Monday, March 6, 2023

WANAWAKE WATUMIE MITANDAO KUFIKIA USAWA WA KIJINSIA

Na Mwandishi Wetu Dodoma

WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt Doroth Gwajima  amewataka wanawake wahakikishe wanatumia huduma za mitandao ili kufikia usawa wa kijinsia kwenye maendeleo kwa kupata taarifa mbalimbali za kijamii kama Afya, Elimu, Kilimo, biashara na zinginezo.

Gwajima ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dodoma kuhusu maadhimisho ya siku ya wanawake duniani yatakayofanyika March 8 mwaka huu.

Amesema kuwa  pengo la wanawake kumiliki simu na kutumia Mtandao linaongezeka zaidi kwa wanawake wenye umri  mkubwa ( wazee) , wanawake wanaoishi vijinini, pamoja na wanawake wenye ulemavu Mwaka 2022 takwimu zinaonesha asilimia 63 ya wanawake duniani walitumia Mtandao ukilinganisha na asilimia 69 ya wanaume.

Aidha amesema kuwa kwa kushirikiana na jamii yenyewe serikali itaendelea kuelimisha na kufanyia kazi kuondoka vikwazo vyote vinavyozuia mwanamke kutumia Teknolojia ya kidigitali.

Pia ametoa wito kwa wanawake na jamii kwa ujumla kujitokeza kuadhimisha sikukuu ya wanawake duniani chini ya uongozi wa waheshimiwa Wakuu wa Mikoa na ameimiza wanawake kujiunga na majukwaa ya uwezeshaji wanawake kiuchumi yaliyo ngazi zote Hadi vijinini Ili kunufaika na uwezeshaji wa serikali na wadau wake.

Sunday, March 5, 2023

WATATU WAFA AJALINI WAMO ASKARI POLISI WAWILI

WATU watatu wakiwemo askari wawili wa Wilaya ya Kipolisi Chalinze Mkoa wa Pwani wamefariki dunia huku mmoja akijeruhiwa baada ya gari dogo walilokuwa wakisafiria kuacha njia na kupinduka.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Mjini Kibaha Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani ACP Pius Lutumo alisema kuwa watu hao walifariki papo hapo.

Lutumo alisema kuwa tukio hilo lilitokea mnamo Machi 5 mwaka huu majira ya saa 11:45 alfajiri huko maeneo ya Mavi ya Ng'ombe Kijiji cha Mboga Kata ya Msoga Tarafa ya Chalinze katika Barabara ya Chalinze/Segera.

"Gari lenye namba za usajili T 323 BAL aina ya Toyota Cresta likiendeshwa na mkaguzi msaidizi wa Polisi Ndwanga Dastani (28) askari wa kituo cha Polisi Chalinze akitokea Chalinze kuelekea Lugoba liliacha njia kutoka upande wa kushoto wa barabara na kwenda upande wa kulia na kugonga kalavati kisha kupinduka na kusababisha vifo vya watu watatu na mmoja kujeruhiwa,"alisema Lutumo.

Aliwataja askari waliokufa kuwa ni Mkaguzi msaidizi wa Polisi Ndwanga Dastani (28) aliyekuwa dereva wa gari hilo, Konstebo  Emmiliana Charles (26) wote askari wa kituo cha Polisi Chalinze na Karimu Simba (27) ambaye ni karani wa Mahakama ya Wilaya Lugoba.

"Majeruhi huyo ambaye naye  ni askari wa Kituo cha Polisi Chalinze Konstebo Mwanaidi Shabani (25) ameumia maeneo mbalimbali ya mwili wake na amepelekwa katika Hospital ya Taifa ya Muhimbili kwa matibabu zaidi,"alisema Lutumo.

Aidha alisema kuwa uchunguzi wa awali umeweza kubaini kuwa chanzo cha ajali hiyo ni mwendokasi na dereva kushindwa kulimudu gari na kupinduka.

