Wednesday, June 7, 2023

WANANCHI WA SANZALE WALIOSHINDWA MAHAKAMANI WAZUNGUMZE NA MMILIKI


KUFUATIA hukumu iliyotolewa na Baraza la Ardhi na Nyumba Kibaha kuwa wavamizi 86 kwenye eneo linalomilikiwa na Yusuph Kikwete waondoke Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge amewataka wananchi hao kuongea na mmiliki huyo ili waangalie namna ya kuwasaidia.

Kunenge ameyasema hayo kwenye Kitongoji cha Sanzale kata ya Magomeni wilaya ya Bagamoyo kufuatia wananchi hao kumwomba ashughulikie suala hilo kwenye ziara ya kutatua kero za wananchi kwenye mkoa huo ambapo amesema suala hilo ni amri ya mahakama na ni la kisheria na limeamuliwa kwa kufuata sheria.

Amesema suala la kisheria haliwezi kuingiliwa kwani walalamikaji walipaswa kufuata taratibu za kisheria kama waliona kuwa maamuzi yaliyotolewa hawakuridhika nayo ikiwa ni pamoja na kukata rufaa ndani ya siku 45 baada ya hukumu ambapo hawakufanya hivyo njia pekee ni kukaa na mmiliki huyo ili aangalie namna ya kuwasaidia.

Aidha amesema kutokana na maamuzi hayo ya kumpa ushindi mmiliki huyo tayari dalali ameshapatikana ili kuondoa watu hao kwenye kitalu namba D kwenye viwanja namba 14 hadi 25 ambapo kumejengwa nyumba 47, nyumba ambazo hazijakamilika 13, maboma 14 na vibanda 12.




No comments:

Post a Comment