Thursday, January 9, 2025

LICHA YA UNYNANYASAJI KIJINSIA NURU AWADH AWAANGUSHA VIGOGO WANAUME



WANAWAKE wanaowania nafasi za uongozi wanakabiliwa na changamoto za unyanyasaji wa kijinsia kutokana na baadhi ya watu au wagombea kuwa kejeli kuwa hawana uwezo wa kuongoza wao kazi yao ni kulea, kupika kumhudumia mume,”alisema Nuru Awadh.

Hiyo ni baadhi ya misemo wanayokutana nayo wanwake wanapoingia kwenye kuwania nafasi mbalimbali za uongozi dhana ambayo imekuwa ikiwakatisha tamaa baadhi ya wanawake hivyo kushindwa kujiingiza kwenye kuwania nafasi za uongozi.

Baadhi ya wanawake wameshindwa kuendelea na siasa au kuwania nafasi za uongozi wamekuwa wakizuliwa kashfa kuwa ni wahuni tu jambo ambalo siyo la kweli kwani wao nao wana uwezo wa kuongoza kama ilivyo kwa wanaume.Hayo ni maneno ambayo ymesmwa na Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Miembe saba B Nuru Awadh kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) wakati akiongea na mwandishi wa habari wa gazeti la HabariLeo ofisini kwake alisema kuwa ukatili wa kijinsia na mfumo dume bado upo na una warudisha nyuma wanwake kuwania nafasi za uongozi  au kuingia kwenye siasa.

Kuna dhana imejengeka kuwa kiongozi lazima awe mwanaume na mwanamke hawezi kuwa kiongozi hali hiyo imekuwa ikiwarudisha nyuma wanawake ambapo jamii inapaswa iikemee na kuwapa wanwake nafasi sawa na wanaume.

“Namshukuru mama alinipambania nipate elimu lakini kwa upande wa baba hakuwa na msukumo kwa watoto wa kike kupata elimu hali ambayo ilisababisha nishindwe kwenda chuo cha ualimu baada ya kumaliza elimu ya sekondari,”alisema Awadh.

Awadh alisema kuwa wakati wa kuwania nafasi ya uenyekiti alikutana na unyanyasaji wa kijinisa kwani watu walimtolea kila aina ya kashfa lakini alipambana kwani alijua ni masuala ya kisiasa tu ili kumharibia asishinde kuanzia ndani ya chama hadi kwenye uchaguzi wa mtaa ambapo alishindana na kiongozi kutoka chama cha Chadema na yeye kumshinda na alikuwa mwanaume.

Alisema kuwa wanaume waachane na mfumo dume kwani unarudisha nyuma maendeleo kwani kuna viongozi wazuri wanawake na wana uwezo mkubwa wa kuongoza kuliko hata wanaume hivyo wasitumie nafasi hiyo kuwakandamiza wanawake.

“Nimetolewa maneno mengi ya kashfa na watu wa kawaida na baadhi ni viongozi ili tu kunidhoofisha lakini sikukata tamaa niliendelea kupambana na kushinda namshukuru na mume wangu kwani alinipa moyo na aliendelea kuniunga mkono hadi nikafanikiwa kushinda lakini kama huna moyo unaweza kuacha siasa,”alisema Awadh.

Alisema kuwa mume wake alipambana na kuna wakati alimuombea kura kwenye maeneo mbalimbali na hata wakati wa kampeni aliambatana naye ili kumsaidia aweze kushinda kwenye nafasi hiyo ya uenyekiti hivyo kumpa moyo na kutokata tamaa na hata kumsaidia kuhudumia watoto wakati yeye anapokuwa anayatekeleza majukumu yake.

Alisema kuwa amekuwa akitenga muda wa kuhudumia jamii na kuhudumia familia yake kwani anahakikisha kila kitu kinakwenda sawa na pia anatenga siku kwa ajili ya kwenda ofisini hasa ikizingatiwa kuwa yeye ni mjasiriamali ambapo hutenga muda kwa majukumu yote hayo bila kuathiri sehemu nyingine.

