Thursday, January 9, 2025

LICHA YA UNYNANYASAJI KIJINSIA NURU AWADH AWAANGUSHA VIGOGO WANAUME



WANAWAKE wanaowania nafasi za uongozi wanakabiliwa na changamoto za unyanyasaji wa kijinsia kutokana na baadhi ya watu au wagombea kuwa kejeli kuwa hawana uwezo wa kuongoza wao kazi yao ni kulea, kupika kumhudumia mume,”alisema Nuru Awadh.

Hiyo ni baadhi ya misemo wanayokutana nayo wanwake wanapoingia kwenye kuwania nafasi mbalimbali za uongozi dhana ambayo imekuwa ikiwakatisha tamaa baadhi ya wanawake hivyo kushindwa kujiingiza kwenye kuwania nafasi za uongozi.

Baadhi ya wanawake wameshindwa kuendelea na siasa au kuwania nafasi za uongozi wamekuwa wakizuliwa kashfa kuwa ni wahuni tu jambo ambalo siyo la kweli kwani wao nao wana uwezo wa kuongoza kama ilivyo kwa wanaume.Hayo ni maneno ambayo ymesmwa na Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Miembe saba B Nuru Awadh kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) wakati akiongea na mwandishi wa habari wa gazeti la HabariLeo ofisini kwake alisema kuwa ukatili wa kijinsia na mfumo dume bado upo na una warudisha nyuma wanwake kuwania nafasi za uongozi  au kuingia kwenye siasa.

Kuna dhana imejengeka kuwa kiongozi lazima awe mwanaume na mwanamke hawezi kuwa kiongozi hali hiyo imekuwa ikiwarudisha nyuma wanawake ambapo jamii inapaswa iikemee na kuwapa wanwake nafasi sawa na wanaume.

“Namshukuru mama alinipambania nipate elimu lakini kwa upande wa baba hakuwa na msukumo kwa watoto wa kike kupata elimu hali ambayo ilisababisha nishindwe kwenda chuo cha ualimu baada ya kumaliza elimu ya sekondari,”alisema Awadh.

Awadh alisema kuwa wakati wa kuwania nafasi ya uenyekiti alikutana na unyanyasaji wa kijinisa kwani watu walimtolea kila aina ya kashfa lakini alipambana kwani alijua ni masuala ya kisiasa tu ili kumharibia asishinde kuanzia ndani ya chama hadi kwenye uchaguzi wa mtaa ambapo alishindana na kiongozi kutoka chama cha Chadema na yeye kumshinda na alikuwa mwanaume.

Alisema kuwa wanaume waachane na mfumo dume kwani unarudisha nyuma maendeleo kwani kuna viongozi wazuri wanawake na wana uwezo mkubwa wa kuongoza kuliko hata wanaume hivyo wasitumie nafasi hiyo kuwakandamiza wanawake.

“Nimetolewa maneno mengi ya kashfa na watu wa kawaida na baadhi ni viongozi ili tu kunidhoofisha lakini sikukata tamaa niliendelea kupambana na kushinda namshukuru na mume wangu kwani alinipa moyo na aliendelea kuniunga mkono hadi nikafanikiwa kushinda lakini kama huna moyo unaweza kuacha siasa,”alisema Awadh.

Alisema kuwa mume wake alipambana na kuna wakati alimuombea kura kwenye maeneo mbalimbali na hata wakati wa kampeni aliambatana naye ili kumsaidia aweze kushinda kwenye nafasi hiyo ya uenyekiti hivyo kumpa moyo na kutokata tamaa na hata kumsaidia kuhudumia watoto wakati yeye anapokuwa anayatekeleza majukumu yake.

Alisema kuwa amekuwa akitenga muda wa kuhudumia jamii na kuhudumia familia yake kwani anahakikisha kila kitu kinakwenda sawa na pia anatenga siku kwa ajili ya kwenda ofisini hasa ikizingatiwa kuwa yeye ni mjasiriamali ambapo hutenga muda kwa majukumu yote hayo bila kuathiri sehemu nyingine.

“Baada ya kushinda mikakati au malengo yangu ni kuhakikisha tunaboresha barabara ya Mtaa ambayo imeharibika sana na tumeanza kuweka vifusi sehemu korofi ila matarajio ni kuichonga kwani licha ya mvua kunyesha na kuiharibu haikubahatika kuchongwa hivyo kuwa kwenye hali mbaya,”alisema Awadh.

Alisema kuwa kipaumbele chake kingine ni ujenzi wa zahanati kwani wanatumia umbali mrefu kwenda kupata huduma za afya ambapo hupata huduma kwenye Zahanati ya Mwendapole ambako ni mbali na hutumia gharama kubwa ambapo ikijengwa hapo itakuwa imewasaidia wakazi wa mtaa huo.

“Malengo yangu mengine kwa kushirikiana na wananchi ni kukabiliana na migogorpo ya ardhi kwani kuna changamoto kubwa ya migogoro hivyo atashirikiana na wajumbe wake kuitatua migogoro hiyo ambayo imekuwa ikiwapotezea watu muda mwingi kuitatua na hiyo ni kero kubwa sana kwenye mtaa wangu,”alisema Awadh.

Aidha alisema kuwa baadhi ya maeneo yana changamoto ya maji hivyo atahakikisha anawasiliana na Dawasa ili watatue changamoto kwenye baadhi ya maeneo ili wananchi waweze kupata huduma hiyo kwa karibu na suala la mawasiliano kuna maeneo hayapati mawasiliano ya simu na kusababisha kero kwa wananchi.

“Katika kukabiliana na changamoto ndani ya mtaa nimeteua kamati ambazo zitafutailia changamoto hizo kulingana na sekta na kero hizo nilizipata wakati wa kampeni na uongozi utakuwa shirikisha kwa kuwashirikisha wananchi ambapo kwa sasa bado hatujakaa mkutano wa mtaa hivyo tunaanza kutatua kupitia kero tulizozipata wakati ule,”alisema Awadh. Alibainisha kuwa wananchi walimpa kura na kusema kuwa wamewapa uongozi wanaume kwa vipindi viwili hivyo ni wakati wa wanawake sasa kuongoza na anajivunia Rais Dk Samia Suluhu Hassan kwa uongozi wake nao ni chachu ya yeye kuingia kwenye nafasi hiyo ili naye aweze kuwasidia wananchi kutatua kero akiwa kama muongoza njia.

No comments:

Post a Comment