Sunday, January 5, 2025

MADEREVA 11 MKOANI PWANIWAFUNGIWA LESENI

JUMLA ya makosa 17,246 ya usalama barabarani yamekamatwa huku madereva 11 wakifungiwa leseni zao Mkoani Pwani kwa makosa mbalimbali waliyoyafanya wakiwa barabarani.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Mjini Kibaha Kamanda wa Polisi Mkoani Pwani ACP Salim Morcase amesema madereva hao wamefungiwa leseni kwa mujibu wa sheria.

Morcase amesema kuwa madereva hao walifungiwa leseni kwa makosa ya kuendesha magari wakiwa wamelewa, kuendesha magari kwa uzembe na kuyapita magari mengine pasipo kuchukua tahadhari.

"Madereva wengine 24 walifikishwa mahakamani kwa makosa ya kupandisha abiria kwenye magari ambayo yanapelekwa nje ya nchi IT na kusababisha ajali za barababani,"amesema Morcase.

Amesema kuwa madereva hao walifikishwa mahakamani kwa mujibu wa kifungu cha 28 (3) (b) cha Sheria ya usalama barabarani sura ya 168 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2022. 

"Tumetoa elimu ya usalama barabarani kwa makundi mbalimbali, bodaboda, madereva wa mabasi makubwa, madereva wa mabasi madogo na madereva wa magari ya shule,"amesema Morcase.

Ameongeza kuwa wametoa elimu madereva wa pikipiki 4,293 katika vijiwe 199 vya pikipiki na abiria wa mabasi makubwa na madogo wapatao 13,094 kwenye maeneo mbalimbali.

"Elimu waliyoipata ni umuhimu wa kufahamu namba za gari unayosafiria, wahudumu wa basi hilo, dereva na kondakta na kufahamu muda wa kuanza safari, umuhimu wa kutoa taarifa kwa mamlaka husika pale abiria anapoona vitendo
vya uvunjifu wa sheria za usalama barabarani ambavyo vitahatarisha usalama,"amesema Morcase.

Amebainisha kuwa pia wamewaelimisha abiria juu ya mwendokasi, kuyapita magari mengine bila ya tahadhari, madhara ya kupakia mizigo ya hatari ndani ya mabasi na kushushwa kwenye basi pale gari linapofika mizani ili lisionekane kama limezidisha uzito.

No comments:

Post a Comment