“Baada ya kushinda mikakati au malengo yangu ni kuhakikisha tunaboresha barabara ya Mtaa ambayo imeharibika sana na tumeanza kuweka vifusi sehemu korofi ila matarajio ni kuichonga kwani licha ya mvua kunyesha na kuiharibu haikubahatika kuchongwa hivyo kuwa kwenye hali mbaya,”alisema Awadh.

Alisema kuwa kipaumbele chake kingine ni ujenzi wa zahanati kwani wanatumia umbali mrefu kwenda kupata huduma za afya ambapo hupata huduma kwenye Zahanati ya Mwendapole ambako ni mbali na hutumia gharama kubwa ambapo ikijengwa hapo itakuwa imewasaidia wakazi wa mtaa huo.

“Malengo yangu mengine kwa kushirikiana na wananchi ni kukabiliana na migogorpo ya ardhi kwani kuna changamoto kubwa ya migogoro hivyo atashirikiana na wajumbe wake kuitatua migogoro hiyo ambayo imekuwa ikiwapotezea watu muda mwingi kuitatua na hiyo ni kero kubwa sana kwenye mtaa wangu,”alisema Awadh.

Aidha alisema kuwa baadhi ya maeneo yana changamoto ya maji hivyo atahakikisha anawasiliana na Dawasa ili watatue changamoto kwenye baadhi ya maeneo ili wananchi waweze kupata huduma hiyo kwa karibu na suala la mawasiliano kuna maeneo hayapati mawasiliano ya simu na kusababisha kero kwa wananchi.

“Katika kukabiliana na changamoto ndani ya mtaa nimeteua kamati ambazo zitafutailia changamoto hizo kulingana na sekta na kero hizo nilizipata wakati wa kampeni na uongozi utakuwa shirikisha kwa kuwashirikisha wananchi ambapo kwa sasa bado hatujakaa mkutano wa mtaa hivyo tunaanza kutatua kupitia kero tulizozipata wakati ule,”alisema Awadh. Alibainisha kuwa wananchi walimpa kura na kusema kuwa wamewapa uongozi wanaume kwa vipindi viwili hivyo ni wakati wa wanawake sasa kuongoza na anajivunia Rais Dk Samia Suluhu Hassan kwa uongozi wake nao ni chachu ya yeye kuingia kwenye nafasi hiyo ili naye aweze kuwasidia wananchi kutatua kero akiwa kama muongoza njia.

USAWA WA KIJINSIA WAWEZESHA CATHERINE KUSHINDA UENYEKITI LICHA YA VIKWAZO VYA WANAUMEA


MWENYEKITI wa Serikali ya Mtaa wa Sofu kata ya Sofu wilaya ya Kibaha Mkoni Pwani Catherine Lyimo ni moja ya viongozi wanawake aliyeweza kuwa na ushawishi mkubwa uliowafanya wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kumpa kura za kishindo na kumshinda aliyekuwa mwenyekiti wa Mtaa huo mwanaume aliyeongoza kwa kipindi cha miaka 10.Hayo inaonyesha jinsi gani watu wamenaza kubadilika na kuwaamini wanawake kuwa viongozi na hiyo inatokana na jinsi serikali ilivyoweka mazingira ya usawa baina ya wanaume na wanawake kuanzia kwenye elimu uongozi na sehemu mbalimbali ili kuwa na usawa wa kijinsia.

Hali hiyo imejidhihirisha ambapo kwenye Halmashauri ya Mji wa Kibaha wenyeviti wanawake kwenye mitaa ni 10 hali ambayo ni tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma ambapo mila na desturi zilikuwa zikiwabana wanawake kuwa viongozi ambapo walikuwa hawapewi nafasi kabisa za kuwania uongozi au hata kwenye suala la elimu.

Lyimo aliondoa dhana hizo za wanwake kutoaminiwa na kuwa viongozi ambapo aliweza kuwashinda wanaume ambapo mwenyekiti aliyemaliza muda wake aliongoza kwa kipindi cha miaka 10 na mwingine alifanya kampeni kwa kipindi cha miaka zaidi ya miwli akijiandaa kutwaa nafasi hiyo.