"Miili ya marehemu imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti katika Hospitali ya Lugoba kwa ajili ya kusubiri taratibu za mazishi,"alisema Lutumo.

Thursday, March 2, 2023

WATAKA KUHARAKISHWA UJENZI NYUMBA YA MKURUGENZI NA WAKUU WA IDARA

MADIWANI wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha wametaka kuharakishwa ujenzi wa nyumba ya Mkurugenzi na wakuu wa Idara kwani imepita muda mrefu ujenzi huo bado haujaanza.

Wakizungumza kwenye kikao cha baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo walisema kuwa kwa kuwa tayari azimio la ujenzi huo limeshapitishwa hakuna sababu ya kuchelewesha ujenzi.

Diwani wa Kata ya Mtambani Godfrey Mwafulilwa alisema kuwa kama hakuna changamoto yoyote ni vema kuanza ujenzi ili watumishi hao wawe na makazi ndani ya Halmashauri.

Mwafulilwa alisema kuwa kama eneo hilo halina mgogoro wowote kwanini ujenzi hauanzi ambapo eneo hilo ni jirani na ilipojengwa hospitali ya Wilaya.

"Tunataka kikao kijacho tupate majibu kuwa ujenzi unaanza lini ili tuweze kuufanya kwa wakati kwani hakuna sababu ya kuchelewesha ujenzi,"alisema Mwafulilwa.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha Erasto Makala alisema kuwa baadhi ya Madiwani walikuwa na hofu kuwa eneo hilo lilikuwa na migogoro.

Makala alisema kuwa eneo hilo lilikuwa na migogoro baadhi ya watu waliibuka na kusema ni lao hivyo kama lina changamoto ni vema wakaelezea ili waweze kujua.

Naye Ofisa Ardhi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha Brown Nziku alisema kuwa eneo hilo zamani lilikuwa likimilikiwa na Taasisi ya Mkonge na kupewa kampuni ya UFC lakini ilifutiwa hati na Rais ambapo watu walilivamia.

Nziku alisema kuwa baada ya kurudishwa serikalini ilikabidhiwa Halmashauri ambapo walipewa hekari 9.5 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya Mkurugenzi na wakuu wa Idara.

Alisema kuwa kwa sasa hatua iliyofikiwa ni ya manunuzi na baada ya hapo ujenzi utaanza mara moja.


NANE WAJERUHIWA AJALI YA BASI LA HAPPY NATION

WATU nane wamejeruhiwa baada ya basi walilokuwa wakisafiria la kampuni ya Happy Nation kutoka Bukoba kwenda Dar es Salaam kuacha njia na kupinduka.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake kamanda wa Polisi Mkoani Pwani ACP Pius Lutumo alisema kuwa basi hilo lilipinduka baada ya kujaribu kulipita gari lililokuwa limesimama.

Lutumo alisema kuwa ajali hiyo ilitokea Februari 2 mwaka huu majira ya 8:30 usiku kwenye Kijiji cha Ruvu Kata ya Vigwaza Wilaya ya Kipolisi Chalinze Bagamoyo.

"Basi hilo lenye namba za usajili T 526 DVJ lilikuwa likiendeshwa na Vincent Mbasha (39) mkazi wa Mbezi Jijini Dar es Salaam na chanzo lilikuwa likilikwepa gari la mizigo aina ya Scania lenye namba T 299 BYF na tela namba T 308 BYF lilikuwa limepata hitilafu na kutoweka alama yoyote kuashiria kuwa kuna gari ndipo dereva huyo wa basi akalikwepa na kupinduka,"alisema Lutumo.

Alisema kuwa basi hilo lilikuwa na abiri 47 ambapo majeruhi wako hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani Tumbi kwa matibabu zaidi ambapo hali zao zinaendelea vizuri. 

