Wednesday, June 7, 2023

WALIOVAMIA RAZABA WATAKIWA KUONDOKA


KUFUATIA wananchi zaidi ya 5,000 kuvamia eneo la Ranchi ya Zanzibar Bagamoyo (RAZABA) kwenye Kata ya Makurunge Halmashauri ya Bagamoyo serikali imewataka wananchi hao kuondoka na kuikabidhi Wakala wa Usimamizi wa Misitu Tanzania (TFS) kulisimamia eneo hilo.

Hayo yalisemwa na Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge wakati wa ziara yake kwenye maeneo  ya Saadani, (RAZABA) na Mji Mkongwe Bagamoyo na kutoa matamko ya utekelezaji wa maamuzi ya Baraza la Mawaziri kuhusu Migogoro ya matumizi ya Ardhi Mkoani  Pwani.

Kunenge alisema kuwa maamuzi ya kuwaondoa wananchi hao yametokana na serikali baada ys kushughulikia migogoro ya ardhi ambapo Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aliunda timu ya Mawaziri nane wa kisekta iliyoshirikiana na timu ya wataalam  na kufika katika maeneno mbalimbali likiwemo la RAZABA na kutoa mapendekezo ambayo yaliridhiwa na baraza la Mawaziri kwa utekelezaji.

"Shamba hilo lilikuwa ranchi ya Mifugo ambayo ilitolewa na serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, eneo hili lilikuwa na ukubwa wa hekari 28,097 ambazo ziligawanywa katika shamba namba 364,365/1 na 365/2 Makurunge,"alisema Kunenge.

Alisema kufuatia maagizo hayo aliwataka wananchi waliovamia eneo hilo la RAZABA kuondoka kwa sababu ni mali ya serikali na kuanzia sasa eneo hilo litakuwa chini ya usimamizi wa Wakala wa Usimamizi wa Misitu Tanzania (TFS).

No comments:

Post a Comment