Sunday, February 9, 2025

KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA TAMISEMI YARIDHISHWA MIRADI YA ELIMU NA AFYA HALMASHAURI YA MJI KIBAHA





KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) imekagua miradi ya ikiwemo ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Mji Kibaha iliyogharimu kiasi cha shilingi bilioni 4.1.

Hayo yamesemwa na Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Mji Kibaha Catherine Saguti kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashari wakati akitoa taarifa juu ya ujenzi wa hospitali hiyo.

Dk Saguti amesema kuwa mapokezi ya fedha za mradi wa Ujenzi wa Hospitali na ununuzi wa vifaa tiba kutoka Serikali Kuu yalitolewa kwa awamu nne 
jumla ya shilingi bilioni 3.3 kwa ajli ya ujenzi na shilingi milioni 400  kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba. 

"Fedha hizo zimepokelewa kwa awamu kuanzia mwaka wa fedha 2019/2020, 2020/2021, 2021/2022 na 2024/25 na jumla ya majengo ambayo yamejengwa hadi sasa ni 14 na majengo 11 yamekamilika na yanatumika huku majengo matatu yanaendelea na utekelezaji katika hatua ya
ukamilishaji,"amesema Saguti.

Amesema kuwa Halmashauri imechangia jumla ya shilingi milioni 446.7 kwa ajili ya ukamilishaji wa
miundombinu na majengo ambayo hayakukamilika kwa fedha za Serikali Kuu.

Pia kamati hiyo imetembelea ujenzi wa kituo cha afya cha Kata ya Pangani kilichogharimu kiasi cha shilingi milioni 914 huku Halmashauri ya Mji Kibaha ikichangia kiasi cha shilingi milioni 189 kutokana na mapato ya ndani.

Wabunge hao wa Kamati ya Tamisemi walitembelea mradi wa shule mpya ya sekondari ya Kata ya Tangini iliyogharimu kiasi cha shilingi milioni 528.9.

Ujenzi huo umetokana na mradi wa Uboreshaji wa Elimu ya Sekondari (SEQUIP) ina uwezo wa kuchukua wanafunzi 398 wa kidato cha kwanza na cha pili wanawake 191 na wanaume 207.

Katika hatua nyingine kamati hiyo ya kudumu ya Bunge ya Tamisemi pia ilitembelea ujenzi wa Shule ya Msingi Mtakuja Kata ya Pangani ambayo ina mfumo wa Kiingereza ambayo imegharimu kiasi cha shilingi milioni 309.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Zainab Katimba amesema kuwa serikali ya awamu ya sita imewekeza fedha nyingi kwenye miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ya afya na elimu.

Katimba amesema kuwa Serikali imewekeza kwenye miradi mingi ili kuwaletea wananchi huduma karibu na maendeleo ili kupunguza changamoto.

Amesema kuwa maagizo na maelekezo yaliyotolewa na kamati ili kuboresha miradi hiyo wataifanyia kazi ili iwe na ubora na kuwa na manufaa kwa wananchi.  

Akitoa majumuisho ya ziara ya Kamati Mwenyekiti wa kamati hiyo Justin Kamoga amesema wameridhishwa na ujenzi wa miradi hiyo kwani imejengwa kwa viwango vizuri.

Kamoga amesema licha ya miradi hiyo kujengwa vizuri lakini kuna baadhi ya changamoto ndogo ndogo ikiwa ni pamoja na kukamilisha baadhi ya maeneo yaliyobakia.

No comments:

Post a Comment