Saturday, April 6, 2024

MTAA WA KWAMFIPA WAANZA UJENZI WA SEKONDARI

MTAA wa Kwamfipa Kata ya Kibaha Mkoani Pwani umeishukuru serikali kwa kuwapatia kiasi cha zaidi ya shilingi milioni 60 kwa ajili ya ujenzi wa Shule ya Sekondari ambayo utawapunguzia changamoto wanafunzi wa Mtaa huo wanaotembea umbali wa Kilometa nane kwenda Shule ya Sekondari ya Simbani.

Hayo yamesemwa Mjini Kibaha na Mwenyekiti wa CCM Kata ya Kibaha Mohamed Muanda alipotembelea kuangalia maendeleo ya ujenzi huo kwani ni ukombozi kwa wanafunzi wanaotoka kwenye Mtaa huo.

Muanda amesema kuwa hicho kilikuwa kilio cha wananchi wa Mtaa huo pamoja na Mtaa wa Mwendapole ambapo Mitaa hiyo miwili ina jumla ya shule tatu za Msingi ambapo wanafunzi wote husoma Shule hiyo ya Simbani ambayo ni ya Kata.

Kwa upande wake Mjumbe wa Serikali ya Mtaa huo Jumanne Mwinshehe amesema kuwa wananchi walijitolea kwa kufanya usafi kabla ya ujenzi kuanza huo ukiwa ni mchango wa wananchi na wataangalia fedha za Halmashauri zitaishia wapi ili wananchi wachangie ambapo ujenzi huo uko hatua ya msingi.

Naye Christina Sabai wanafunzi wanakwenda Sekondari mbali na kwa watoto wa kike ambao hukumbana na changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na kurubuniwa na waendesha pikipiki na kuhatarisha masomo yao kwa kupata ujauzito.

Aidha fundi wa ujenzi wa mradi huo wa Shule hiyo Juma Mabula amesema watatumia siku 75 kukamilisha ujenzi huo kwani vifaa vyote viko hivyo wanaamini watakamilisha kwa muda uliopangwa ili wanafunzi waanze kusoma.

Friday, April 5, 2024

TAASISI YA KUMUOMBEA RAIS NA WASAIDIZI WAKE YAFANYA MAOMBI KUIOMBEA SERIKALI

 

Na Wellu Mtaki, Dodoma

Taasisi ya kumuombea Rais  na wasaidizi wake imefanya maombi ya kuombea viongozi wa serikali akiwemo Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, Spika wa Wabunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Tulia Akson pamoja na Mawaziri na Wabunge. 

Katibu Mkuu wa taasisi hiyo Angelina Malembeka akizungumza na vyombo vya habari mara baada ya maombi hayo amesema lengo ni kuwaombea ili waongoze kwa hekima.

Malembeka amesema kuwa anaamini taasisi hiyo itaweza kusaidia mambo mengi yasiyofaa yasipate nafasi na malengo ya taasisi ni kumuombea Rais  na wasaidizi wake pamoja na wataalamu mbalimbali wanaofanya shughuli za jamiii ndani ya nchi.

"Katika utekelezaji wa miradi mbalimbali na utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) mambo yanaenda vinzuri ila wao wanafanya kazi ya kuombea Ili kuhakikisha utekelezaji unaenda vizuri zaidi,"amesema Malembeka.

Alisema wanaona mambo yanaenda vizuri katika miradi mbalimbali na utekelezaji wa ilani ya CCM na kazi yao ni kuombea viongozi wawe na ujasiri, nguvu na kuwapa matumaini na ikumbukwe kuwa suala hili la kuombea Rais na wasaidizi wake ni suala la muendelezo na kazi yake ni kujenga Taifa lenye hofu ya Mungu.

Aidha amesema kuwa idadi ya wanachama ni zaidi ya wanachama 600 lakini walioshiriki maombi hayo walikuwa ni 208 ambapo wengine hawakuhudhuria kutokana na sababu mbalimbali.


