Saturday, August 19, 2023

MNEC HAMOUD JUMAA ATAKA SUALA LA BANDARI RAIS ASISEMWE VIBAYA





MJUMBE wa Halmashauri Kuu Taifa (NEC) Hamoud Jumaa amevitaka baadhi ya vyama vya upinzani nchi kuacha kumsema vibaya Rais Dk Samia Suluhu Hassan kuhusu suala la mkataba wa Bandari badala yake watoe ushauri.

Jumaa aliyasema hayo Kata ya Mtambani Mlandizi Kibaha alipokuwa mgeni rasmi kwenye uzinduzi wa operesheni ya kuanza maandalizi ya uchaguzi ngazi ya serikali za vijini yenye kauli mbiu ya Simika Bendera.

Alisema kuwa anawashangaa wapinzani kutoa maneno mabaya kwa Rais kuhusu mkataba wa Bandari ambapo walipaswa kutoa ushauri na si kumsema vibaya.

"Suala la mkataba wa bandari ni jambo la msingi na Rais yuko makini na mkataba huo ili kuongeza mapato ya nchi na kama wao wanaona kuna jambo basi washauri na siyo kutoa maneno yasiyofaa,"alisema Jumaa.

Aidha alisema kuwa wanamshukuru Rais kwani ameonyesha uvumilivu mkubwa licha ya kusakamwa kuhusu suala la bandari ambalo mchakato wake bado unaendelea.

"Tumechoka kusikia Rais anasemwa vibaya yule ni kiongozi hivyo lazima aheshimiwe ila tunampongeza kwa ustaamilivu anaouonyesha kwani hawajibu licha ya kusemwa vibaya,"alisema Jumaa.

Aliwataka viongozi kuwajali viongozi wa ngazi za chini hususani mabalozi na viongozi wa mashina kwani wao ndiyo wako karibu na wanachama kwani ili kushinda uchaguzi kwani ndiyo malengo ya chama chochote.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Said Kanusu alisema kuwa anashangazwa na watu kutoa maneno kuwa eti bandari imeuzwa wapinzani wameishiwa hoja.

Kanusu alisema kuwa wananchi wawe na imani na wasikatishwe tamaa na wanaoleta hoja zisizo na msingi ajenda ya nchi ni kuleta maendeleo na miradi.

Naye Diwani wa Kata ya Mtambani Godfrey Mwafulilwa alisema kuwa kauli mbiu hiyo ni kuimarisha ngazi ya chini ya mabalozi kuwapa nguvu kwani wanakazi kubwa kukiimairisha chama.

Mwafulilwa alisema kuwa ngazi ya msingi sana ni balozi ambapo chama kinarudi chini ambako huko ndiko kwenye wanachama na hoja za wanachama na wananchi.

Alisema kuwa Rais ni mvumilivu na hawavutiwi na tabia inayofanywa na watu wanamchafua wao wanapaswa kuja na hoja na ushauri ila siyo kumchafua.

JUKWAA LA WAZALENDO HURU TANZANIA KUUNGA MKONO ROYAL TOUR


JUKWAA la Wazalendo Huru Tanzania Mkoa wa Pwani katika kuunga jitihada za Rais Dk Samia Suluhu Hassan kutangaza utalii inatarajia kufanya ziara Visiwani Zanzibar kutembelea vivutio vya utalii.

Akizungumza na waandishi wa Habari Mjini Kibaha mwenyekiti wa Taasisi hiyo Hadija Juma alisema kuwa hiyo ni sehemu mojawapo ya kuunga mkono jitihada za serikali kwa vitendo.

Juma alisema kuwa utalii ni moja ya vyanzo vikuu vya pato la Taifa hivyo wameona waihamasishe jamii kutembelea vivutio vilivyopo ikiwa ni utalii wa ndani.

Kwa upande wake katibu wa taasisi hiyo Hawa Cheka alisema kuwa lengo lao ni kuelezea mafanikio ya serikali kwenye nyanja mbalimbali za kiafya, kielimu, kisiasa, kijamii na kiuchumi.

