Friday, June 9, 2023

HALMASHAURI ZATAKIWA KUTENGA BAJETI ZA MICHEZO


HALMASHAURI za Mkoa wa Pwani zimetakiwa kutenga bajeti kwa ajili ya shughuli za michezo ili kuinua vipaji vya vijana kwenye michezo.

Hayo yalisemwa Mjini Kibaha na Katibu Tawala wa Mkoa huo Rashid Mchata wakati akifunga mashindano Umoja wa Michezo na Sanaa kwa Shule za Sekondari Tanzania (UMISSETA) Mkoa wa Pwani.

Mchata alisema kuwa mbali ya bajeti pia Halmashauri zihakikishe kila shule inatenga eneo kwa ajili ya michezo ili wanafunzi wapate sehemu ya kucheza.

Naye ofisa michezo wa mkoa huo Grace Bureta alisema kuwa jumla ya wachezaji 120 wamechaguliwa kuunda timu ya  Mkoa ambayo itashiriki mashindano ya Taifa yatakayofanyika  mkoani Tabora ambapo timu hiyo imeiingia kambini kwenye shule ya sekondari Kibaha.

Naye mdau wa michezo Musa Mansour alisema kuwa kwa kuwa michezo ni ajira wadhamini waangalie kwa kuboresha upande wa zawadi ili ziwe kivutio kwa vijana kushiriki michezo.

Thursday, June 8, 2023

WAKAZI CHANGWAHELA WARIDHIA KUHAMA


WAKAZI wa Kitongoji Changwahela wilayani Bagamoyo wameridhia kutekeleza agizo la Serikali la kuondoka katika eneo walilolivamia na kufanya shughuli za kibinadamu na kufanya uharibifu wa mazingira.

Akizungumza na wananchi kwenye Kitongoji hicho na kutoa maagizo hayo ya serikali akiwa katika kushughulikia changamoto zinazotokana na migogoro ya ardhi Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge amesema kuwa kuna uharibifu mkubwa umefanywa na wananchi hao ikiwemo ukataji wa  mikoko ambayo inatunza kingo za bahari na kuhifadhi mazingira ya fukwe na mazalia ya samaki.

Kunenge amesema kuwa maagizo hayo ni utekelezaji wa maamuzi yaliyofanywa na baraza la Mawaziri kufuatia ushauri wa timu ya mawaziri nane wa kisekta iliyoundwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan mwaka 2019/2020 ambao walishirikiana na wataalamu kushughulikia migogoro ya ardhi mkoani humo na maeneo mengi nchini.

Akiwa Wilayani Bagamoyo alifika katika Kitongoji cha Sanzale Kata ya Magomeni na aliwaelekeza wakazi waliyovamia eneo la Yusuph Kikwete kupisha ili mwenyewe aweze kuendelea na shughuli za uwekezaji au wakae nae na kukubaliana watakavyoona inafaa.

Wakati huo huo ametoa muda wa siku 90 kwa Halmashauri ya Chalinze Wilaya ya Bagamoyo kukamilisha  zoezi la urasimishaji makazi kwa ajili ya mpango wa matumizi bora ya ardhi kwa wananchi wa waliopewa eneo la hekari 5,520 za Ranchi ya Taifa ya Ruvu.

Wednesday, June 7, 2023

WANANCHI WA SANZALE WALIOSHINDWA MAHAKAMANI WAZUNGUMZE NA MMILIKI


KUFUATIA hukumu iliyotolewa na Baraza la Ardhi na Nyumba Kibaha kuwa wavamizi 86 kwenye eneo linalomilikiwa na Yusuph Kikwete waondoke Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge amewataka wananchi hao kuongea na mmiliki huyo ili waangalie namna ya kuwasaidia.

Kunenge ameyasema hayo kwenye Kitongoji cha Sanzale kata ya Magomeni wilaya ya Bagamoyo kufuatia wananchi hao kumwomba ashughulikie suala hilo kwenye ziara ya kutatua kero za wananchi kwenye mkoa huo ambapo amesema suala hilo ni amri ya mahakama na ni la kisheria na limeamuliwa kwa kufuata sheria.

Amesema suala la kisheria haliwezi kuingiliwa kwani walalamikaji walipaswa kufuata taratibu za kisheria kama waliona kuwa maamuzi yaliyotolewa hawakuridhika nayo ikiwa ni pamoja na kukata rufaa ndani ya siku 45 baada ya hukumu ambapo hawakufanya hivyo njia pekee ni kukaa na mmiliki huyo ili aangalie namna ya kuwasaidia.

Aidha amesema kutokana na maamuzi hayo ya kumpa ushindi mmiliki huyo tayari dalali ameshapatikana ili kuondoa watu hao kwenye kitalu namba D kwenye viwanja namba 14 hadi 25 ambapo kumejengwa nyumba 47, nyumba ambazo hazijakamilika 13, maboma 14 na vibanda 12.




CHANGWAHELA WATAKIWA KUPISHA ENEO KWA AJILI YA HIFADHI YA MIKOKO

HALMASHAURI ya Bagamoyo imetakiwa kukaa na mwekezaji wa Sea Salt ili kutoa hekari 50 kwa wananchi wa Kitongoji cha Changwahela kata ya Mapinga wilaya ya Bagamoyo ambao wameondolewa kwenye eneo ambalo ni la uhifadhi wa Mikoko.

Akitoa taarifa ya Mawaziri nane wa kisekta ambao walitembelea eneo hilo ambalo ni la mikoko lilikuwa mgogoro wa ardhi na mwekezaji huyo alikuwa na eneo lenye ukubwa wa hekari 600 ambazo nyingine hakuziendeleza na kutakiwa azitoe kwa wananchi hao, Mkuu wa mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge amesema nyumba 90 ndizo zitapewa hekari hizo.

