WANANCHI wa Mkoa wa Pwani wametakiwa kutumia fursa za kiuchumi kwa kuwashwa mwenge wa uhuru mkoani humo Aprili 2 mwaka huu.
Hayo yamesemwa jana Mjini Kibaha na Mkuu wa Mkoa huo Abubakar Kunenge alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake.
Amesema kuwa kuwashwa mwenge wa uhuru Mkoani Pwani ni fursa kiuchumi kwa wananchi pia ni chachu ya maendeleo kwani wananchi watafanya biashara za chakula, malazi, usafiri, vinywaji na utalii.
"Wananchi tumieni fursa hiyo ya uzinduzi wa mbio hizo za mwenge wa uhuru kwa kufanyabiashara ambapo kutakuwa na wageni wengi na hata wenyeji ambao watahitaji huduma mbalimbali,"amesema Kunenge.
Amesema kuwa sherehe hizo za uzinduzi zitapambwa na matukio mengi yakiwemo ya halaiki na burudani nyingine za wasanii.
"Baada ya uzinduzi huo mwenge wa uhuru utakimbizwa katika Halmashauri tisa za mkoa huo ambapo utakagua, kutembelea na kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo,"amesema Kunenge.
Aidha amewahamasisha na kuwaomba wananchi wote wa Mkoa wa Pwani na maeneo jirani kujitokeza kwa wingi kushiriki katika uzinduzi huo.
"Maandalizi yanaendelea vizuri ambapo muda bado unatosha na mwaka huu tumejipanga vyema kuhakikisha tunafanya vizuri,"amesema Kunenge.
mwisho.
No comments:
Post a Comment