“Yaani na wewe unataka kuwa mwenyekiti ungetuambia mapema sisi tumeshajipanga muda mrefu na wala huwezi kushinda na unajisumbua hivyo nafasi hii tuachie sisi wanawake hawawezi kuwa viongozi na hutajawahi kuongozwa na mwanamke,”alisema Lyimo.

Akizungumza na HabariLeo Lyimo alisema kuwa licha ya kuambiwa maneno hayo hayakumkatisha tamaa ambapo zikiwa zimesalia siku mbili huku akiona hakuna mwanamke yoyote aliyejitokeza kuwania nafasi ya kupata mwakilishi wa CCM kuwania nafsi ya uenyekiti yeye aliamua kujitosa.

Alisema kuwa kwenye uchaguzi huo yeye alipata kura 283 mpinzani wake akapata kura 119 na mshindi wa tatu alipata kura 83 ambapo jumla walikuwa wanaume wanne ambapo aliwabwaga na kupata nafasi ya kukiwakilisha chama kwenye uchaguzi wa Mtaa ambapo hata hivyo hakukuwa na chama cha upinzani na kuchukua nafasi hiyo na anamshukuru mume wake ambaye alimuunga mkono kwa kumpatia gari kwa ajili ya kufanya kampeni na hakuwa na wivu wa kimapenzi kwani anamwamini hivyo kutomzuia kufanya siasa.

“Mume wangu aliniruhusu kugombea lakini alikuwa na wasiwasi wa mimi kushinda lakini nilijipa moyo na kumwambia yeye anisaidie tu na matokeo atayaona mama yangu alikuwa akiunga mkono anapiga simu na kuniombea hata ndugu zangu nao waliniunga mkono na kupata baraka zao hivyo nikawa sina wasiwasi,”alisema Lyimo.

Alisema baada ya kufanikiwa kushika nafasi hiyo aliweka malengo ambayo ni kutatua changamoto za wananchi ikiwa ni pamoja na kujenga ofisi badala ya kutegemea ofisi za watu ambapo hazina nafasi kwa ajili ya kutoa huduma kwa wananchi.

Alisema kuwa eneo tayari wanalo wanachofanya ni kuwaandikia wadau wa maendeleo kwenye mtaa huo kwa kushirikiana na wananchi kufanya ujenzi huo ambao ni ndoto yake kuhakikisha mkakati wa kuwa na ofisi unafanikiwa.

“Mpango mkakati wa mtaa kwa sasa ni kuwa na ofisi yake badala ya kutumia ofisi za watu wengine tunataka tuwe na ofisi yetu wenyewe ili tufanye kazi kwa uhuru badala ya kutegemea wengine kwani kutumia ofisi za watu wengine kuna changamoto zake,”alisema Lyimo.

Aidha alisema kuwa anamatumaini ofisi itajengwa kutokana na ushirikiano anaoupata kutoka kwa wananchi na wadau wa maendeleo kwani anaamini ushirikiano huo utafanikisha kupatikana kwa ofisi ya mtaa huo.

“Nataka kwa kushirikiana wananchi na wadau kuhakikisha tunaacha alama ya uongozi kwa kujenga ofisi yetu kwani tukiwa na ofisi yetu tutakuwa na uhuru na tutajenga kutokana na mahitaji ya mtaa wetu ambapo itakuwa na vyumba kwa ajili ya kutoa huduma kwa wananchi,”alisema Lyimo.

Alibainisha kuwa jambo lingine ambalo atahakikisha linafanyika ni kuwagawia wananchi eneo la kufanyiabiashara kwa ananchi wa mtaa huo ili waweze kupata huduma ya soko karibu kwani wanataka liwe soko dogo ili kuwaongezea wananchi kipato na kutoa huduma.

“Tunahitaji tuwe na eneo ambalo litakuwa kama soko ambapo wananchi watauza bidhaa zao badala ya kwenda mbali kufuata mahitaji yao nyumbani tunataka wapate hapa jirani na pia itakuwa ni sehemu ya kujiongezea kipato,”alisema Lyimo.

