Friday, February 7, 2025

KITUO CHA AFYA VIGWAZA MBIONI KUKAMILIKA

KITUO cha afya cha Kata ya Vigwaza Halmashauri ya Chalinze Wilaya ya Bagamoyo Mkoani Pwani kiko kwenye hatua za mwisho kukamilika ambapo kitatoa huduma mbalimbali zikiwemo za upasuaji hivyo kuwaondolea kero za akinamama za kujifungua.

Aidha serikali imetoa kiasi cha shilingi milioni 525 kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho cha afya kwenye Kata hiyo hivyo kuondoa changamoto hasa za mama wajawazito wakati wa kujifungua.
 
Diwani wa Kata ya Vigwaza Mussa Gama akizungumza Vigwaza wakati wa maadhimisho ya miaka 48 ya kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) amesema kwa sasa wananchi hususani wanawake waliokuwa wanashindwa kujifungulia kwenye Zahanati ya Vigwaza ambapo hawatapelekwa tena Mlandizi na Chalinze kupata huduma hizo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) Lulu Rajabu kata ya Vigwaza amesema wanawake walikuwa wakikumbana na adha ya kutembea kilometa tisa na zaidi kipindi wanaposhindwa kujifungulia kwenye Zahanati.

Katika maadhimisho hayo wanachama wa CCM kutoka maeneo mbalimbali ya kata hiyo walioshiriki kupanda miti kwenye kituo hicho sambamba na kufanya harambee ya ujenzi wa ofisi ya chama ambapo zaidi ya milioni tatu zilichangwa 


No comments:

Post a Comment