WANANCHI wametakiwa kuacha kuharibu noti kwani endapo wakikutwa na hatia adhabu yake ni faini ya shilingi 500,000 kwa noti moja au kifungo cha mwaka mmoja jela.
Aidha alisema kuwa kwa mtu atakayebainika kutengeneza noti bandia akibainika kifungo chake ni cha maisha jela na vifaa vyote vilivyotumika kuzitengeneza vitataifishwa.
Hayo yalisemwa Jijini Dar es Salaam na Ofisa kutoka Kurugenzi ya usimamizi wa Sarafu kutoka Benki Kuu (BoT) Shedrack Mapunda alipokuwa akielezea kuhusu utambuzi wa alama za usalama katika noti na utunzaji bora wa noti wakati wa mafunzo ya waandishi wa habari juu ya uchumi na fedha.
Mapunda alisema kuwa baadhi ya watu hawafahamu sheria za fedha kuwa haziruhusu uharibifu wa sarafu kwani hilo ni kosa kisheria na adhabu zipo.
"Endapo utabainika umeharibu noti utachukuliwa hatua za kisheria na ukibainika utafikishwa mahakamani kwani ukikutwa na hatia kila noti moja iliyoharibiwa adhabu yake ni 500,000 au jela mwaka mmoja,"alisema Mapunda.
Alisema kwa mtu ambaye atakutwa na hatia kwa ya kukutwa na noti bandia sheria inambana na anaweza kufungwa kifungo cha miaka saba jela hivyo umakini unahitajika.
"Wananchi wanapaswa kutoharibu noti kwani sheria zipo lakini kwa sasa wamejikita kutoa elimu zaidi lakini baadaye wataanza kutumia sheria hizo ili kudhibiti wale wanaoharibu noti na unapokutwa ba noti bandia huwezi kusema hukufahamu .
Alisema kuwa wananchi anapaswa kutunza noti na kutoharibu kwani hilo ni kosa kisheria kwani kuna baadhi wanazikanyaga au kuzikata au kutumia kwa njia ambayo siyo sahihi.
Kwa upande wake Meneja Msaidizi wa Idara ya Mawasiliano BoT Noves Moses alisema kuwa baadhi ya watu wamekuwa wakitumia noti kutengeneza mataji wakati wa sherehe.
Moses alisema kuwa baadhi ya watu wamekuwa wakitengeneza kadi kwa noti jambo ambalo ni kinyume cha sheria hivyo jamii inapaswa kupewa elimu juu ya matumizi mabaya noti kwani nikosa kisheria.
No comments:
Post a Comment