MBUNGE wa Jimbo la Kibaha Mjini Silvestry Koka ameishukuru Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Dk Samia Suluhu Hassan kuipandisha hadhi Halmashauri ya Mji Kibaha kuwa Manispaa.
Koka ametoa shukrani hizo Mjini Kibaha wakati wa Mkutano wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Pwani kuunga mkono azimio la Mkutano Mkuu wa (CCM) Taifa kumpitisha Rais Dk Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea pekee wa kiti cha Urais kupitia chama hicho kwenye uchaguzi Mkuu wa mwaka huu na kumbukumbu ya kuzaliwa Rais.
Aidha Mbunge huyo amepongeza kuteuliwa Dk Hussein Mwinyi kuwa mgombea Urais kwa tiketi ya CCM Zanzibar na kuchaguliwa kwa Dk Emanuel Nchimbi kuwa Mgombea Mwenza na Steven Wasira kuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM.
Amesema kuwa hicho kilikuwa ni kilio chao kwa miaka mingi hivyo kupandishwa hadhi kwa Kibaha kutachochea maendeleo kwa wananchi kwani hata bajeti itakuwa ni kubwa na hata maslahi kwa watumishi wa umma.
Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mohamed Mchengerwa ametangaza rasmi hali ambayo ilizua furaha kubwa na amesema kuwa suala hilo ni jambo ambalo lililokuwa likisubiriwa kwa muda mrefu na sasa limekuwa.
Mchengerwa amesema kuwa kulikuwa hakuna sababu ya kutokuwa Manispaa lakini sasa wakati umefika na sasa Serikali imeridhia Mji wa Kibaha kuwa Manispaa ambapo ni makao makuu ya Mkoa wa Pwani.
No comments:
Post a Comment