Aidha aliwataja majeruhi hao kuwa ni Nuru Mohamed (38), Selimanda Abdala (63), Amina Jumanne (48), Faudhia Ismail (23), Fredina Omary (15) Abtatus Jovin (18), Idat Reman (27) na Aida Suleiman (24).

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge ambaye aliwatembelea majeruhi hao alisema kuwa madereva wanapaswa kuzingatia sheria za usalama barabarani ili kuepusha ajali zisizo za lazima.

Kunenge alisema kuwa alipata taarifa kuwa dereva huyo alitaka kulipita gari hilo upande wa kulia badala ya kushoto ambapo ni uzembe hivyo ni vema wakazingatia sheria.

Naye Mganga mfawidhi wa Tumbi Amani Malima alisema kuwa waliwapokea majeruhi hao ambapo wameumia maeneo mbalimbali ya miili yao na wanaendelea vizuri na matibabu.

Malima alisema kuwa wagonjwa hao wanaendelea na vipimo mbalimbali vikubwa ilikugundua majeruhi hao wameumia kiasi gani.


Wednesday, March 1, 2023

MAOFISA ELIMU KATA,WALIMU WAJENGEWA UWEZO

HALMASHAURI ya Mji Kibaha imeendesha semina ya kuwajengea uwezo maofisa Elimu kata,walimu walimu wa shule za msingi na sekondari juu ya masuala ya VVU/UKIMWI mahala pa kazi kwa lengo la kuondoa unyanyapaa na ukatili wa kijinsia.

Mratibu wa UKIMWI wa Halmashauri ya Mji Kibaha Siwema Cheru amesema semina hiyo ni mwendelezo wa Mafunzo mengine ambayo yamekuwa yakitolewa kwa wadau mbalimbali ili kuondoa vitendo vya unyanyasaji sehemu za kazi na kwamba sasa wamefikiwa waratibu wa Elimu kata na walimu ambao ni wadau wakubwa kwenye jamii na wanakaa na wanafunzi muda mrefu ambao pia ni wahanga


Dr.Mariam Ngaja ameeleza kuwa walimu wakipata uelewa wa semina hiyo wanawajibu wa kuwafundisha wanafunzi wao kuhusu afya ya uzazi kwa Vijana na maradhi yanayoambukizwa kwa njia ya ngono na Elimu ya madawa ya kulevya.


Ngaja ameongeza kuwa semina hiyo ambayo ni utekezaji wa Kawaida wa Idara ni utekelezaji wa mkakati wa nne wa Taifa wa kudhibiti UKIMWI Tanzania hasa kwa wasichana balehe na wanawake Vijana .


Mwalimu Augustine Seso aliyeshiriki semina hiyo ameishukuru Halmashauri kwa kuigharamia na kwamba imewafikia muda muafaka na Sasa wanakwenda kwenye jamii kutimiza lengo la kutoe Elimu ili kuondosha unyanyasaji na ukatili wa kijinsia kwenye jamii.

WATENDAJI KATA WAKABIDHIWA PIKIPIKI

HALMASHAURI ya wilaya ya Kibaha Mkoani Pwani imewapatia Pikipiki watendaji wa Kata tano ili kuondoa changamoto ya kushindwa kuyafikia maeneo ambayo hayafikiki kirahisi.

Akikabidhi Pikipiki hizo kwa watendaji hao wa Kata katika ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha Mbunge wa Kibaha Vijijini Michael Mwakamo amewataka watendaji kuzitumia pikipiki hizo kama ilivyokusudiwa na serikali na siyo kwenda kuzifanya boda boda.

Mwakamo amesema kuwa pikipiki hizo ni kutoka Serikali kuu kwa ajili ya kuondoa changamoto ya usafiri kwa watendaji kata ili kuwarahisishia majukumu yao. 

"Niwasihi watendaji waliopewa pikipiki leo mkazitumie kama ilivyokusudiwa na tusizikute zimebeba abiria mtaani maana siyo nia ya kukabidhiwa bali ni kutekeleza majukumu ya kazi zenu,"amesema Mwakamo.

