TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Pwani imefanikiwa kuongeza makusanyo kutoka kiasi cha shilingi milioni 4.6 hadi 12 kwa wiki kwenye kizuizi cha Maliasili cha Wilaya ya Kibiti.
Aidha kutokana na kuongezeka kwa mapato hayo kwa mwaka mmoja kupitia kizuizi hicho Maliasi watakuwa na uwezo wa kukusanya kiasi cha shilingi milioni 480 kwa mwaka.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Pwani Alli Sadiki alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake juu ya mafanikio yaliyopatikana kipindi cha miezi mitatu iliyopita kuanzia Oktoba hadi Disemba mwaka jana.
Sadiki amesema kuwa mafanikio ya makusanyo hayo yamefikiwa baada ya Takukuru kufanya uzuiaji katika mfumo wa ukusanyaji wa mapato kwa kutumia mashine ya Pos.
"Uzuiaji huo ulikuja baada ya taasisi hiyo kutoridhishwa na ukusanyaji mapato kwani yalikuwa ni madogo kulingana na uwezo mkubwa wa kizuizi hicho,"amesema Sadiki.
Amesema kuwa Takukuru ilisimamia ukusanyaji kuanzia Novemba 5 mwaka 2024 hadi Novemba 11 mwaka huo kwa saa 24 na kufanikiwa kukusanya kiasi hicho cha shilingi milioni 12 badala ya shilingi milioni 4.6 kwa wiki moja.
Aidha amesema kuwa walibaini kuwa baadhi ya wakusanyaji ushuru walipewa fedha na wenye mizigo ili wasitozwe malipo ya serikali, baadhi ya magari hayakukaguliwa hivyo kukwepa kulipa ushuru, baadhi ya wakusanyaji kupewa mwanya ukadiriaji wa chini wa malipo.
Pia katika kipindi hicho walifanya ufuatiliaji wa miradi 52 ya maendeleo yenye thamani ya shilingi bilioni 12 ambapo hakukuwa na mapungufu huku mingine ikiwa inaendelea na utekelezaji.
Ameongeza kuwa miradi hiyo ni ya sekta za afya, elimu, maji, barabara na katika uelimishaji umma wamefanya semina, mikutano ya hadhara, vipindi vya redio, kuimarisha klabu za wapinga rushwa na Takukuru Rafiki ambapo wamezifikia kata 11.
"Katika kipindi hicho Takukuru ilifungua kesi 24 mahakamani ambapo washitakiwa 13 wametiwa hatiani na tulipokea malalamiko 60 kati ya hayo 37 yalihusu rushwa na yanafanyiwa kazi yakiwa kwenye hatua mbalimbali,"amesema Sadiki.
Ametoa wito kwa wananchi wa Mkoa huo kuendelea kuunga mkono jitihada za mapambano dhidi ya rushwa kwa kuwafichua wale wanaoshiriki vitendo vya rushwa.
No comments:
Post a Comment