Kunenge amesema maamuzi ya baraza la mawaziri lilitoa maamuzi hayo baada ya kulitembelea na kuona jinsi lilivyofanyiwa uharibifu wa mikoko ambayo ni kingo ya bahari na mazalia ya samaki hivyo Halmashauri wakae na mwekezaji wajadili kutoa hekari 50 kwa ajili ya wananchi hao ambao walijenga nyumba za makuti.

Amesema eneo hilo litasimamiwa na Wakala wa Huduma za Misitu TFS ambapo litabaki kwa ajili ya uhifadhi na siyo kwa ajili ya shughuli za kibinadamu.

SERIKALI YATOA MAAMUZI UENDESHAJI MAGOFU YA KAOLE BAGAMOYO

KUNENGE akiwa Bagamoyo alimuagiza Kamishna Msaidizi wa Ardhi kufuta hati ya upimaji   eneo la Mji Mkongwe uliofanyika ndani   ya eneo la hifadhi kwa kuwa zilitolewa ndani ya GN namba 1983  na kutatua mgogoro wa ardhi eneo la magofu ya Kaole na familia ya Omary Sherdel.

Alimtaka kamishna msaidizi wa ardhi wa mkoa kukamilisha ufuatiliajj kwenye mamlaka husika juu ya sheria namba 64 na 10 na maboresho ya mwaka 1976.

"Kumekuwa na uvamizi kwenye magofu na malikale na watu hawafuati utaratibu ambapo kumekuwa na mgogoro wa magofu ya Kaole na kuna marekebisho ya sheria namba 10 ya mwaka 1964 na maboresho namba 20 ya mwaka 1979 na kanuni zake kuweka ulazima wa majengo yote yenye zaidi ya miaka 100 yawe chini ya umiliki wa serikali badala ya mtu binafsi,"alisema Kunenge.

Aliongeza kuwa TFS ikusanye mapato ya mali kale kwenye mahoteli au nyumba za kulala wageni na marekebisho ya Gn namba 49 ya mwakab1973 baada ya kumega eneo la hekari 24.7 lililotolewa kwa wananchi.

KITONGOJI CHA KAJANJO KIJIJI CHA SAADANI CHATENGEWA HEKARI 50

Katika hatua nyingine akiwa Kijiji cha Saadani  Kunenge ameagiza leseni ya kampuni ya Sea Salt kupunguza eneo la hekari 50 kati ya 2,000 zinazomilikiwa na kampuni hiyo litagawiwa kwa ajili ya wananchi wa Kitongoji cha Kajanjo.

Alisema eneo hilo la hekari 50 wamepewa wakazi wa kitongoji hicho ambapo kimevunjwa ambapo kuna kaya 17 ambazo zilikuwa hapo na kuongezeka na kufika 120 pia makambi ya muda 72 ambayo wanajihusisha na uvunaji mikoko waondoke kwenye hifadhi ya mikoko.

"Hifadhi ya Saadani SANAPA ilipe kiasi cha shilingi milioni 287 kwa ajili ya mashamba na maendelezo kwa kaya 17 pia kamishna msaidizi wa ardhi abadilishe hati ya eneo la Sea Salt kwa kupunguziwa hekari 50 na mmiliki huyo alinde mipaka yake na watu wasiingie tena kwenye eneo hilo,"alisema Kunenge.

Alimtaka Kamshna Msaidizi wa Ardhi kufuta hati ya mmiliki wa sasa wa East Africa Resort kwa kuwa zipo ndani ya hifadhi na haijaendelezwa na kumtaka Mkurugenzi wa Halmshauri ya Chalinze kufuta kitongoji cha Kajanjo na kuhakisha wananchi wanahamishiwa kwenye hekari hizo 50.

WALIOVAMIA RAZABA WATAKIWA KUONDOKA


KUFUATIA wananchi zaidi ya 5,000 kuvamia eneo la Ranchi ya Zanzibar Bagamoyo (RAZABA) kwenye Kata ya Makurunge Halmashauri ya Bagamoyo serikali imewataka wananchi hao kuondoka na kuikabidhi Wakala wa Usimamizi wa Misitu Tanzania (TFS) kulisimamia eneo hilo.

Hayo yalisemwa na Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge wakati wa ziara yake kwenye maeneo  ya Saadani, (RAZABA) na Mji Mkongwe Bagamoyo na kutoa matamko ya utekelezaji wa maamuzi ya Baraza la Mawaziri kuhusu Migogoro ya matumizi ya Ardhi Mkoani  Pwani.

Kunenge alisema kuwa maamuzi ya kuwaondoa wananchi hao yametokana na serikali baada ys kushughulikia migogoro ya ardhi ambapo Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aliunda timu ya Mawaziri nane wa kisekta iliyoshirikiana na timu ya wataalam  na kufika katika maeneno mbalimbali likiwemo la RAZABA na kutoa mapendekezo ambayo yaliridhiwa na baraza la Mawaziri kwa utekelezaji.

"Shamba hilo lilikuwa ranchi ya Mifugo ambayo ilitolewa na serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, eneo hili lilikuwa na ukubwa wa hekari 28,097 ambazo ziligawanywa katika shamba namba 364,365/1 na 365/2 Makurunge,"alisema Kunenge.

Alisema kufuatia maagizo hayo aliwataka wananchi waliovamia eneo hilo la RAZABA kuondoka kwa sababu ni mali ya serikali na kuanzia sasa eneo hilo litakuwa chini ya usimamizi wa Wakala wa Usimamizi wa Misitu Tanzania (TFS).