Cheka alisema kuwa mbali ya malengo hayo pia ni kuwafanya Watanzania kuwa Wazalendo, kuwa waadilifu, kuheshimu mila na desturi na kujitolea kwenye shughuli za maendeleo.

Friday, August 18, 2023

SERIKALI YATOA BILIONI 12 UJENZI VITUO VIDOGO KUSAMBAZA BIDHAA ZA PETROLI NA DIZELI VIJIJINI

 

Serikali imetoa billion 12 kwa ajili ya mradi wa kuwezesha ujenzi wa vituo vidogo vya kusambaza bidhaa za Petroli na Diseli vijijini Tanzania bara kwa lengo la kulinda Mazingira na Afya ya watumiaji na kuboresha upatikanaji na Usambazaji wa Mafuta vijijini.

Mkurugenzi Mkuu Wa Wakala wa Nishati Vijiini REA Mhandisi Hassan Said amesema hayo leo Jijini Dodoma katika Mkutano na waandishi wa habari akisema usambazaji wa mradi huo  unahusu kuwekeza ujenzi wa vituo vidogo vya mafuta katika maeneo mbalimbali Vijiini.

Said amesema kuwa moja ya changamoto inayosababisha wananchi wasitumie nishati safi na kuendelea kutumia nishati ya asili yaani mkaa na kuni ni pamoja na upatikanaji wake kwani nishati asilia zimekua zikipatikana kwa urahisi.

Aidha amesema Wakala umeanza kutekeleza Mradi wa kusambaza mitungi ya gesi ya kupikia kwa utaratibu wa utoaji ruzuku kuwezesha usambazaji wa mitungi ya gesi ya kupikia (LPG) 71,000  yenye thamani ya shilingi bilioni 3 pamoja na majiko banifu 200,000  (laki mbili) katika maeneo ya vijijini huku kwa mwaka wa fedha 2023/24 jumla ya fedha  takribani bilioni 10 zimetengwa kwaajili ya kufanikisha mradi huo.

Pia ametoa rai kwa Watanzania kutumia mafundi wanaotambulika na Shirika la Umeme Tanzania ( TANESCO) kuondoa lawama zinazotolewa na wananchi dhidi ya Serikali zinazosababishwa vishoka wanaofanya uunganishaji wa umeme kinyume cha sheria.

Serikali imetoa jumla ya shilingi trillioni 1.7 kwa Wakala wa Nishati Vijiini (REA) kwaajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali  ya nishati nchini.

Kadhalika Serikali kupitia REA kwa kushirikiana na Benki ya Dunia (WB) imetenga Dola za Kimarekani milioni 6 kwa ajili ya mradi wa usambazaji wa majiko banifu ya kupikia.

DKT KIJAJI AWATAKA WAFANYABIASHARA KUJENGA MIUNDOMBINU YA UWEKEZAJI

 


Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Ashatu Kachwamba Kijaji amewataka wafanyabiashara wa Mkoa wa Dodoma kuchangamkia fursa zinazojitokeza kwa kujenga miundombinu wezeshi kwa wawekezaji na wageni  kwani baada ya Serikali kuhamia Jijini Dodoma kumekuwa na ongezeko la wageni kutoka sehemu mbalimbali Duniani.

Kijaji ameyasema hayo leo Agosti 17, 2023 wakati wa Kikao kazi na wafanyabiashara wa Jiji la Dodoma katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Jengo la Mkapa ambapo kikao hicho kimewahusisha wajasiriamali na wafanyabiashara pamoja na majukwaa yanayojihusisha na ujasiriamali. 

Waziri Kijaji amesema uchumi imara wa Taifa upo mikononi wa sekta binafsi hivyo amewahimiza wafanyabiashara hao kutumia fursa zote zinazojitokeza  iwe ni sekta binafsi au kutoka serikalini ili kuendelea kukuza uchumi wa nchi. 