Amemtaka Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha kuhakikisha wanawasaidia kwenye matengenezo na kuwawekea mafuta pikipiki hizo kwani ni vyombo vya kazi na wasivitumie kama vyombo binafsi. 

Awali Mwakamo aliishukuru Serikali ya awamu ya Sita chini ya Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kutimiza ahadi ya kutoa vitendea Kazi kwa watendaji wa ngazi zote Ili kurahisisha utendaji kazi kwa watumishi wa Umama.Kata zilizopokea pikipiki ni Soga, Magindu, Kwala, Gwata na Dutumi ambazo ni kata zilizopo pembezoni mwa Halmashauri.

WALIMU KUZAWADIWA VIWANJA



KATIKA kuhakikisha wanafunzi wanaomaliza kidato cha nne hawapati sifuri Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Nickson John amesema itatoa viwanja kwa walimu shule zao zitakazofanya vizuri.

Akizungumza kwenye kikao cha wadau wa elimu kwenye Halmashauri ya Mji Kibaha kilichofanyika Kibaha alisema kuwa kuna changamoto katika ufuaulu na masomo ya Sayansi.

John alisema kuwa lengo ni kuondoa asilimia 50 ya wanafunzi ambao wanashindwa kuendelea na masomo kutokana na kutofanya vizuri kwenye mitihani yao ya kumaliza kidato cha nne.

"Tutatoa viwanja kwa walimu ambao watafanya vizuri kwa kuongeza ufaulu ambapo tungetamani kusiwe na daraja sifuri na daraja la nne kwani madaraja haya yanawafanya wasiweze kuendelea na masomo tunataka angalau kuanzia daraja la tatu na kupanda juu,"alisema John.

Alisema kuwa mbali ya kutoa viwanja pia kutakuwa na motisha mbalimbali zitatolewa ikiwemo fedha taslimu kwa walimu watakaofanya vyema na mkazo utawekwa kwenye masomo ya Sayansi ambayo matokeo yake siyo mazuri.

"Pia tunataka Mwalimu anapaswa kuhakikisha mwanafunzi katika somo lake apate alama C na kama atashindwa kufikia hapo itabidi aulizwe changamoto ni nini,"alisema John.

Aliwataka wazazi na wadau wa elimu kushirikiana na shule ili kufanikisha kuondoa sifuri kwenye shule za sekondari zilizokwenye Halmashauri ya Mji Kibaha.

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri Musa Ndomba alisema kuwa uongozi wa shule ukabili changamoto na siyo kulalamika hata kwa mambo yaliyo ndani ya uwezo wao.

Ndomba alisema kuwa watahakikisha mipango na mikakati iliyowekwa wanaitekeleza ili kuondoa matokeo mabaya kwa wanafunzi wanaomaliza elimu ya Sekondari ili kupata wasomi watakaoshiriki kwenye uchumi ikizingatiwa mkoa wa Pwani ni wa viwanda.

Awali ofisa Elimu Halmashauri ya Mji Kibaha Rosemary Msasi alisema kuwa ufaulu kwa wanafunzi wa kidato cha nne kwa kipindi cha miaka mitano 2018 hadi 2022 umeongezeka.

Msasi alisema kuwa ufaulu huo umeongezeka kwa asilimia 7.89 kwa kutoka asilimia 84.4 hadi asilimia 92.2 na ule wa kidato cha sita kutoka asilimia 99.4 hadi asilimia 100.9.

Baadhi ya walimu wakuu ambao shule zao zilifanya vizuri walisema kuwa kikubwa ni ushirikiano uliopo baina ya walimu wazazi na wanafunzi na Halmashauri.

Kikao hicho cha wadau baadhi ya walioshiriki ni pamoja na kamati ya usalama Wilaya, maofisa elimu wa Kata, watendaji wa kata, wakuu wa shule za msingi na sekondari.

Mwisho.