Alisema kuwa nyingine ni kutafuta eneo kwa ajaili ya kujenga soko ambalo litatumiwa na wananchi wa mtaa huo ili waweze kujiongezea kipato kw akuinua uchumi wao badala ya kutumia masoko ya mtaa wa jirani wa Picha ya Ndege ambao ndiyo uliuzaa mtaa huo wa Sofu.

“Mimi mbali ya kuwa mjumbe pia nilikuwa mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Kata ya Sofu niliwasaidia sana watu kupata mikopo ya asilimia 10 kutoka Halmashauri kwani nilikuwa nikiwasaidia na hata kuwaandalia katiba na walifanikiwa kupata mikopo hiyo hivyo wengi walikuwa wakinipenda na nilipoingia kwenye kinyanganyiro sikupata shida sana kwani mimi sikufanya kampeni kama wenzangu na wala sikutoa rushwa ya fedha na wala sikuwa na fedha za kutoa,”alisema Lyimo.

Akizungumzia kuhusu rushwa ya ngono kwenye uchaguzi anasema hakukutana nayo kutokana na msimamo wake na changamoto kubwa ni wanawake kutojiamini wakifikiri kuwa uongozi ni wa wanaume kumbe hata wao wanaweza wanawenza kuongeza amewabadilisha wanawake wengi na kujiamini na kuomba nafasi mbalimbali za uongozi kwani wao ni jeshi kubwa. Aidha alisema kuwa mtu aliyemvutia na kuingia kwenye sisa ni Ester Matiko kutokana na jinsi anavyowasilisha hoja zake Bungeni na anatamani aje kuwa mbunge wa Viti maalumu baadaye na hata kuja kuwa waziri kwa miaka ijayo na Mtaa huo unazaidi ya wananchi 2,000.

LICHA YA KUKUTANA NA UKATILI WA KIJINSIA MBONI AUKABILI AWAGARAGAZA WANAUME


KWENYE uchaguzi wa serikali za mitaa ambao ulifanikisha kupatikana kwa wenyeviti na wajumbe baadhi ya wanawake walijitokeza kuwania nafasi hizo na kushindana na wanaume ambapo wanawake baadhi yao walijikuta katika wakati mgumu kwa kukumbana na ukatili wa kijinsia hasa kashfa kutoka kwa wanaume na hata wakati mwingine toka kwa wanawake wenzao.

Hali hiyo inatokana na mfumo dume ambao unamkandamiza mwanamke asiweze kupaza sauti kupitia kwenye nafasi ya uongozi hata hivyo hali hiyo ya mfumo dume kadiri miaka inavyokwenda mbele changamoto hiyo inapungua licha ya kwamba bado haijaisha ndani ya jamii.

Licha ya kuwa mjane na kukumbana na changamoto za kunyanyaswa kijinisa na baadhi ya wagombea na wapiga kura lakini haikumkatisha tamaa, licha ya kwamba maneno aliyokuwa akikashifiwa nayo yalimuumiza sana lakini alivumilia.Huyo siyo mwingine bali ni mwenyekiti wa mtaa wa Bamba Halmashauri ya Mji Kibaha Mkoani Pwani Mboni Mkomwa kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambaye alishinda kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika mwishoni mwa mwaka 2024 ambapo alishinda akiwa ni mgombea pekee kwani hakukuwa na mgombea kutoka vyama vya upinzani.

Mboni alisema kuwa alipata kashfa sana wakati wanaendelea na kampeni ndani ya chama ilifika wakati alitaka hata kujitoa kwenye uchaguzi sababu hakuwahi kupata kashfa kama hizo kwa kama mtu hana moyo anaweza kujitoa ili aepukanane na kashfa kwa kweli uchaguzi una mambo mengi sana ya kukatisha tamaa kuwa mwanamke hawezi kuongoza na mtaa haujawahi kuongozwa na mwanamke hivyo awaachie wanaume.