Waziri Kijaji amewahimiza wajasiriamali kuwa waaminifu na Fedha zinazotolewa na Serikali kama sehemu ya mtaji ili kuwawezesha na wengine kupata hiyo fursa. 

"Lazima tukubaliane na utaratibu uliowekwa uadilifu wetu, uaminifu wetu ni muhimu hakuna fedha za bure sehemu yeyote lazima uwe na uhakika wa fedha kurudi  na mtu unae mpatia fedha hivyo tunatakiwa kumthibitishia Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama alivyo mtetezi wetu namba moja "ameeleza Kijaji

Kwa Upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule akitoa salamu za Mkoa amempongeza Waziri huyo kwa kukutana na kuzungumza na wafanyabiashara hao pamoja na kutatua changamoto na kero  zilizokuwa kikwazo katika utekelezaji wa biashara zao.

Senyamule amesema Mkoa wa Dodoma upo tayari kupokea wawekezaji na kuongeza idadi ya viwanda ili kuongeza na kukuza mapato ya Serikali na uchumi wa nchi ya Tanzania.

Thursday, August 17, 2023

KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA ARDHI, MALIASILI NA UTALII YARIDHISHWA NA UTENDAJI WA TFS


Kamati ya Kudumu ya  Ardhi, Maliasili na Utalii imeridhishwa na utendaji kazi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kwa kuendelea kusimamia vyema rasilimali za misitu.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Mhe. Timotheo Mnzava (Mb) ameyasema hayo leo katika kikao cha Kamati hiyo kilichofanyika ukumbi wa Utawala Annex Bungeni jijini Dodoma.

Mhe. Mnzava amewapongeza wahifadhi kwa kujitolea kufanya kazi kwa bidii.

"Tuwatie moyo hawa wapiganaji wetu kwani wameendelea kutekeleza majukumu yao vyema na kuhakikisha kila kitu kinaenda sawa, waendelee kuitumikia nchi kwa kuwa wanajitolea na sisi kama Bunge tunawaunga mkono" Mhe. Mnzava amesisitiza. 

Aidha, ameitaka Wizara ya Maliasili na Utalii kufanyia kazi mapendekezo ya wajumbe wa Kamati hiyo na kuangalia namna bora ya kuzuia ukataji wa miti kwa kuwa yapo maeneo ambayo wananchi wanaishi kwa kutegemea miti hiyo .

Naye, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) ameishukuru kamati hiyo kwa mapendekezo na kuahidi Serikali itafanyia kazi.

Pia, amefafanua kuwa Serikali inaendelea kuhamasisha wananchi kuacha kukata miti hovyo pamoja na kuacha matumizi ya nishati chafu na badala yake kutumia nishati safi.

Kikao hicho kimehudhuriwa na baadhi ya Watendaji kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii na Wakala ya Huduma za Misitu Tanzania (TFS).

Wednesday, August 16, 2023

WAGONJWA ZAIDI YA 500 WA MTOTO WA JICHO MBARALI KUFANYIWA UPASUAJI BILA MALIPO

 

Na. Majid Abdulkarim, Mbarali 

Wagonjwa zaidi ya 500 wenye matatizo ya mtoto wa jicho wanatarajiwa kupatiwa huduma ya upasuaji wa mtoto wa jicho  kutoka kwa madaktari bingwa wa macho ambao wameweka kambi ya wiki moja katika Wilaya ya  Mbarali Mkoani Mbeya.

Hayo yamebainishwa leo na Mkuu wa Wilaya ya Mbarali, Mhe. Kanali Dennis Mwila wakati wa uzinduzi rasmi wa kambi ya matibabu ya upasuaji wa mtoto wa jicho itakayodumu kwa muda wa siku saba Wilayani hapo.

Kambi hiyo ilianza Agosti 14 mwaka huu na inatarajiwa kumalizika Agosti 20 mwaka huu, ambapo wakazi wa Wilaya hiyo wanaendelea kupata nafasi ya kufanyiwa uchunguzi na kupatiwa matibabu ya upasuaji wa mtoto wa jicho.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kambi hiyo, Kanali Mwila amesema kulingana na taarifa ya Shirika la Afya Duniani (WHO) asilimia Moja ya watu wanapata matatizo ya macho.

