Sunday, January 5, 2025

COREFA KUJENGA OFISI UWANJA WAKE

CHAMA Cha Soka Mkoa wa Pwani (COREFA) kimepata eneo lenye ukubwa wa hekari tano kwa ajili ya ujenzi wa ofisi na uwanja wake.

Hayo yamesemwa Mjini Kibaha na Mwenyekiti wa Corefa Robert Munis alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake.

Munis amesema kuwa eneo hilo ambalo liko Mtaa wa Viziwaziwa wamekabidhiwa na Halmashauri ya Mji Kibaha ambapo tayari wamekabidhiwa barua ya kupewa eneo hilo.

"Tumepewa masharti ya kuhakikisha tunajenga ofisi na uwanja ndani ya muda wa mwaka mmoja tunaishukuru Halmashauri kwa kutupatia eneo hilo na tutahakikisha tunalifanyia kazi,"amesema Munis.

Amesema kuwa lengo ni kuhakikisha Corefa inamiliki uwanja wake ambapo kwa sasa hawana uwanja na ofisi waliyonayo wamepangisha hivyo kuwa na ofisi na uwanja itakuwa jambo zuri.

"Kwa kushirikiana na wajumbe wa bodi ya udhamini inayoongozwa na Waziri wa Viwanda na Uwekezaji Dk Suleiman Jafo watahakikisha ofisi na uwanja vinajengwa kwa muda uliopangwa,"amesema Munis.

Aidha amesema kuwa kamati ya utendaji itakaa kuandaa mipango kuhusiana na namna ya kufanikisha namna ya kuanza ujenzi huo.

"Tunataka tuwe na timu zitakazokuwa zinatumia viwanja vizuri na kuhakikisha tunapandisha timu hadi zifike ligi kuu ambapo kwa sasa Mkoa huo hauna timu yoyote iliyoko ligi kuu,"amesema Munis.

Wakati huo huo imempatia kiasi cha shilingi 100,000 mwandishi wa habari za michezo Abdala Zalala kwa kutambua mchango wake wa kuhamasisha mchezo wa soka ndani ya Mkoa huo.

Kwa upande wake Zalala amesema kuwa anakishukuru chama hicho kwa kutambua mchango wake na kumpa zawadi hiyo na kuahidi kuendelea kuhamasisha soka hasa kwa vijana ndani ya  Mkoa huo bila ya kuchoka.

Zalala amewataka waandishi wa habari wenzake nao kujikita kuandika habari za Soka ili kuinua mchezo huo uweze kutia ajira kwa vijana

No comments:

Post a Comment