WAFANYABIASHARA wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha Mkoani Pwani wametakiwa kuungana ili waweze kupata fursa mbalimbali za kiuchumi zilizopo kwenye Wilaya hiyo.
Hayo yalisemwa Mlandizi Wilayani Kibaha na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT) Mkoa wa Pwani Abdala Ndauka wakati wa mkutano na wafanyabiashara wa Mlandizi.
Ndauka alisema kuwa serikali au wadau wanashindwa kuwafikia wafanyabiashara kutokana na kutokuwa na umoja lakini wakijiunga kwenye umoja ni rahisi kunufaika.
"Serikali haifanyi kazi na mtu mmoja bali inawapa fursa watu kutokana na makundi hivyo ili wafanyabiashara wa Halmashauri hiyo wanufaike na fursa hizo lazima waungane,"alisema Ndauka.
Alisema kuwa Jumuiya ya wafanyabiashara Halmashauri hiyo ilikuwepo lakini ilivunjika hivyo wafanyabiashara walikosa fursa nyingi lakini nia waliyoionesha ya kurudi itawasaidia sana.
"Mnapoungana mnakuwa na sauti moja hivyo ni rahisi kusikilizwa tofauti na mfanyabiashara anapolalamika peke yake pia inasaidia kupata haki zao na kupunguza vitendo vya rushwa na serikali kupata mapato,"alisema Ndauka.
Aidha alisema kuwa na wafanyabiashara hao hawapaswi kuchanganya siasa na biashara kwani inasababisha mgawanyiko baina yao na siasa wawaachie wanasiasa.
Kwa upande wake mratibu wa mkutano huo Majuto Ngozi alisema kuwa wanamshukuru mwenyekiti wa kutoa elimu kwa wafanyabiashara juu ya umuhimu wa kuungana.
Ngozi alisema wataendelea na mchakato ili kuunda Jumuiya yao kwa kutoa elimu kwa wafanyabiashara wengi zaidi ili kuwa na utaratibu mzuri na kufanya uchaguzi wa viongozi ili kupata uongozi imara.
Naye moja ya wafanyabiashara Fihiri Msangi ambaye ni moja ya wanachana wa Jumuiya hiyo alisema kuwa amepata manufaa makubwa ikiwa ni pamoja na kupata fursa ya kutembelea maeneo mbalimbali ya kibiashara.
Msangi alisema kuwa ameweza kupata pasi ya kusafiria kupitia Jumuiya hivyo kuwa na urahisi wa kwenda nje ya nchi kwa ajili ya kutafuta fursa nje ya nchi.
Katika mkutano huo wafanyabiashara hao walikubaliana kuunda Jumuiya hiyo lakini wapewe elimu juu ya faida za Jumuiya ili wapate uelewa wa pamoja ambapo waliomba wapewe katiba ili waone miongozo ya Jumuiya hiyo.
No comments:
Post a Comment