“Nilishangaa kuona hata baadhi ya wagombea wenzangu wanaume walikuwa wakinitolea maneno ya kashfa lakini nashukuru wananchi hawakujali kashfa hizo lakini walinipa kura za kutosha na kuwashinda wanaumewawili na sisi wanawake tulikuwa wawili ambao tulikuwa tunashindana nao,”alisema Mkomwa.

Kwenye uchaguzi huo wa ndani ya chama Mkomwa alipata kura 269 aliyemfuatia alikuwa mwanaume aliyepata kura 171 huku mwanamke mwenzake akipata kura 93 na kumfanya apate nafasi ya kukiwakilisha chama kwenye uchaguzi wa serikali ya mtaa huo na yeye kuwa mshindi.  

“Suala la rushwa ikiwemo ya ngonio kipindi cha uchaguzi ipo lakini mimi nilifanya kampeni bila ya kutoa fedha niliwaambia wanichague niwaletee maendeleo lakini fedha za kuwapa sina nashukuru walinielewa na kunipa nafasi hiyo na kuwanyima wanaume ambao walijivunia jinsi yao,”alisema Mkomwa.     

Alisema kuwa wakati akiomba kura aliweka vipaumbele ambavyo atavifanyia kazi wakati wa uongozi wake ni pamoja na ujezi wa vyoo vya shule ya sekondari Bamba inakamilika ili mwaka huu 2025 ifunguliwe na kupokea wanafunzi zaidi ya 100 wa mtaa huo ambao wanasoma shule za sekondari za mbali ambapo hutembea umbali wa kilometa sita kwenda na kurudi shuleni. 

Alisema kuwa wanaishukuru serikali ambayo ilitoa kiasi cha shilingi milioni 50 kwa ajili ya ujenzi huo pia wananchi nao walichangia kila kaya 2,000 na kufanikisha ujenzi huo kufikia hapo na kubaki hatua ndogo ili ianze ikiwa ni ukosefu wa matundu nane.

“Tuliomba tena fedha Halmashauri milioni 12 kwa matundu sita ila walituambia kuwa tusubiri na wanafunzi waendelee kusoma huko lakini mara fedha zitakapoingia wanafunzia hao watahamishiwa shuleni hapo ndiyo tunasubiri tunataka wanafunzi wanaotoka kwenye mtaa wetu waanze kusoma hapo pia itasaidia maeneo ya mitaa jirani ambao nao watanufaika,”alisema Mkomwa.

Alisema kuwa changamoto nyingine ambayo iko kwenye mipango yake katika kuitatua ni baadhi ya wakazi wa mtaa wake wapatao 23 hawana huduma ya maji kabisa hali ambayo inawasababisha kupata shida ya kupata maji kwa ajili ya matumizi mbalimbali ya kawaida.

Alisema kuwa jambo lingine ni kuwa na stendi  ya mabasi kwani sasa hakuna sehemu nzuri ya mabasi kugeuzia ambapo Kongowe ni mwisho wa ruti za baadhi ya mabasi huwa yanageuzia hapo hivyo wanaongea na Wakala wa Barabara Tanzania Tanroads kuwapatia eneo la hifadhi ya barabara kwenye kituo cha mafuta cha Tawaqal kuwa na stendi hapo na ndoto yake pia ni kujenga zahanati kwenye mtaa huo ndiyo ndoto yake kabla hajamaliza uongozi wake.

“Hivi ni baadhi ya vipaumbele ambavyo nilijiwekea na haya yametokana nay ale wananchi waliyokuwa wakiayuliza kipindi cha kampeni ndiyo nimeanza nayo lakini uongozi wangu utakuwa shirikishi kwani wananchi wao ndiyo watakaokubaliana tuende na jambo gani la kimaendeleo,”alisema Mkomwa.

Alisema kuwa yeye alikuwa mjumbe wa serikali ya mtaa huo kwa kipindi cha miaka mitano na alikuwa pia Mwenyekiti wa Umoja wa wanawake Tanzania (UWT) tawi la Bamba na alikuwa akitumiwa akimwakilisha mwenyekiti aliyepita ambaye ni marahemu Majid Kavuta ndiyo aliyemhamasisha kuwa kiongozi na hata watu walikuwa wakimwambia agombee nafasi hiyo.