 

Thursday, April 4, 2024

MKUU WA MKOA DODOMA ROSEMARY SENYAMULE AKAGUA MIRADI YA MAENDELEO

Ziara ya kikazi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule, imeendelea Wilayani Kondoa April 3/ 2024 ambapo amefanya ukaguzi wa miradi mbalimbali inayotekelezwa wilayani humo ikiwemo Ujenzi wa Wodi ya wazazi, jengo la Mochwari na jengo la upasuaji katika hospitali ya wilaya ya kondoa.

Aidha amekagua ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule ya sekondari  ya wasichana Kondoa pamoja ukaguzi wa nyumba ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya kondoa mji ambapo ujenzi unaendelea na unatarajia kukamilika muda wowote kwani umefika hatua za umaliziaji ( Finishing).

Hatahivyo Mhe. Senyamule ameendelea kuwahimiza watumishi wa sekta ya afya kuendelea kutunza mazingira yanayozunguka katika vituo vyao ili kuendelea kuweka mazingira safi na ya kuvutia siku zote ikiwemo kupanda miti kwa mpangilio unaofaa.

SIDO YAWATAMBUA WAJASIRIAMALI WATAKIWA KUZALISHA BIDHAA BORA KUKUZA UCHUMI

KATIBU Tawala Mkoa wa Pwani Rashid Mchatta amewataka wajasiriamali  watakiwa kuzingatia uzalishaji wa bidhaa zao kitaalam ili kukuza uchumi wa mkoa huo.

Mchatta ameyasema hayo wakati akikabidhi vyeti vya kwa wajasiriamali wenye viwanda vidogo na vidogo kabisa wa mkoa huo ambao wametambuliwa na Shirika la Viwanda Vidogo Vidogo (SIDO) Mkoa wa Pwani.

Amesema kuwa wajasiamali hao wanapaswa kuzingatia ubora na viwango pia kushirikiana na taasisi zinazothibitisha viwango vya bidhaa ili ipate soko ndani na nje ya nchi.

Aidha ameipongeza SIDO kwa jitihada za kuwawezesha wajasiriamali ambapo Mkoa huo una jumla ya viwanda 1,533 vikubwa 122 vya kati 120 vidogo 274 na vidogo sana 1,117.

Naye Meneja wa SIDO Mkoa wa Pwani Beata Minga amesema kuwa unatambua jitihada za wajasiriamali ambao wameanzisha viwanda ambavyo vitaongeza ajira na kuongeza pato la mwananchi mkoa na Taifa.

Minga amesema kuwa vyeti hivyo vya kuwatambua vitawasaidia pale wanapohitaji kutambuliwa na taasisi nyingine ambazo ni za uwezeshaji na zoezi hilo litakuwa endelevu ambapo jumla ya wajasiriamali 65 wametambuliwa 

Wednesday, April 3, 2024

*MTOTO* *ATOLEWA* *SARAFU KOONI*

Wataalamu katika Idara ya ENT ya Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) wamefanikiwa kuitoa sarafu iliyokuwa imekwama kwenye koo la mtoto mdogo kwa siku sita.

Daktari Bingwa wa Masikio, Pua na Koo wa BMH, Emmerenceana Mahulu, amesema BMH imempokea  mtoto huyo wa miaka miwili siku ya Alhamisi ya tarehe 26, Machi.

"Tumefanikiwa kuitoa sarafu iliyokuwa imekwama kwenye koo la mtoto kwa siku sita kwa kutumia kifaa tiba kinachoitwa _esophagoscopy_," amesema Daktari huyo Bingwa ambaye pia Kaimu Mkuu wa Idara ya ENT ya BMH.

Dkt Mahulu amefafanua kuwa sehemu ya koo ilipokuwa imekwama sarafu  ilisabisha uvimbe, akiongeza kuwa ilikuwa imeacha uwazi kidogo ambayo ilikuwa ikiruhusu vimiminika kama uji, maji juisi kupita.

"Mtoto anaendelea vizuri baada ya matibabu na anaweza kula vizuri kwa sasa. Tumeishamruhusu na tutamuona tena baada ya wiki moja ili kuona maendeleo yake," amesema. 

