SERIKALI imewaagiza wananchi zaidi ya 5,000 waliyovamia na kuishi katika Ranchi ya Zanzibar Bagamoyo (RAZABA) kuondoka na kuikabidhi Wakala wa Usimamizi wa Misitu Tanzania (TFS) kulisimamia eneo hilo.
Agizo hilo limetolewa leo Juni 6, 2023 na Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge wakati wa Ziara yake eneo la Saadani na (RAZABA) na Mji Mkongwe Bagamoyo ya kutoa matamko ya Utekelezaji wa Maamuzi ya Baraza la Mawaziri kuhusu Migogoro ya Matumizi ya Ardhi Mkoani Pwani.
Kunenge amesema maamuzi ya kuwaondoa wananchi hao yametokana na serikali kushughulikia migogoro ya ardhi ambapo Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aliunda timu ya Mawaziri wanane wa kisekta iliyoshirikiana na timu ya wataalam na kufika katika maeneno mbalimbali likiwemo la RAZABA na kutoa mapendekezo ambayo yaliridhiwa na baraza la Mawaziri kwa utekelezaji.
"Shamba hilo lilikuwa ranchi ya Mifugo ambayo ilitolewa na serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, eneo hili lilikuwa na ukubwa wa hekari 28,097 ambazo ziligawanywa katika shamba namba 364,365/1 na 365/2 Makurunge,"amesema Kunenge.
“Naagiza wananchi wa eneo hili la RAZABA kuondoka mara moja kwa sababu ni mali ya serikali na kuanzia sasa lipo chini ya usimamizi wa Wakala wa Usimamizi wa Misitu Tanzania TFS,” amesema Kunenge.
Katika hatua nyingine akiwa Kijiji cha Saadani Kunenge ameagiza leseni ya kampuni ya Sea Salt kupunguza eneo la hekari 50 kati ya 2,000 zinazomilikiwa na kampuni hiyo ambalo litagawiwa kwa ajili ya wananchi wa Kitongoji cha Kajanjo.
Amemtaka Kamshna Msaidizi wa Ardhi kufuta hati ya mmiliki wa sasa wa East Africa Resort kwa kuwa zipo ndani ya hifadhi na hakijaendelezwa.
Aidha amemtaka Mkurugenzi wa Halmshauri ya Chalinze kufuta kitongoji cha Kajanjo na kuhakisha Wananchi wanahamishiwa kwenye hekari hizo 50.
Pia amemuagiza Kamishna Msaidizi wa Ardhi, kufuta hati ya upimaji eneo la Mji Mkongwe, uliofanyika ndani ya eneo la hifadhi kwa kuwa zilitolewa ndani ya GN namba 1983 na kutatua mgogoro wa ardhi eneo la magofu ya Kaole na Familia ya Omary Sherdel.
No comments:
Post a Comment