WALIMU wanawake 300 kutoka Chama Cha Walimu Tanzania (CWT) Wilaya ya Kibaha Mkoani Pwani wanatarajia kukutana kwenye Kongamano la ujasiriamali ambalo litafanyika mwezi Agosti mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari Mjini Kibaha Mwenyekiti wa CWT kitengo cha wanawake Rose Nyambweta alisema kuwa wameamua kuandaa kongamano hilo ili walimu hao wajifunze masuala ya ujasiriamali.
Nyambweta alisema kuwa kwenye kongamano hilo kutakuwa na vitu mbalimbali ambavyo walimu hao watafundishwa masomo ya ujasiriamali na masuala ya fedha ikiwa ni pamoja na kujiwekea akiba na ukopaji wa fedha usio na madhara.
"Kongamano hilo litakuwa na wataalamu wa mafunzo hayo ya ujasiriamali ikiwemo wa kutengeneza batiki, sabuni za vipande, vikoi na sabuni za maji ni vitu vya kijasiriamali ili wauze waongeze kipato chao,"alisema Nyambweta.
Kwa upande wake Katibu wa CWT Wilaya ya Kibaha Kitengo cha Wanawake Florence Ambonisye alisema kuwa kutokana na walimu kuwa na mahitaji makubwa wamejikuta wakiingia kwenye mikopo umiza maarufu kama kausha damu na mingineyo lakini ujadiriamali unaweza ukawaondoa kwenye mikopo hiyo inayowaumiza.
Naye Katibu wa CWT Wilaya ya Kibaha John Kigongo ambaye pia ni mjumbe alisema kuwa mara baada ya mafunzo hayo walimu hao wanawake wataunda vikundi vya ujasiriamali ambavyo vitawezeshwa ili vifanye uzalishaji.
No comments:
Post a Comment