Saturday, January 4, 2025

JESHI LA POLISI MKOANI PWANI LIMEKAMATA WATU 173 KWA TUHUMA ZA MAKOSA MBALIMBALI



WATUHUMIWA 173 wamekamatwa Mkoani Pwani kutokana na makosa mbalimbali ikiwa ni pamoja na nyaya za Shaba kilogramu 3,687.

Aidha kati yao watu wanne wamekamatwa kwa tuhuma ya kukutwa na meno ya Tembo nane yanayokadiriwa kuwa uzito wa kilogramu 67.

Hayo yamesemwa na Kamanda wa Polisi (ACP) Salim Morcase alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Mjini Kibaha kuelezea mafanikio ya misako na operesheni. 

Morcase amesema kuwa watuhumiwa hao walikamatwa katika kipindi cha mwezi Desemba mwaka jana 2024.

"Pia watuhumiwa hao walikamatwa na mafuta ya mafuta ya transfoma lita 80, mafuta ya dizeli lita 3,547, mitungi ya gesi 10, madawati 15 ya Shule ya Msingi Kibadagwe, mafuta ya kula dumu 45 sawa na lita 900,"amesema Morcase.

Amesema kuwa watuhumiwa 54 wamekamatwa kwa tuhuma za kukutwa na bhangi kilogramu 3 na gramu 120.5, mirungi kilogramu 7 na gramu 40, pia watuhumiwa 44 wakikamatwa na pombe ya moshi lita 86 na mtambo wa kupikia pombe hiyo.

"Watuhumiwa wengine walikamatwa na vitu mbalimbali vikiwemo injini ya gari aina ya Corolla, pikipiki 35, simu za mkononi 13, nondo 35 na vipande 12, kompyuta mpakato 1, redio 1, spika 2, vitanda 2 na magodoro yake na mabomba ya chuma 5,"amesema Morcase.

Akizungumzia kuhusu nyara za Serikali amesema watu wanne walikamatwa na nyama ya Swala vipande nane vyenye uzito wa kilogramu 32, vichwa vitano na miguu ya Tohe.

"Pia watu saba wamekamatwa kwa tuhuma za kuiba ngombe sita wenye thamani ya shilingi milioni 8.1 ambapo ngombe hao tumewaokoa,"amesema Morcase.

Amewataka wananchi kuendelea kutoa taarifa zinazohusu uhalifu na wahalifu kwa viongozi wa serikali za mitaa watendaji wa kata au kwa wakaguzi kata waliopo kwenye kata zao.






No comments:

Post a Comment