“Pia Rais Dk Samia Suluhu Hassan alinihamasisha sana kuwa kiongozi kutokana na jinsi anavyoongoza nchi na Spika wa Bunge Tulia Akson naye ni moja ya watu waliokuwa kioo kwangu na moja ya vitu vilivyonifanya nichaguliwe ni jinsi nilivyokuwa nawasaidia wananchi na ilinibidi niingie kwenye siasa baada ya mume wangu kufariki dunia nikasema sasa nitajiliwaza wapi ndiyo kuingia japo ndugu zangu hawakupenda mimi kuingia kwenye siasa,”alisema Mkomwa.

Alibainisha akiwa mjumbe wa serikali ya mtaa na kiongozi wa UWT alisaidia sana wanawake na vijana na watu wenye ulemavu kupata mikopo ya Halmashauri ya asilimia 10 na moyo wa kuwasaidia pindi wajapo ofisini na alikuwa akisaidia vijana ikiwa ni pamoja na kwenye msuala ya michezo na vijana walimwambia wanataka awe mlezi wa mtaa huo ili awasidie.

“Nawasihi wanawake wasiwe na hofu ya kuwania nafasi ya uongozi wapambanie ndoto zao ili kufikia malengo waliyojiwekea na waachane na maneno ya kukatoisha tamaa kwani uongozi hauangalii jinsi bali ni utekelezaji wa majukumu na kufuata miongozo taratibu sheria na kanuni za uongozi zilizowekwa,”alisema Mkomwa.  

Akizungumzia juu ya mwenyekiti huyo Simon Mbelwa alisema kuwa mtaa huo umepata kiongozi mzuri na alikuwa karibu na wananchi hivyo wamepata kiozi sahihi kwani ni msikivu na mpenda maendeleo anaamini kuwa ataufiukisha mbali mtaa huo.

Mbelwa alisema kuwa kiongozi huyo ana uzoefu mkubwa kwani kabla ya ksuhika nafasi hiyo alikuwa mjumbe hivyo anajua changamoto za wananchi na jinsi gani atazitatua kwa kupitia mipango na ushirikishaji wananchi kupitia vikao vya mtaa.

Kwa upande wake Swaiba Kazi alisema kuwa wanawake ni viongozi wenye uwezo mkubwa na dhana kuwa mwanamke hana uwezo si ya kweli na haipaswi kuungwa mkono na wanaweke wameonyesha gani kiongozi anatakiwa afanye.Kazi alisema kuwa wanwake wana uwezo mzuri wa kuongoza na ndiyo sababu wameaminika na kupewa nafasi hizo za juu kuanzia ngazi za chini hadi Uras hivyo wanapaswa kuungwa mkono na siyo kuwavunja moyo na mtaa huo una jumla ya wananchi 7,546 ana watoto watatu na ni mjasiriamali.    Mwisho.  

Monday, January 6, 2025

MTAA WA MIEMBE SABA WAWEKA VIFUSI KUBORESHA BARABARA YA MTAA


MTAA wa Miembe Saba B Wilayani Kibaha Mkoani Pwani umezanza zoezi la kuweka vifusi kwenye barabara ya Mtaa ili kuwaondolea kero wananchi wa Mtaa huo.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Mwenyekiti wa Mtaa huo Nuru Awadhi amesema kuwa barabara hiyo yenye urefu wa kilometa saba imeharibika sana kutokana na kuharibiwa na mvua kubwa zilizonyesha mwaka jana.

Awadhi amesema kuwa wameanza kusambaza vifusi hivyo ambavyo wameviomba kutoka kwa wadau mbalimbali wa maendeleo wa mtaa huo ili kufanikisha uboreshaji wa barabara hiyo ya vumbi.

"Nawashukuru wadau wa maendeleo katika mtaa ambao wamejitolea kupatikana kwa kifusi hichi ambacho kitatusaidia ili kupunguza kero kwa wananchi wanayoitumia barabara hii,"amesema Awadhi.