Kwa mujibu wa mama wa mtoto, Juliana Yuda, mkazi wa kijiji cha Mkoka, Kongwa, Dodoma, mtoto wake, ambaye alitoka kucheza na wenzake siku ya Jumamosi ya  tarehe 20, Machi, alirudi nyumbani muda wa mchana akiwa analia.

"Mtoto alikuwa hawezi kula kwa muda wa siku sita, alikuwa anashindia uji, juisi na maji tu. Hali yake ilizidi kuwa mbaya Siku ya Alhamisi," anasema.

Anaongeza kuwa Alhamisi ya tarehe 26, Machi alimpeleka mtoto Hospitali ya Wilaya ya Kongwa ambapo alipewa rufaa kuja BMH baada ya kupigwa picha ya x-ray na kubaini sarafu imekwama kwenye koo.

Tuesday, April 2, 2024

WAFANYAKAZI OFISI YA RAIS FEDHA MIPANGO ZANZIBAR NA WAFANYAKAZI WIZARA YA FEDHA WASAIDIA WATU MAHITAJI MAALUM




Na Wellu Mtaki, Dodoma

Wafanyakazi Ofisi ya Rais fedha na Mipango Visiwani Zanzibar wakishirikiana na wafanyakazi wa wizara ya fedha wametembelea vituo vinne vya watu wenye mahitaji Maalum.

Vituo hivyo ni kituo cha Safina Street Network, Asmaa Bint Shams, kituo Cha  wasioona watu wazima Buigiri na Shule ya Msingi ya watoto wenye mahitaji maalum Buigiri ikiwa ni muendelezo wa ziara yao kila mwaka kutembelea vituo vya watu wenye maitaji Maalum na kutoa misaada ya chakula na fedha.

Hayo yamesemwa na ofisa Uendeshaji Ofisi ya Rais fedha na mipango Zanzibar Rajab Uweje wakati akizungumza na vyombo vya habari Jijini Dodoma mara baada ya ziara wameweza kutambua  mahitaji mengine ya vituo hivyo na ametoa ahadi awamu zijazo watajitaidi kuhakikisha wanatatua changamoto zao.

"Tumetoa ahadi katika vituo hivi tumechukua changamoto zao tuone awamu ijayo tuje kutatua changamoto tunaondoka hapa tukiwa tunaenda kuongea na viongozi wetu kuwaeleza hali iliyopo huku ili awamu ingine tuje tusaidie kutatua changamoto,"amesema  Uweje.

Pia ametoa wito kwa walezi wa vituo hivyo kuendelea kuwatunza watoto hao  na kuwasimamia  vizuri ili kujenga Taifa  lenye raia wema.

Kwa upande wake mwenyekiti wa Hazina Sports Club Mugusi Musita amesema kuwa upo muhuhimu wa jamii kutambua kusaidia watu wenye maitaji maalum kutokana ha changamoto zilizopo kwenye jamii zao hivyo anaiomba jamii kiujumla kuhakikisha wanakuwa mstari wa mbele kusaidia watoto kwani watoto ndiyo Taifa la kesho.

"Vituo vinamahitaji mengi na makubwa sana   kama viongozi  watambue watoto hawa wanamaitaji sana tumekuja kuwapa chochote ila naona kama havitoshi pia tutachuka nafasi hii kupeleka taarifa za cha changamoto hizi katika Halmashauri ya Chamwino nao waone namna ya kusaidia," amesema Musita.

Naye Mratibu wa  Shirika la Safina Street Network Dodoma Ebeneza Ayo ameiomba jamii kuacha kutoa hela kwa watoto wa mitaani ndiyo inasababisha watoto hao kuendelea  kukaa mitaani kuombaomba bali jamii iendelee kuwapa msaada kwa kuwasidi kuwapekeka katika vituo vya kulelewa ili waweze kupata msaada pamoja na elimu Ili kusaidia kutengeneza Taifa lenye nguvu kazi.

