Thursday, June 8, 2023

WAKAZI CHANGWAHELA WARIDHIA KUHAMA


WAKAZI wa Kitongoji Changwahela wilayani Bagamoyo wameridhia kutekeleza agizo la Serikali la kuondoka katika eneo walilolivamia na kufanya shughuli za kibinadamu na kufanya uharibifu wa mazingira.

Akizungumza na wananchi kwenye Kitongoji hicho na kutoa maagizo hayo ya serikali akiwa katika kushughulikia changamoto zinazotokana na migogoro ya ardhi Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge amesema kuwa kuna uharibifu mkubwa umefanywa na wananchi hao ikiwemo ukataji wa  mikoko ambayo inatunza kingo za bahari na kuhifadhi mazingira ya fukwe na mazalia ya samaki.

Kunenge amesema kuwa maagizo hayo ni utekelezaji wa maamuzi yaliyofanywa na baraza la Mawaziri kufuatia ushauri wa timu ya mawaziri nane wa kisekta iliyoundwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan mwaka 2019/2020 ambao walishirikiana na wataalamu kushughulikia migogoro ya ardhi mkoani humo na maeneo mengi nchini.

Akiwa Wilayani Bagamoyo alifika katika Kitongoji cha Sanzale Kata ya Magomeni na aliwaelekeza wakazi waliyovamia eneo la Yusuph Kikwete kupisha ili mwenyewe aweze kuendelea na shughuli za uwekezaji au wakae nae na kukubaliana watakavyoona inafaa.

Wakati huo huo ametoa muda wa siku 90 kwa Halmashauri ya Chalinze Wilaya ya Bagamoyo kukamilisha  zoezi la urasimishaji makazi kwa ajili ya mpango wa matumizi bora ya ardhi kwa wananchi wa waliopewa eneo la hekari 5,520 za Ranchi ya Taifa ya Ruvu.

No comments:

Post a Comment