KITUO cha Msaada wa Kisheria Kibaha (KPC) kimeishauri serikali kudhibiti vibanda vinavyoonyesha video maarufu kama vibanda umiza ambapo baadhi ya watoto chini ya miaka 18 kufanyiwa vitendo vya ukatili.
Aidha kimeshauri wazazi kuwa makini na kuwapatia watoto wao simu ambapo baadhi wamekuwa wakizitumia vibaya kujifunza mambo yasiyofaa.
Akifundisha somo la Ndoa kwa viongozi wa Mita na Kata ya Visiga mwezeshaji kutoka (KPC) Humphrey Munuo alisema kuwa baadhi ya mabanda hayo yamekuwa yakionyesha video mbaya ambazo zinasababisha watoto kujifunza vitendo viovu vikiwemo vya ngono.
Alisema kuwa baadhi ya watu wakubwa wamekuwa wakiwarubuni watoto hao kwa kuwalipia kuingia kwenye mabanda hayo na kuwafanyia vitendo vya ubakaji.
"Serikali ifanye ufuatiliaji wa mabanda hayo picha zinazoonyeshwa na pia iwafuatilie baadhi ya watu wanaowafanyia watoto vitendo vya ubakaji ambapo vitendo hivyo hufanyika kupitia mabanda hayo,"alisema Munuo.
Aliongeza kuwa pia iangalie maudhui yanayoonyeshwa kwenye mabanda hayo kwani inavyoonekana baadhi ya tabia watoto wanajifunza kupitia kwenye mabanda hayo pamoja na Play Station.
"Juu ya Tehama wazazi wawe makini kwa watoto wao ambao ni wanafunzi kuwapatia simu kwani baaadhi ya picha au video hazina maadili mazuri hali inayosababisha mmomonyoko wa maadili",alisema Munuo.
Alibainisha kuwa digitali ni nzuri lakini lazima wazazi wawe makini na matumizi hayo kwa watoto wao ili wasijiingize kwenye vitendo vibaya na kuharibu maisha yao.
No comments:
Post a Comment