NAIBU Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Hamis Mwinjuma amevitaka vyombo vya habari kuandika habari sahihi kipindi cha uchaguzi ili kudumisha amani.Ameyasema hayo Mjini Dodoma alipokuwa akifunga Mkutano wa Mwaka wa Vyombo vya Utangazaji Nchini.
Mwinjuma amesema kuwa vyombo vya habari vina nafasi kubwa ya kutoa taarifa sahihi ambazo zitawafanya wananchi kuchagua viongozi bora ambao watailetea nchi maendeleo.
"Kazi yenu kubwa ni kutoa taarifa sahihi kwa wananchi ambao wanaviamini vyombo vya habari kupata taarifa za ukweli na siyo za kupotosha ili kupata viongozi bora,"amesema Mwinjuma.
Kwa upande wake Mhandisi Endrew Kisaka ambaye alimwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) amesema kuwa vyombo vya habari vinapaswa kuandika habari za vyama vya siasa wakati wa uchaguzi bila ya upendeleo.
Kisaka amesema kuwa waandishi wazingatie kuandika sera na siyo majibizano au udini, ukabila na kutoingilia faragha za watu na kotoegemea upande wowote bali watoe nafasi kwa watu wote.
Naye katibu wa Mtandao wa Bloggers Tanzania (TBN) Khadija Kalili ameishukuru TCRA na kuiomba kupunguza gharama za usajili ambapo kwa sasa ni shilingi 500,000 ambayo ni kubwa hivyo wengi kushindwa kulipia.
Kalili alisema kuwa TBN ilisajiliwa mwaka 2015 na ilianza na wanachama 100 hadi kufikia 300 ambapo baadhi walijitoa kutokana na kushindwa kusajili.
Mkutano huo wa mwaka ambao uliansaliwa na TCRA ulihusisha washiriki 528 ambao wanajihusisha na masuala ya utangazaji na watoaji maudhui mtandaoni nchini, waandishi wakongwe wa Redio Tanzania.
No comments:
Post a Comment