"Tuwapende hao watoto wanaotoka katika manzingira hatarishi tuwe  tayari kuwasaidia kwa mambo  mbalimbali tunavyokutana nao mitaani tujaribu kuwasaidia  waweze kwenda kwenye vituo au ofisi ustawi wa jamii na sio kuwapa hela kwani ukiwapa hela ndiyo wanazidi kukaa mitaani , lakini pia hata sisi wenye mashirika ya kuwasaidia watoto tunachangamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa maji katika kituo chetu hivyo tunaomba jamii iweze kutusaidia,"amesema Ayo.

Mwenyekiti wa Makazi ya watu wasioona Buigiri  Yaledi Daudi ameiomba serikali kuwasaidia kujenga maeneo yao ya Makazi kutokana na nyumba zao kuwa chakavu ili waweze kuishi maisha bora.

"Kwa upande wa serikali tunamshukuru  sana Rais Samia kwa kazi nzuri anayofanya na natoa wito kwa serikali kuwa nyumba zetu tunazoishi zimekuwa chakavu tunaomba serikali itujengee nyumba ili kuwa na maisha bora,"amesema Daudi

Ikumbukwe kuwa ziara hizi hufanyika kila mwaka ikiwa na lengo la kuwasaidia watu waishio manzingira magumu pamoja na watu wenye uhitaji mbalimbali, ziara hizi ufanyika katika maeneo ya visiwani Zanzibar na Bara kwa awamu tofauti tofauti.

Sunday, March 31, 2024

KANISA LATAKIWA KUWEKEZA KWA WANAWAKE





Na Wellu Mtaki,Dodoma.

Askofu wa Kanisa Anglikana Dayosisi ya Central Tanganyika Dodoma Dr. Dickson Chilongani  amewataka wahumini wa kanisa hilo kuwekeza nguvu kazi kwa wanawake kwani ukiwekeza kwa mwanamke unakuwa umenufaika.

Kauli hiyo ameitoa Leo Tarehe 31 March 2024 Katika kanisa la Dayosisi Central Tanganyika Dodoma wakati akilihubiria kanisa  kuhusu habari za yesu kristo Mleta Mageuzi pamoja na kueleza habari za kuwekeza Mwanamke kuharakisha Maendeleo.

Amesema kuwa lazima mkubali kwamba ukiwekeza kwa mwanamke mwisho wa yote inalipa ila kwa wanaume inaweza isikulipe na ifikiapo wakati unawaitaji wanaweza usiwaone kwenye itaji lako.

"Wekeza kwa wanawake: Harakisha maendeleo.” Kwa kauli mbiu hii wanawake walitaka watambuliwe na waaminiwe zaidi kuwa wanaweza. Na hapa tena siku ya pasaka tunawaona wanawake wakiwa mstari wa mbele. Saa 12 Alfajiri wakati wanaume bado wanachapa usingizi, Mariamu Magdalene, Mariamu mamaye Yakobo na Salome wanakwenda kaburini na manukato ya thamani ili kuupaka mwili wa Yesu. Wanafanya hivi kwavile Yesu aliposulubiwa, sabato ilikuwa inakaribia na kwahiyo mazishi yalikuwa ni ya haraka haraka, hawakuwa na muda wa kuuandaa mwili wake kwa maziko" Amesema Chilongani.

"Kwahiyo saa 9 mchana Yesu anapokata roho, wanaoshuhudia kifo chake ni wanawake. Inapofika jioni, Yesu anapozikwa, wanaoshuhudia kaburi na mazishi yake ni wanawake. Wanaume wameingia mitini" amesema Chilongani

Aidha amehisihi jamii kuwe na usawa ambao utasaidia kumuwesesha mwanamke kujiamini Katika kujikomboa  kimaisha kwani kumekuwa na mageuzi makubwa sana kwa wanawake na hii ndio inahashiria wanawake wanaweza kuongoza .

