WAZEE Wilayani Kibaha Mkoani Pwani wameiomba Serikali kuwawekea utaratibu wa mikopo ili wajikwamue kiuchumi kama ilivyo kwa makundi yanayonufaika na mikopo ya asilimia 10 ya Halmashauri.
Wamesema serikali imetenga asilimia 10 ya mikopo itokanayo na mapato ya Halmashauri kwa ajili ya makundi ya wanawake vijana na makundi ya watu wenye ulemavu.
Akisoma risala ya wazee Katibu Msaidizi wa Baraza la Ushauri la Wazee Kata ya Sofu Mariam Mchali amesema kuwa wazee wengi wanakabiliwa na hali ngumu ya kiuchumi kwa kuwa na mikopo maalumu itakayowawezesha kujikwamua kiuchumi.
"Na sisi tunaomba tungepewa mikopo kama ilivyo kwa wanawake vijana na watu wenye ulemavu ili wale wenye uwezo wa kufanya biashara na shughuli nyingine za ujasiriamali waweze kujikwamua kiuchumi,"amesema Mchali.
Mchali amesema kuwa licha ya umri mkubwalakini baadhi yao bado wana uwezo wa kufanya shughuli za ujasiriamali hivyo wanastahili kupewa nafasi ya kupata mikopo inayotolewa na Halmashauri ili waweze kujitegemea badala ya kuendelea kutegemea misaada.
"Tunaiomba Serikali kuboresha ustawi wetu kwa kutuwekea utaratibu wa kupata bima za afya bila malipo kwani baadhi yao wanashindwa kumudu gharama za matibabu na kuwa na mahitaji makubwa ya huduma za afya,"amesema Mchali.
Amesema kuwa Serikali iangalie uwezekano wa kuwawekea wazee utaratibu wa kupata bima za afya bila malipo kwa sababu wapo wazee ambao hawana uwezo wa kiuchumi na hawako katika mpango wa TASAF.
"Changamoto nyingine ni upweke inayowakabili wazee waliofiwa na wenza wao pamoja na baadhi ya watoto kuwatelekeza wazazi wao hali inayoongeza ugumu wa maisha kwa wazee wasiokuwa na uwezo wa kujihudumia,"amesema Mchali.
Naye Mwenyekiti wa Baraza la Ushauri la Wazee Mkoa wa Pwani John Kirumbi amesema kuwa mabaraza hayo yameanzishwa kwa mujibu wa sheria na hayahusiani na chama chochote cha siasa bali yana jukumu la kuwasilisha changamoto za wazee na kushirikiana na Serikali kuzitafutia ufumbuzi ikiwa ni pamoja kuandaa utaratibu wa kuwatafuta wanasheria watakaowasaidia wazee wanaodhulumiwa haki zao hususan katika masuala ya ardhi na umiliki wa nyumba.
Kirumbi amesema kuwa mabaraza hayo yana jukumu kubwa la kuwaunganisha wazee na Serikali ili kuhakikisha wanashiriki katika ngazi za maamuzi kuanzia vijiji mitaa kata hadi wilaya na changamoto kubwa ya wazee ni afya na kwa sasa wameanza utaratibu wa kuandaa fomu zitakazotumika kubainisha hali za kiuchumi za wazee ili wajue mahitaji yao na namna ya kuwasaidia pale wanapohitaji msaada.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Sofu Mashaka Mahande amesema kuwa yuko tayari kushirikiana na wazee hao katika kushughulikia changamoto zinazowakabili kwani wazee ni hazina ya maarifa na uzoefu katika jamii hivyo wanapaswa kuheshimiwa kuthaminiwa na kutunzwa kutokana na mchango wao katika malezi na maendeleo ya jamii.
Mahande amesema kuwa yuko tayari kushirikiana na wazee katika kutafuta ufumbuzi wa changamoto zao kwani wazee ni nyenzo muhimu katika jamii wana maarifa na uzoefu mkubwa hivyo wanapaswa kuheshimiwa kuthaminiwa na kulindwa na atahakikisha anasimamia masuala yao ili haki na mahitaji yao yazingatiwe.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Ushauri la Wazee Kata ya Sofu Annie Balisidya amesema lengo la maadhimisho hayo ni kuwakutanisha wazee ili watambuane kufahamiana na kujadili changamoto zinazowakabili kwa pamoja na kuweka mikakati ya kukabiliana nazo.
Balisidya amesema kuwa kata hiyo ina wazee zaidi ya 300 wenye hali tofauti za kiuchumi wakiwemo wenye uwezo mdogo na wasiokuwa na uwezo kabisa na mikusanyiko kama hiyo inawapa nafasi ya kueleza changamoto zao na kujadiliana namna ya kuzitatua kwa kushirikiana na viongozi.
Naye mmoja wa wazee Anna Mwakihaba ameiomba Serikali kurejesha utaratibu wa kuwapatia wazee maziwa na unga wa lishe kwani wengi wanakabiliwa na changamoto za kiafya zinazohitaji lishe bora.
Mwakihaba amesema kuwa wazee wanapokwenda hospitalini hupewa dawa ambazo zinahitaji mtu kupata lishe bora lakini baadhi yao wanashindwa kumudu gharama za lishe kutokana na hali zao za kiuchumi na wazee wengi wanapokwenda hospitalini wanapewa dawa na wanashauriwa kula vizuri kabla ya kuzitumia lakini wakati mwingine hatuna uwezo wa kupata chakula hicho hawana hivyo Serikali iangalie namna ya kuwasaidia kwa maziwa na unga wa lishe.

No comments:
Post a Comment