Saturday, February 15, 2025

WAZIRI KABUDI ATAKA WATANGAZAJI KUACHA MBWEMBWE WATUMIE KISWAHILI SANIFU

WAZIRI wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Profesa Kabudi amewataka watangazaji kuacha mbwembwe na kubananga Kiswahili na kutumia Kiswahili Sanifu ili Tanzania iendelee kuwa nchi inayotumia Kiswahili fasaha.

Profesa Kabudi ameyasema hayo Mjini Dodoma wakati akifungua mkutano wa mwaka wa vyombo vya utangazaji nchini.

Amesema kuwa Tanzania ni nchi kinara wa lugha ya Kiswahili lakini endapo hakutakuwa na juhudi za makusudi za kukisimamia Kiswahili hatutakuwa vinara tena wa lugha hiyo.

"Watangazaji wanapaswa kutumia Kiswahili fasaha na sanifu kwani tuna utajiri wa misamiati hivyo tukitumie vizuri ili kuandaa vipindi vyenye tija kwa wasikilizaji,"amesema Kabudi.

Naye Mkurugenzi wa Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Dk Jabiri Bakari amesema kuwa wamekuwa wakifanya utafiti juu ya maudhui ya mtandaoni ili kutoa taarifa sahihi na za umahiri.

Bakari amesema kuwa kuna utafiti umefanywa ambapo utakamilika mwezi huu lengo kuu likiwa ni kuboresha utoaji wa maudhui mitandaoni.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Maudhui Saida Muki amesema kuwa watangazaji wa maudhui mitandaoni wanapaswa kuweka maslahi ya nchi mbele  na kujiepusha na maudhui yanayokiuka maadili.

 

No comments:

Post a Comment