Amesema kuwa wameweka kifusi sehemu na bado kinahitajika kifusi zaidi ambapo tunaweka kwanza kwenye maeneo korofi ili kupunguza changamoto ya ubovu wa barabara.

"Tumepata changamoto kubwa ya ubovu wa barabara kwani sisi kwa bahati mbaya barabara yetu haikuchongwa kama baadhi ya barabara za mitaa mingine zilibahatika kuchongwa hivyo kupunguza athari za ubovu tofauti na kwetu,"amesema Awadhi.

Aidha amesema kuwa wanaendelea kuwahamasisha wananchi kuendelea kusaidia ili wakabiliane na changamotro hiyo ili kuongeza vifusi zaidi ili kuweza kuvisambaza kwenye barabara yote.

"Tuliongea na diwani ambapo alisema watafanya mpango wa kutuletea greda lakini majibu ni kuwa ni bovu hivyo tutatasubiri hadi litengenezwe ndipo tulilete kwetu lakini hiyo itakuwa ni muda mrefu ndipo tukaona njia ya haraka ni kumwaga kwanza kifusi kwenye sehemu korofi,"amesema Awadhi.

Aliongeza kuwa wao walipata bahati mbaya kutochongewa barabara yao lakini mitaa mingine ilichongewa barabara zao ambazo zilichongwa mwaka jana angalau imepunguza changamoto za ubovu.

"Mtaa wetu una wananchi zaidi ya 4,000 hivyo kila mmoja wetu akipambana tutaweza kuboresha miundombinu yetu ya barabara ambapo kuna shule za Msingi tatu na moja ya sekondari hivyo inaonyesha jinsi gani changamoto ya ubovu wa barabara inavyokuwa shida,"amesema Awadhi.

Sunday, January 5, 2025

WAHUKUMIWA MAISHA NA MIAKA 20 KWA UKATILI WA KIJINSIA

WATUHUMIWA wawili Mkoani Pwani waliokuwa wanakabiliwa kwa kesi za ukatili wa kijinsia wamehukimiwa vifungo tofauti ambapo mmoja amefungwa kifungo cha maisha jela na mwingine amefungwa kifungo cha miaka 20 jela.

Aidha jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani lilipeleka Mahakamani kesi 125 za makosa mbalimbali ambapo kati ya kesi hizo 47 zimepata mafanikio kwa watuhumiwa kuhukumiwa vifungo mbalimbali.

Hayo yamesemwa Mjini Kibaha na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani ACP Salim Morcase alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari juu ya mafanikio ya jeshi hilo kwa kipindi cha mwezi Disemba 2024.

Morcase amesema kuwa jumla ya kesi za ukatili wa kijinsia kulikuwa na kesi tano za makosa ya kubaka na kulawiti.

"Watuhumiwa hao wawili walipata adhabu hizo ambapo wa kwanza alipatikana na hatia ya kubaka na kulawiti na wa pili alikutwa na hatia ya unyanyasaji wa kingono,"amesema Morcase.

Amesema kuwa watuhumiwa 52 wamehukumiwa vifungo tofauti tofauti kutokana na aina ya makosa yaliyokuwa yakiwakabili.

MADEREVA 11 MKOANI PWANIWAFUNGIWA LESENI

JUMLA ya makosa 17,246 ya usalama barabarani yamekamatwa huku madereva 11 wakifungiwa leseni zao Mkoani Pwani kwa makosa mbalimbali waliyoyafanya wakiwa barabarani.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Mjini Kibaha Kamanda wa Polisi Mkoani Pwani ACP Salim Morcase amesema madereva hao wamefungiwa leseni kwa mujibu wa sheria.

Morcase amesema kuwa madereva hao walifungiwa leseni kwa makosa ya kuendesha magari wakiwa wamelewa, kuendesha magari kwa uzembe na kuyapita magari mengine pasipo kuchukua tahadhari.