Aidha, Kanali Mwila amelipongeza Shirika la Kimataifa la Helen Killer kwa kuanza kampeni ya kutokomeza magonjwa ya macho Juni 2022 ambapo wametoa vifaa vyenye thamani ya Sh: Mil. 140 kwa Mkoa wa Mbeya na walitoa mafunzo kwa watumishi wa Afya ngazi ya jamii wapatao 570.

“Juni, 2022 Shirika la Helen Killer liliweza kugundua wagonjwa 1,750 ambao walikuwa na tatizo la mtoto wa jicho  kwa awamu tatu tofauti”, ameeleza Kanali Mwila.

Amesema, katika kambi hiyo inayoendelea jumla ya watu 500 wanatarajiwa kupatiwa huduma ambapo zaidi ya kiasi cha Sh:  Mil. 110 kitatumika katika kuwapatia huduma ya upasuaji wa mtoto wa jicho.

Amesema, kwa mwaka jana (2022) wagonjwa 29,000 waliyo onwa katika Mkoa Mbeya, wagonjwa 3,406 walikuwa na tatizo la mtoto wa jicho na magonjwa mengine.

Vile vile, Kanali Mwila ameipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan  kwa kuwa imara katika kuwasogezea huduma za Afya karibu.

Naye, Meneja Mpango wa Taifa wa Macho kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Bernadetha Shilio amesema kuwa mbinu inayotumika kuwapata wagonjwa  ni kupitia wahudumu ngazi ya jamii ambao wanaambatana na wataalamu wa Afya nyumba kwa nyumba na kuwabaini wagonjwa.

Dkt. Shilio amesisitiza kuwa Huduma za upasuaji katika kambi hiyo ya siku saba katika Hospitali ya Wilaya ya Mbarali zinatolewa bila malipo chini ya ufadhili wa Shilika la Kimataifa la Helen Killer.  

Kwa upande wake Mwakilishi wa Mratibu wa Macho kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI, Ernest Paul amesema Serikali itahakikisha inawezesha upatikanaji wa huduma za macho karibu na wananchi hususani ngazi ya msingi.

BODI YA MKONGE NCHINI IMESAMBAZA MICHE MILIONI 6.9 BURE KWA WAKULIMA WADOGO


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.Samia Suluhu Hassan amedhamiria kufanya mageuzi katika kilimo cha Mkonge Kwa kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kusambaza miche 6,991,200 ya mbegu za mkonge bure kwa wakulima wadogo katika Wilaya 16 nchini.

Mageuzi hayo yamefanya Tanzania kuwa Nchi ya pili Duniani kwa kuzalisha mkonge ikitanguliwa na Brazili.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Mkonge Tanzania Saddy Kambona wakati akizugumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa majukumu wa bodi hiyo na mwelekeo katika mwaka huu wa fedha 2023/24.

Kambona ametaja Wilaya zilizopatiwa mbegu hizo ni Korogwe, Muheza, Tanga, Mkinga, Handeni, Kilindi, Rorya, Bunda, Butiama, bariadi, Bagamoyo, Kisarawe, Mkuranga, Manyoni, Singida Vijijini na Mkalama.

Amesema Rais Dk.Samia ametoa fedha kwa ajili ya kununua mitambo mipya ya kuchakata Mkonge na kufufua mitambo ya kuchakata mkonge ya mashamba ya Kibaranga Wilayani Muheza, Tanga na shamba la serikali la TPL lililopo Kata ya Bwawani Wilayani Arumeru, Arusha ambalo linasimamiwa na kuendeshwa na TSB.

Aidha,Kambona amesema Serikali iliongeza lengo na kuiagiza Bodi ya Mkonge Tanzania kuhakikisha kuwa uzalishaji unaongezeka hadi kufikia tani 120,000 kwa Mwaka, ifikapo Mwaka 2025/2026.