"Haya ni mageuzi makubwa sana, kwavile wakati huu wa Yesu Israeli ilikuwa ni nchi yenye mfumo dume na ukilitimba uliokithiri kwelikweli dhidi ya wanawake. Mwanamke alikuwa si kitu. Ndio sababu hata katika Yohana 6 tunasoma kwamba Yesu alilisha watu 5000 kwa samaki 2 na mikate 5. Lakini waliohesabiwa walikuwa ni wanaume peke yao, wanawake hawakuhesabiwa. Ni kana kwamba walikuwa si binadamu. " Amesema Chilongani

Pia amesisitiza wahumini wa kanisa hilo watambue kuwa mwanamke ni mtekekezaji mzuri wa majukumu na hanahakikisha anafanya kazi kwa weledi bali wapo watu ambao awana imani naye na hao ndio wanapelekea kushusha uchumi wa mwanamke kiujumla.

"Na hata katika mahakama za Israeli ushahidi wa mwanamke kisheria ulikuwa haukubaliki. Lakini bado Yesu anawafanya wanawake kuwa mashahidi wa kufufuka kwake na anawatuma wawaambie wanafunzi wake waende Galilaya watamkuta" amesema Chilongani.

Aidha amewataka wahumini wamtangulize Mungu Katika maitaji ya maombi Yao na waachane na tabia ya kupanga aina ya maitaji wanayoyataka kwa Mungu Bali wamwache Mungu atatenda mwenyewe.

"Ni lazima tujifunze kumtanguliza Yesu Kristo na siyo kumtangulia. Askofu Mkuu mstaafu marehemu John Ramadhani aliwahi kusema: “Wakristo wengi badala ya kumtanguliza Roho Mtakatifu wanamtangulia”. Mtu badala ya kumwomba Mungu ampe mke mwema, anampa Mungu masharti kwamba anataka mke mweupe tena mwenye mwanya. Huko ni kumtangulia Mungu. Badala ya kuomba gari, anaomba Scania, wakati hata baiskeli yenyewe hana. Huko ni kumtangulia Mungu. Kumtanguliza Mungu ni kumwomba mke au gari na kuacha mapenzi yake mema yatimizwe" amesema Chilongani 

Pia  hamewahimiza wanawake kuwania nafasi mbalimbali za uongozi Katika ngazi ya kanisa na serikali kwa ujumla na kuzingatia usawa wa kijinsia.

"Somo linatutaka tuwaamini wanawake na tuthamini mchango wao katika kanisa na jamii. Katika kanisa mwaka huu Dayosisi yetu ina mkutano mkuu (sinodi), na tumeanza chaguzi mbalimbali katika ngazi zote. Ningeomba sana kuwe na usawa. Zisiwepo nafasi za wanaume peke yao na za wanawake peke yao" amesema Chilongani 

"Katika taifa, chaguzi pia zimeanza kufanyika kuelekea kwenye uchaguzi mkuu. Ni vyema kuwe na usawa, tuwaamini wanawake. Kubwa zaidi, kumekuweko na baadhi ya wanaume wanaomzodoa Rais Samia kana kwamba hawezi lolote kwasababu tu ni mwanamke. Ni kana kwamba hawaoni kazi ambazo Rais wetu amezifanya katika kipindi chake hiki kifupi cha uongozi. Watu wa jinsi hii ni wabinafsi na hawatufai katika jamii" amesema Chilongani 

Kanisa Kuu la Roho Mtakatifu ni kanisa la Kiuaskofu katika Dayosisi ya Central Tanganyika. Dayosisi ya Central Tanganyika ilianzishwa mwaka 1927. Ilikatwa kutoka Dayosisi ya Mombasa. Kabla ya hapo Kenya, Uganda, Tanzania, Rwanda, Burundi na DRC Congoeneo lote hili lilikuwa chini ya umisheni wa CMS Afrika na kujulikana kama Dayosisi ya Eastern Equatorial Africa na Askofu wa kwanza alikuwa James Hannington (1884 – 1885). Huyu alikuwa shahidi wa kwanza baada ya kuuwawa na Kabaka Mwanga katika eneo la Busuga nchini Uganda 29/10/1885.