"Madereva wengine 24 walifikishwa mahakamani kwa makosa ya kupandisha abiria kwenye magari ambayo yanapelekwa nje ya nchi IT na kusababisha ajali za barababani,"amesema Morcase.

Amesema kuwa madereva hao walifikishwa mahakamani kwa mujibu wa kifungu cha 28 (3) (b) cha Sheria ya usalama barabarani sura ya 168 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2022. 

"Tumetoa elimu ya usalama barabarani kwa makundi mbalimbali, bodaboda, madereva wa mabasi makubwa, madereva wa mabasi madogo na madereva wa magari ya shule,"amesema Morcase.

Ameongeza kuwa wametoa elimu madereva wa pikipiki 4,293 katika vijiwe 199 vya pikipiki na abiria wa mabasi makubwa na madogo wapatao 13,094 kwenye maeneo mbalimbali.

"Elimu waliyoipata ni umuhimu wa kufahamu namba za gari unayosafiria, wahudumu wa basi hilo, dereva na kondakta na kufahamu muda wa kuanza safari, umuhimu wa kutoa taarifa kwa mamlaka husika pale abiria anapoona vitendo
vya uvunjifu wa sheria za usalama barabarani ambavyo vitahatarisha usalama,"amesema Morcase.

Amebainisha kuwa pia wamewaelimisha abiria juu ya mwendokasi, kuyapita magari mengine bila ya tahadhari, madhara ya kupakia mizigo ya hatari ndani ya mabasi na kushushwa kwenye basi pale gari linapofika mizani ili lisionekane kama limezidisha uzito.

COREFA KUJENGA OFISI UWANJA WAKE

CHAMA Cha Soka Mkoa wa Pwani (COREFA) kimepata eneo lenye ukubwa wa hekari tano kwa ajili ya ujenzi wa ofisi na uwanja wake.

Hayo yamesemwa Mjini Kibaha na Mwenyekiti wa Corefa Robert Munis alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake.

Munis amesema kuwa eneo hilo ambalo liko Mtaa wa Viziwaziwa wamekabidhiwa na Halmashauri ya Mji Kibaha ambapo tayari wamekabidhiwa barua ya kupewa eneo hilo.

"Tumepewa masharti ya kuhakikisha tunajenga ofisi na uwanja ndani ya muda wa mwaka mmoja tunaishukuru Halmashauri kwa kutupatia eneo hilo na tutahakikisha tunalifanyia kazi,"amesema Munis.

Amesema kuwa lengo ni kuhakikisha Corefa inamiliki uwanja wake ambapo kwa sasa hawana uwanja na ofisi waliyonayo wamepangisha hivyo kuwa na ofisi na uwanja itakuwa jambo zuri.

"Kwa kushirikiana na wajumbe wa bodi ya udhamini inayoongozwa na Waziri wa Viwanda na Uwekezaji Dk Suleiman Jafo watahakikisha ofisi na uwanja vinajengwa kwa muda uliopangwa,"amesema Munis.

Aidha amesema kuwa kamati ya utendaji itakaa kuandaa mipango kuhusiana na namna ya kufanikisha namna ya kuanza ujenzi huo.

"Tunataka tuwe na timu zitakazokuwa zinatumia viwanja vizuri na kuhakikisha tunapandisha timu hadi zifike ligi kuu ambapo kwa sasa Mkoa huo hauna timu yoyote iliyoko ligi kuu,"amesema Munis.

Wakati huo huo imempatia kiasi cha shilingi 100,000 mwandishi wa habari za michezo Abdala Zalala kwa kutambua mchango wake wa kuhamasisha mchezo wa soka ndani ya Mkoa huo.

Kwa upande wake Zalala amesema kuwa anakishukuru chama hicho kwa kutambua mchango wake na kumpa zawadi hiyo na kuahidi kuendelea kuhamasisha soka hasa kwa vijana ndani ya  Mkoa huo bila ya kuchoka.

Zalala amewataka waandishi wa habari wenzake nao kujikita kuandika habari za Soka ili kuinua mchezo huo uweze kutia ajira kwa vijana