo kinyume cha taratibu za kazi kwani watumishi hao ni hewa lakini cha ajabu
walikuwa wakilipwa mishahara kwa kila mwezi na kuitia serikali hasara kiasi
hicho,” alisema Ndikilo.
Ndikilo alisema kuwa kati ya hao watumishi hewa ni wale ambao
wamefariki dunia, wasio kuwepo kazini kuacha kazi na wastaafu lakini walikuwa
wanalipwa kama vile wako kazini jambo ambalo ni kinyume cha sheria na
wanastahili kuchukuliwa hatua kali mara watakapo kutwa na tuhuma hizo.
“Zoezi hili litaendelea kufanyika ili kubaini ni njia gani
walizokuwa wakizitumia hadi kufikia kulipwa fedha hizo ili hali hawako kazini
na kuisababishia serikali hasara kubwa kiasi hicho hali ambayo imefanya zoezi
hilo kufanywa kwa watumishi wa serikali ili kuwabaini,” alisema Ndikilo.
Aidha alisema alisema kuwa kama kuna watu walikuwa wakifoji
na kujipatia fedha hizo endapo watabainika watachukuliwa hatua kali za kisheria
ili kukomesha wizi huo wa kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu kwa kuiibia
serikali.
Alisisitiza kuwa suala la watumishi hewa lilikuwa ni kama
kansa ambayo inaitafuna nchi lakini baada ya Rais Dk John Magufulia kubaini na
kuagiza kutafutwa watumishi hewa ni dhahiri hatua zitakazochukuliwa zitakomesha
watumishi hewa waliokuwa wanaiibia serikali.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment